VURUGU ZASABABISHA WATU WATATU KUFARIKI SONGEA
Na Gideon Mwakanosya,Songea.
WATU
watatu wamefariki dunia na idadi kubwa ya watu wanadaiwa kujeruhiwa
kutokana na hali tete iliyozuka katika mji wa Songea mkoani Ruvuma,
baada ya mamia ya wananchi na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la
yeboyebo, kuandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi na ofisi ya mkuu wa
mkoa huo, wakipinga mauaji ya raia ambayo yameshamiri katika mji huo.
Kufuatia
maandamano hayo kushika kasi katika mji huo, jeshi la polisi
lililazimika kuingilia kati kwa kuanza kupiga mabomu ya machozi na
risasi za moto hewani ikiwa ni lengo la kuwatawanya raia hao wasiendelee
kuleta vurugu.
Wakati
mabomu na risasi hizo zikipigwa, ghasia za hapa na pale zilianza
kujitokeza baadhi ya wananchi wakirusha mawe kuelekea kituo kikuu cha
polisi na wengine wakipaza sauti wakielekeza lawama kwa jeshi hilo
kwamba limeshindwa kudhibiti mauaji hayo.
Vurugu
hizo zimesababisha ofisi za serikali na taasisi binafsi mkoani Ruvuma
kufungwa kwa muda yakiwemo maduka na huduma za kifedha katika mabenki
zimesimama kwa muda.
Huduma
za usafiri katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani nazo zimesimama
huku madereva wa mabasi na abiria wakikimbia kujificha kwa lengo la
kuepukana na mabomu ya machozi na risasi za moto zilizokuwa zikipigwa
hewani.
Matukio
ya mauaji katika mji wa songea yalianza kujitokeza mapema mwezi Novemba
mwaka jana yakiendelea hadi sasa, ambapo kila baada ya siku kadhaa watu
walikuwa wanauawa katika mazingira ya kutatanisha huku miili ya
marehemu ikikutwa imejeruhiwa vibaya.
Watu
tisa wameuawa katika mji huo tokea matukio ya mauaji yaanze kujitokeza
katika mji wa Songea na kwamba watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na
mauaji hayo wanashikiliwa na polisi.
Watuhumiwa
wanaoshikiliwa na jeshi la polisi ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju
(14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa mtaa wa
Lizaboni mjini Songea.
Pamoja
na mambo mengine mpaka habari hizi zinaingia mitamboni Kamanda wa
polisi mkoani Ruvuma hawakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo huku
simu zake zikiwa zimefungwa na askari polisi mjini hapa wakiendelea
kupiga mabomu ya machozi, kwa lengo la kutawanya watu.
Post a Comment