Loading...

WANNE WAHOFIWA KUFA MAJI KUTOKANA NA GARI KUSOMBWA NA MAJIChanzo stephanomango.blogspot.com 

NA DUSTAN  NDUNGURU  SONGEA. 


WATU wanne wanahofiwa kufa maji na wengine watatu kunusurika katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji kwenye mto Mnywamaji kijiji cha Ngumbo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo limetokea machi 14 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Ngumbo.

Kamuhanda alisema kuwa gari lenye namba za usajili T492 AWY Landrover 110 lililokuwa likisafiri kutoka Mbinga mjini kuelekea katika kijiji hicho lilisombwa na maji wakati lilipokuwa likivuka katika daraja la mto Mywamaji ndani likiwa na watu saba.

Alifafanua kuwa kujaa kwa maji hayo kulifuatia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na kwamba maji hayo yalikuwa yameambatana na mawe jambo ambalo lilisababisha gari hilo kusukumwa.

Kamuhanda aliwataja wanaohofiwa kufa maji kuwa ni Lukas Mbunda(59) ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nkili,Maiko Due(39) mkazi wa Mbinga mjini na Evangelista Mzili(37) mkazi wa kijiji cha Unango.

Alimtaja mtu wa nne ambaye mwili wake umepatikana ni Aidan Mahundi(19) ambaye ni fundi magari mkazi wa kijiji cha Paradiso na kwamba watu watatu walionusurika ni Mathias Mbunda,Rose Mpombo ambao wamelazwa katika kituo cha afya Nkili na dereva wa gari hilo John Hyera ambaye alitoweka mara baada ya tukio hilo.

Hata hivyo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top