Jeshi la polisi mkoani Ruvuma limewatia mbaroni watu wawili wakazi wa eneo la Mkuzo katika halmashauri ya manispaa ya Songea ambao wana uhusiahano wa kimapenzi kwa tuhuma za kumuua mtoto mdogo wa jinsia ya kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu kwa madai kuwa mtoto huyo amekuwa akikwakosesha starehe zao za kimapenzi pale wanapohitaji kukutana.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa mbili na nusu asubuhi huko katika eneo la Mkuzo ambako inadaiwa kuwa mtoto huyo aliuwawa kwa kunyongwa shingo na watuhumiwa ambao aliwataja kuwa ni Jema Msemwa (19) na Yohana Njelekela (22) wote wakazi wa Mkuzo.
Alifafanua kuwa inadaiwa kuwa mei 29 mwaka huu majira ya saa za asubuhi huko katika kituo cha polisi cha mjini Songea ilipokelewa taarifa kuwa kuna binti mmoja aliyefahamika kwa jina la Jema mkazi wa Mkuzo ambaye alikuwa na mtoto mdogo wa kike aitwae Rebeca Cheni (1.3) alikuwa amefika nyumbani kwa dada yake akiwa hana mtoto jambo ambalo lilipelekea kuanza kuwa na mashaka naye.
Alisema kuwa Jema baada ya kuulizwa na dada yake kuhusu mtoto ndipo alijibu kuwa amemuacha kwa mpenzi wake aliyemtaja kwa jina moja la Hamisi ambaye alidai kuwa anaishi eneo la Luwawasi, hivyo kwa kushirikiana na mume wa huyo dada yake walimlazimisha Jema waende kwa Hamis kumchukua mtoto. Lakini wakiwa njiani kabla hawajafika Jema alibadili maelezo yake na kusema kuwa hajui alikomuacha mtoto wake ndipo dada yake alipoamua kumfikisha katika kituo cha polisi ili waweze kupata msaada zaidi wa kubaini mahali alikomuacha mtoto.
Alibainisha zaidi kuwa Jema alipofikishwa katika kituo cha polisi alihojiwa kwa kina zaidi ndipo alipoeleza kuwa mei 27 mwaka huu akiwa ametokea Njombe huku akiwa na mtoto wake na siku iliyofuata majira ya saa saba mchana aliondoka nyumbani kwa dada yake na kuelekea kwa mpenzi wake aliyemtaja kwa jina moja la Hamisi ambako alidai kuwa anaenda kulala.
Alieleza zaidi kuwa Jema baada ya kufika huko walishauriana na mpenzi wake watoke kwa matembezi na ilipofika majira ya saa moja usiku walirudi nyumbani kwa Hamisi ndipo Jema aliulizwa na mpenzi wake Hamisi kuwa mtoto huyo hatembei wakati ana umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu, na Jema alimjibu kuwa hata yeye mpaka sasa jambo hilo linamsikitisha.
Kamanda Kamhanda alisema kuwa baada ya maelezo hayo inadaiwa kuwa Hamisi alikasirika na hatimaye alimweleza Jema kwakuwa mtoto huyo si wa kumzaa yeye lazima amuue ili amuoe Jema ili waendelee kuishi vizuri zaidi jambo ambalo Jema hakukubaliana nalo na alitoka nje ya nyumba na kumwacha mtoto akiwa amelala kitandani kwenye chumba cha Hamisi.
Alisema Jema aliporudi ndani ya chumba hicho alimkuta mtoto wake akiwa anakoroma na baada ya kumuuliza Hamisi kulikoni alimjibu kwa ukali na kumtaka ambebe mtoto wake aondoke, hivyo Jema akamchukua mtoto wake na kuelekea nyumbani kwa dada yake na kabla hajafika nyumbani kwa dada yake Hamisi alimfuata kwa kutumia pikipiki na kumsihi Jema asiende kwa dada yake na badala yake mtoto huyo wakamtupe lakini pia wakiwa njiani majira ya saa nne usiku Jema aligundua kuwa tayari mtoto huyo alikuwa amekwisha fariki Dunia ndipo wote kwa pamoja walielekea eneo la Bombambili mtoni ambako walimficha mtoto huyo kwenye kichaka kwa kumfunika kitenge. Na baada ya tukio hilo Jema na Hamisi walirudi nyumbani kwa Hamisi
Kamanda Kamhanda alisema kuwa mei 29 mwaka huu majira ya saa moja asubuhi, Jema aliondoka nyumbani kwa Hamisi na kuelekea nyumbani kwa dada yake akiwa hana mtoto na alipofika dada yake alimuuliza mtoto yuko wapi na alijibu kuwa mtoto yupo kwa Hamisi jambo ambalo halikuwa la kweli ndipo dada dada yake alifikisha taarifa katika kituo cha polisi ambapo askari walimhoji Jema na alikiri kuwa mtoto wake Rebeca amefariki na alikwenda kuwaonyesha mahali ambapo mwili wa marehemu ulikuwa umefichwa.
Alisema kuwa kwa uchunguzi wa polisi wa awali unaonyesha kuwa mwili wa marehemu Rebeca haukuwa na jeraha lakini shingo yake ilikuwa imelegea na ilionekana kuwa alifariki kutokana na kunyongwa shingo na upelelezi wa kina umebaini kuwa mtuhumiwa aliyejiita Hamisi baada ya kukamatwa mei 30 mwaka huu majira ya saa tisa usiku akiwa amelala nyumbani kwake alifahamika kuwa jina lake halisi ni Yohana Njelekela na siyo Hamisi kama alivyokuwa akimdanganya Jema.
Hata hivyo Kamhanda alisema kuwa polisi inaendelea kufanya upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo na kwamba utakapokamilika watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji linalowakabiri.
Post a Comment