MTOTO wa umri wa mwaka mmoja na nusu Betisia Nombo mkazi wa kitongoji cha Jangwani kilichopo katika kijiji cha Mbangamao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma amefariki Dunia na wazazi wake wote wawili wamejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao baada ya nyumba yao kuteketea kwa moto.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Desidelit Msimeki alisema kuwa tukio hilo lilitokea June 13 mwaka huu majira ya saa 2 usiku hukuo katika kitongoji cha Jangwani Mbangamao wilayani humo na aliwataja waliojeruhiwa kwa kuungua na moto kuwa ni Sabinus Nombo (34) na Veronica Mapunda (20) wote wakazi wa kitongoji hicho.
Alifafanua zaidi kuwa siku hiyo ya tukio huko katika kitongoji cha Jangwani nyumba moja iliyokuwa imeezekwa kwa nyasi ambayo mmiliki wake ni Nombo iliungua moto wakati Nombo na familia yake wakiwa ndini wanasubiri kwenda kulala.
Alisema kuwa wakati wakiwa wanajiandaa kwenda kulala wakiwa chumbani ghafla kibatari kilichokuwa kinatumika kwenye chumba hicho kililipuka na kuunguza pikipiki aina san lg iliyokuwa ndani ya chumba hicho ambayo ni mali ya Nombo.
Kamanda Msimeki alieleza zaidi kuwa katika tukio hilo Nombo pamojan na mke wake Veronica walijeruhiwa vibaya kwa kuungua moto sehemu mbalimbali za miili yao na kwamba majerehi hao walikimbizwa katika hospitali ya serikali ya wilaya ya Mbinga ambako wamelazwa kwa matibabu zaidi na hali zao bado ni mbaya.
Hata hivyo jeshi lapolisi mkoani humo linaendelea kufanya upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo ili kubaini chanzo cha licha ya kuwa upelelezi wa awali umebaini kuwa moto huo ulisababishwa na kibatari ambacho kinadaiwa kuwa kililipuka na kuanza kuunguza pikipiki.
Post a Comment