Na Gidion Mwakanosya Songea
WAKAZI 69 wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Songea kujibu mashitaka mawili ya kushiriki katika mkusanyiko usio wa halali na kuharibu mlango mmoja wa jengo la CCM la Manispaa hiyo wenye thamani wa shilingi 150,000/= na kuchana Bendera moja ya CCM yenye thamani ya shilingi 20,000/=. Ikiwa mali zote ni za thamani ya shillingi 170,000/=.
Katika Mahakama hiyo ambayo ilifurika watu waliofika kusikiliza kesi hiyo upande wa mashitaka ulioongozwa na mwanasheria wa Serikali kanda ya Songea Edison Mwavanda mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Ruvuma Elizabeth Missana ulidai kuwa washitakiwa wote 69 bila uhalali mnamo februari 22 mwaka huu majira ya kuanzia saa za mchana walikusanyika bila kuwa na kibali kwa nia ya kuvunja amani ya inchi .
Mwanasheria wa Serikali Mwavanda alifafanua zaidi Mahakamani kuwa washitakiwa wote siku hiyo wakiwa katika mtaa wa CCM uliopo Manispaa ya Songea pia walivamia jingo la CCM kisha waliubomoa mlango wenye thamani ya shilingi 150,000/= na baadaye waliichua bendela ya CCM ambayo thamani yake ni shilingi 20,000/= na kuichana.
Hata hivyo washitakiwa wote 69 baada ya kusomewa mashitaka yao yote mawili na kesi yao ilihairishwa hadi machi 8 Mwaka huu itakapotajwa tena na washitakiwa 37 wako nje kwa dhamana na washitakiwa wengine 32 wamerudishwa mahabusu baada ya kukosa watu wa kuwadhamini .
Post a Comment