Na, Gideon Mwakanosya,Songea
VURUGU zilizojitokeza wakati wa maandano ya amani ya wananchi wenye
hasira kali katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
zimesababisha hasara kubwa ya mali
zenye thamani ambayo haikufahamika mara moja na kwamba katika sakata hilo Askari Polisi wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi
kwa tuhuma za kuwapiga risasi za moto watu wawili ambao wamefariki kwenye
maandamano hayo
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa hali ya mji kwa sasa hivi ni
tulivu na hatua mbalimbali za kiusalama zinaendelea kuimarishwa ili wananchi
waendelee na shughuli zao za kila siku
Kamuhanda alisema kuwa kwenye vurugu hizo watu 54 walikamatwa na
wamefikishwa Mahakamani kujibu tuhuma za kufanya maandamano bila kibali na
kusababisha uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea na
vitongoji vyake
Alisema kuwa Askari Polisi waliohusika na kupiga risasi raia kwa sasa
wanahojiwa na Jeshi hilo
ili kupata uhalali wa kutumia risasi za moto katika tukio la maandamano
yaliyofanyika jana na kwamba ikidhibitika kuwa walifanya uzembe watachukuliwa
hatua za kisheria
Alieleza zaidi kuwa wananchi wakiwa kwenye maandamano hayo walivamia
Ofisi za Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Songea
na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Vijijini walipiga mawe milango
na kisha kuchoma bendera na kuleta hasara za mali nyingine za chama hicho,
walivamia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma,walivamia Ikulu ndogo walipiga
mawe, walivamia Kituo cha Polisi na kupiga mawe na kuharibu baadhi ya magari ya
wananchi
Alieleza kuwa waandamanaji walirusha mawe hovyo na kuwajeruhi wananchi
wenzao, kufunga barabara kwa kutumia mawe makubwa, magogo na kuchoma mataili
moto ili gari zinazoingia na kutoka nje ya mji zisiweze kuendelea na safari
zake pia waandamanaji walivamia gari la Polisi na kuanza kurusha mawe na
kusababisha Askari waanze kujihami kwa kurusha mabomu ya machozi
Alifafanua kuwa fujo hizo zinadaiwa kuwa zimetokana kwa sababu wananchi
wamekuwa wakilalamikia matukio mfululizo wa mauaji mbalimbali likiwemo la
mwendesha Pikipiki aliyeuawa februari 22 mwaka huu majira ya 2 asubuhi huko
katika eneo la mto Matarawe, kuwa Jeshi la Polisi halichukui hatua ya
kuwadhibiti wauaji hao
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya alisema
kuwa baada ya kutokea matukio hayo ameitisha viongozi wa Serikali za mitaa ya
yote na kuwapa maagizo kuwa kuanzia sasa ulinzi shirikishi unatakiwa kuanza kwa
kasi zaidi na kwamba kama kunawatu wanajihusisha
na mambo ya uhalifu wajisalimishe haraka kwenye vyombo vya dola badala kusubiri
wakamatwe
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amelaani kitendo
kilichotokea juzi ambacho amesema sio cha kawaida hivyo kufuatia tukio hilo
ameunda tume huru ya watu nane ambayo itafanya kazi ya siku saba ya kuchunguza
kwa kina juu ya hali iliyojitokeza juzi mjini Songea na ripoti inapaswa
kuwasilishwa arahamisi ijayo asubuhi ofisini kwake na kwamba hiyo tume
inahusisha vyombo vyote vya dola
Baadhi ya wananchi wameiomba Serikali ichukue hatua za haraka kudhitibi
hali iliyojitokeza juzi ambapo watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na
Polisi wakati wa wenye hasira kali walipokuwa wakipita mitaani kufanya vurugu
huku wakidai kuwa Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya kazi na mwingine kufa
baada ya kutumbukia kwenye shimo na Pikipiki wakati wa vurugu hizo
Wananchi hao ambao ni wakazi wa
maeneo ya Mfaranyaki, Majengo, Bombambili na Mjini ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema
kuwa hali iliyojitokeza juzi haikuwa ya kawaida hivyo ni vyema Serikali
ikatafuta njia muafaka ya kudhibiti chanzo cha vurugu badala ya kujishughulisha
na kuzuia maandamano ya amani ya wananchi na kwamba thamani yake haikuweza
kufahamika mara moja
Post a Comment