Msafara wa Nape ukiingia katika viwanja vya Mshangano. |
Msafara ukiingia Mshangano |
Nape akisalimiana na viongozi wa chuo kikuu cha St. Augustine - Songea |
Nape akitoa hotuba fupi katika viwanja vya Shule ya Tanga |
Nape akielekea kufungua Tawi la Vijana wa Mshangano |
KATIBU wa itikadi na uenezi na mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi ndugu Nape Moses Nauye amewasili leo katika manispaa ya Songea na kupokelewa kwa shamrashara. Mapokezi ya kiongozi huyo wa kitaifa yamefanyika katika kata ya Shule ya Tanga, tawi la Tanga la Chama cha Mapinduzi lililopo kilometa chache kutoka mjini Songea.
Katika mapokezi hayo yaliyoandamana na vikundi mbalimbali vya burudani wananchi mbalimbali wa manispaa ya Songea walikuwa na shauku ya kuweza kumsikia msemaji mkuu wa chama ambapo alipokelewa kwa maandamo makubwa na kukaribishwa kwenye viwanja vya ofisi za CCM kata ya Tanga kwa burudani ya Lizombe iliyofanywa na wakazi wa kijiji cha Sanko kilichopo manispaa ya Songea pamoja na burudani ya Kioda kutoka Ruvuma.
Wananchi wa kata ya Tanga wameweza kutoa malalamiko yao kuhusiana na kufungwa kwa kiwanda cha kusindika tumbaku kilichopo katika manispaa hiyo ambapo wananchi wameweza kubainisha kuwa kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa wananchi ni kufungwa kwa kiwanda hicho.
Katika kulizungumzia hilo, ndugu Nape Nauye ambaye yupo katika ziara ya kuangalia na kukagua spidi ya maendeleo ambayo ni ahadi za chama cha Mapinduzi kwa wananchi wake na miradi ambayo serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ametoa ahadi na kuiagiza serikali ya chama chake kulifuatilia suala hilo na kutaka baadhi ya watendaji ambao wameshindwa kutekeleza ahadi za serikali wanatakiwa wawapishe na wawachie watendaji ambao wako tayari kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo.
Baada ya kuzungumza na wananchi wa kata ya Tanga, ndugu Nauye alikwenda kuzindua tawi jipya la wanachama wa CCM katika maeneo ya Mshangano. Katika uzinduzi huo ameweza kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na wanachama wa tawi la Mshangano ambao kwa asilimia kubwa wameonekana kuwa ni vijana ambao ni wajasiliamali. Katika kupendezewa na hilo Nauye ameweza kuwaunga mkono vijana hao na kuwapatia kiasi cha shilingi laki tatu kwa ajili ya kuendeleza umoja wao ambapo amewashauri wafungue akaunti benki ili waweze kunufaika na umoja wao katika tawi hilo. Wanachama hao wameahidi kutumia fursa hiyo ili kujipatia kipato zaidi.
Baadaye ndugu Nauye aliweza kukutana na wananchi wa Kata ya Mletele ambapo aliweza kuzungumza nao masuala mbalimbali yahusuyo ujenzi na uimarishaji wa chama cha mapinduzi na wananchi hao wamemuahidi kutomwangusha katika uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika katika kata hiyo kutokana na kufariki kwa diwani wao wa CCM wa kata hiyo. Baada ya kufanya mkutano na wananchi wa kata ya Mletele ndugu Nauye anatarajia kufanya mkutano wa hadhara leo katika viwanja vya Zimanimoto vilivyopo mkabala na uwanja wa mpira wa miguu wa Majimaji kuanzia saa tisa alasiri.
Post a Comment