MAJIGAMBO
na tambo za viongozi, wagombea na wapambe wa vyama vya siasa viwili
vilivyoshiriki kwenye kampeni za kuwania kiti cha udiwani Kata ya
Lizaboni Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma vimefikia
tamati kwa wananchi kupiga kura kumchagua diwani waliokuwa wanamtaka
Wakati wa kampeni wananchi wa Kata ya Lizaboni walipata fursa ya kusikiliza sera za vyama hivyo ambapo wapigakura hao walihitimisha kwa kufanya uchaguzi wa kiongozi waliyemhitaji aprili mosi mwaka huu na kumfanya aliyekuwa mgombea wa Chadema Alanus Mlongo kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo mdogo umefanyika baada ya Kata hiyo kuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo Ally Said Manya(CCM) pia alikuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye alifariki dunia julai mwaka 2011.
Licha
ya kampeni hizo kutawaliwa na vijembe, malumbano na kauli chafu kati ya
vyama na wagombea, lakini wananchi wa Kata ya hiyo walizingatia sera
zilizoonekana kuwa na tija kwao, ambazo pia zinatekelezeka na kumchagua
kiongozi waliyekuwa wanamtaka kwa njia ya kumpigia kura.
Katika uchaguzi huo wapigakura waliopo kwenye orodha ya kudumu kwenye daftari la wapigakura walikuwa ni 7825
lakini waliopiga kura ni 3315 jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa wakazi
wengi wa Kata hiyo hawakuweza kujitokeza kupiga kura licha ya mgombea
wa Chadema kupata kura 1712 wakati Mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika
Kata hiyo George Oddo Mbunda alipata kura 1579.
Nawapongeza
wananchi wa kata ya Lizaboni waliotimiza wajibu wao wa kikatiba katika
uchaguzi huo na kumpigia kura kiongozi ambaye alionekana kukidhi matakwa
ya wananchi kutokana na sera alizokuwa anazinadi wakati wa kampeni.
Matokea
hayo ni salamu tosha kwa viongozi wa Ccm na wa Serikali kuhusu kupuuza
haki na matakwa ya wananchi huku wakibeza kuwa kelele za mlango
hazimsumbui mwenye nyumba, pamoja na kuwa vijana wengi wanaoshabikia
upinzani hawana shahada za kupigia kura
Hayo
ni matokeo ya mbinu dhaifu za kimkakati zilizokuwa zinafanywa na
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea mjini chini ya
uwenyekiti wa Hemed Dizumba za kuamua kufanya siasa za kihuni katika
kampeni zilizopita na za uchaguzi huu mdogo wa udiwani
Kitendo
chake cha kukataa baadhi ya maoni yaliyo wazi na yaliyojificha
yaliyokuwa yanatolewa na wadau wa chama hicho katika kuhakikisha chama
hicho kinaibuka ushindi katika Kata hiyo ndiko kulikosababisha Chama cha
Chadema kiibuke na ushindi na kuongeza idadi yake ya madiwani na
kufikia nane sasa kupitia chama hicho
Siasa
za kihuni kwa sasa hazitakiwi zitumike katika chama kikongwe kama Ccm
ambacho kimepoteza dira machoni na mioyoni mwa watanzania, hivyo kufanya
kampeni dhaifu zilizogubikwa na kwaya, mashairi, ngonjera na lugha
zilizokosa staha hakuwezi kukivusha chama hicho katika chaguzi
zinazokuja
Katika
wimbi kubwa la ufisadi, ukosefu wa ajira kwa vijana, migomo na
maandamano ya makundi mbalimbali na kila aina ya uchafu ambao Serikali
ya Ccm inatupiwa huwezi kumtegemea hata kwa akili ndogo kiasi gani Lukas
Ngongi, Grayson, Juma Kangala na Hamis Abdalah Ally waweze kuleta
ushindi kwa mgombea yoyote yule ndani ya chama hicho kinachojichimbia
kaburi
Ni
watu ambao hawawezi kujenga hoja zenye mantiki katika kuleta ushindi
stahiki kwasababu popote wanaposimama hawawezi kuzungumza lugha zenye
staha, kueleza mikakati ya ushindi, kujibu hoja kwa mpangilio na kueleza
miradi ambayo inatekelezwa na Serikali ya mtaa na hata ya wilaya katika
maeneo wanayoishi
Kutokana
na tabia zao ambazo zimejaa utata watu wenye akili timamu,hawawezi
kushawishika na maneno yaliyojaa dhihaka, matusi katika jukwaa la
kampeni walilokuwa wanalitumia watu wa Ccm kumnadi mgombea wake George
Oddo na badala yake watu walikuwa wanazibeza kampeni zao kwasababu
zimejaa hadithi tupu
Badala
ya kujikita kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali uliofanywa na
aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo marehemu Said Ally Manya, wao wanahangaika
kutoa ahadi au kumshambulia mtu ambaye hana uhusiano na ugumu wa
kampeni waliokuwa wanaupata katika kampeni hizo
Kitendo
cha uongozi wa Ccm kuwaweka watu hao waliojaa siasa za majitaka ambao
walikataliwa kabla ya kuanza na baada ya kumaliza kampeni hizo ndiko
kulikosababisha fedheha kubwa kwa wananchi kukataa kushabikia chama
hicho wakati wa kampeni zake na mwisho kukataliwa katika uchaguzi huo na
kuonyesha uhai mdogo siku za mbeleni na hasa katika uchaguzi mdogo wa
Mletele
Hakuna
sababu yoyote ya msingi utakayoambiwa na viongozi wa Ccm wilaya ya
Songea mjini na wapambe wao kuhusu anguko kubwa tunalolishuhudia hivi
sasa kwa wapinzani kuchukua kwa kasi ya ajabu uongozi kuanzia serikali
za mitaa na sasa udiwani ambapo madiwani wa upinzania wanaingia kwa kasi
kubwa
Washabiki
wa chama cha Ccm kila siku wanaendelea kuamia upinzani huku waliobaki
huko wakiwa wamekata tamaa kabisa na wengine wakiwasha endiketa ya
kutaka kukimbilia chama hicho ambacho kimejaa majungu na siasa za
kuviziana kila kukicha
Dizumba
na viongozi wenzake wa Ccm wa wilaya na wapambe wao ndio wanaosababisha
anguko la chama hicho katika Wilaya ya Songea mjini, hivyo kama kweli
wanakitakia mema chama hicho
wanapaswa kutambua kuwa utawala wa serikali inayofuata mfumo wa
demokrasia, viongozi hawateuliwi bali huchaguliwa na hatma yao ipo
mikononi mwa wananchi
Tambo
na majigambo yao wanapokuwa kwenye kijiwe cha kisiwa ndui hazitakiacha
chama hicho salama hata kidogo kwa sababu watu wengi wana malalamiko na
majonzi kwa vitu vya ajabu wanavyovifanya ambavyo vitapelekea Ccm Songea
mjini kionekana chama dhaifu cha upinzani kutokana na mwenendo huo
Wanapaswa
kutambua kuwa uchaguzi maana yake ni utaratibu wa kuonesha utashi wa
kile unachokitaka na usichokitaka, ni tendo la kuchagua kitu au mtu kwa
sababu ya sifa nzuri. Ndiyo maana watu hupiga kura kuchagua wawakilishi
wao kwenye vikundi mbalimbali vya kijamii, Halmashauri,bungeni na maeneo mengine
Suala la wagombea kusimama ili wapigiwe kura kamwe haliwezi kuhusishwa na utashi wa kiongozi kwani
wanaohudhuria mikutano ya kampeni ndio wanaopima na kumchagua mtu
anayefaa kuwawakilisha katika Halmashauri, bungeni na sehemu zingine
kusudiwa
Kampeni
ni wakati wa wagombea kunadi sera za vyama vyao kwa wananchi ili wajue
ni kina nani, wa chama kipi wanaofaa kupewa ridhaa ya kuwawakilisha
halmashauri,bungeni au kwingineko hivyo kuwatumia watu ambao toka
wamezaliwa hawajawahi kuongoza hata kikundi cha watu kumi na wakati
mwingine kutoa lugha za ovyo ni kutafuta anguko kubwa katika mizania ya
siasa.
Chama
cha Mapinduzi kinawasemaji wazuri wengi kuanzia ngazi ya shina hadi
Wilaya pia kina madiwani, wabunge ambao wanafahamu kuzungumza na wapiga
kura , hivyo kinapaswa kiwatumie watu hao kwani ni hazina kubwa, kwa
sababu wao kuelezea mazuri ya chama na yale yaliyotekelezwa na Serikali
ya chama wanauwezo mkubwa lakini kimewasahau au kuwadharau watu hao
badala yake kinawaendekeza wahuni katika kuutafutia ushindi chama.
Wakati
wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watu hao walitumika kukipigia kampeni
chama na matokeo yake kata tano zilizopo mjini kabisa kuchukuliwa na
Chama cha Chadema na katika uchaguzi huu mdogo uliofanyika hivi karibuni
watu hao wametumika tena na kusababisha Kata hiyo ichukuliwe na
upinzani.
Katika
kampeni hizo zote zilifanywa kinyume cha makusudio yake kwa sababu
badala ya wapiga debe kunadi sera za vyama vyao, walijikita zaidi kwenye
maisha binafsi ya wagombea na familia zao wakiwachafua na kuwazushia
mambo chungu nzima yasiyowahusu wapiga kura.
Waimbaji wakichukua jukumu la kuishauri na kuidhibiti serikali. Na matokeo yake tunayaona. Tupo tulipo kwa sababu tumejiweka tulipo na kama hatua madhubuti hazitachukuliwa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mletele Manispaa ya Songea yatajitokeza kama yaliyotokea katika uchaguzi wa Lizaboni.
Kwa maneno mengine ninachokisema ni kwamba tunakwama kimaendeleo kwa sababu tunafanya siasa zisizo na akili. Ushahidi wa kauli yangu hii ni kampeni tulizoshuhudia hadi sasa. Tuhuma za kutekwa na kuteswa tumezisikia.tuhuma za rushwa na matusi tumezisikia
Siasa zinazolindwa kwa mtutu wa bunduki haziwezi kuwa siasa zitakazomkomboa mwananchi. Siasa zinazoangalia uwiano wa jinsia badala ya uchangamfu wa ubongo haziwezi kuja na suluhu ya matatizo yetu katika Wilaya ya Songea na mkoa kiujumla
Wakati wengi walioingia katika fani ya siasa wameamua kupumzisha akili zao, wananchi nao wameanza kuwashabikia wanasiasa mithili ya mashabiki wa soka ambao hushabikia timu fulani bila kuwa na sababu za msingi.
Ushabiki wa mpira huwa ni ushabiki kutoka moyoni tu, hakuna mtu anakaa na kufikiria kisha kuamua aipende timu ipi. Ndipo tulipofika na matokeo yake sasa tunayaona na tutaendelea kuyaona.
Matokeo ya ushabiki bila fikra, tumejikuta tuna wanasiasa uchwara wengi na bahati mbaya sana katika fikra zao hizo zilizoshindwa kupevuka wanaendelea kuwa viongozi wetu na wanaoamua mustakabali wa maisha yetu na kesho ya taifa letu.
Siasa
za leo kwanza zinaanzia maslahi binafsi, halafu maslahi ya chama na
labda ndio yanafuata maslahi ya taifa. Na ushahidi wa hili ni tatizo la
rushwa katika chaguzi zetu. Mtu mzima anakubali kumpigia huyu au yule
kura kwa sababu yeye amepewa chochote bila kujali ukubwa au thamani ya
alichopewa
Nachelea
kutoa hitimisho kwamba inabidi tufike mahali tuweke mikakati ya
kuwapima uelewa wale wanaotaka nafasi za uongozi katika ngazi zote.
Lakini mchawi wa yote ni vyama vya siasa. Vyama hivi vina nafasi nzuri
sana ya kuchuja wanaofaa na wasiofaa.
Kutokana
na muktadha huo, anguko la Ccm katika uchaguzi wa udiwani wa Lizaboni
nililitegemea na kama watashindwa kujirekebisha kutokana na hulka zao
basi natarajia anguko kubwa zaidi katika uchaguzi mdogo kata ya Mletele
na chaguzi zingine
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
Post a Comment