JESHI la polisi mkoani Ruvuma linamshikilia mwanamke mmoja Rese Mhule (35) mkazi wa kijiji cha Mavanga kilichopo wilayani Ludewa mkoa mpya wa Njombe kwa tuhuma za kumuua bibi yake mzaa baba yake mzazi kwa kumkata na shoka kichwani na kwenye mguu wa kulia akimtuhumu kuwa ndiye aliyemroga ugonjwa wa kifafa unaomsumbua kwa muda mrefu.
Akizungumza ofisini kwake kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimeki alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1.00 asubuhi huko katika kijiji cha Mahanje kilichopo wilayani Songea ambako bibi kizee mmoja aliyetambulika kwa jina la Ambrosia Mgaya (80) aliuwawa kwa kupigwa na shoka kichwani na kwenye mguuwake wa kulia na mjukuu wake ambaye alikuwa ametoka Mavanga kuja kijijini hapo kumwoona.
Msimeki alifafanua zaidi kuwa inadaiwa siku hiyo kabla ya tukio majira ya saa 11.00 alfajiri mtuhumiwa Rose Mhule alikuwa amefika katika kijiji cha Mahanji nyumbani kwa dada yake Josephine Mhule ambaye ndiye aliyekuwa akiishi na mama yao Ambrosia Mgaya ambaye alikuwa akisumbuliwa na maradhi mbalimbali hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mtu mzima.
Alisema kuwa Rose alipokelewa na dada yake kisha alikaribishwa jikoni ambako aliendelea kuota moto na ilipofika majira ya saa 1:00 asubuhi aliingia kwenye chumba ambacho alikuwa amelala mama yake kwa nia ya kumsalimia na kumjulia hali ya maradhi yake yanayomsumbua lakini baada ya muda si mrefu alisikia akiwa anaendelea kuongea naye chumbani.
Alieleza zaidi kuwa inadaiwa muda mfupi tu kupita kilisika kishindo kizito toka kwenye chumba ambacho alikuwa amelala Ambrosia ndipo Josephina alishtuka na baadae aliingia chumbani ambako alimkuta Rose ameshampiga bibi yake kichwani na kwenye mguu wa kulia kwa kutumia shoka huku chumba hicho kikiwa kimetapakaa damu.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi umeonyesha kuwa mtuhumiwa Rose anaumwa ugonjwa wa kifafa hivyo kwa muda mrefu alikuwa akiamini kuwa bibi yake Ambrosia ndiye aliyemroga ugonjwa huo wa kifafa ambao amekuwa akisumbuliwa nao kwa muda mrefu.
Hata hivyo kamanda Msimeki amewatahadharisa wananchi mkoani Ruvuma na kukemea baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijichukulia sheria mikononi kwa imani za ushirikina na badala yake wanapaswa kuchukua hatua zinazostahili ikiwa ni pamoja na kumjua Mungu ili waondokane na imani potofu kama hizo.
Post a Comment