Loading...

Mwanaume afa kwa kuchomwa moto Songea


MTU mmoja wa jinsia ya kiume ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja amekutwa amekufa baada ya kuchomwa moto  na watu wasiofahamika katika eneo ambalo liko jirani na nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina Mkomi Guest House  iliyopo manispaa ya Songea.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Detidelit Msimeki alisema kuwa tukio hilo limetokea juni 27 mwaka huu usiku majira ya saa 2:00 huko katika eneo la nyumba ya kulala wageni ya Mkomi ambako mtu asiyefahamika alikutwa akiwa amechomwa moto  

Alibainisha zaidi inadaiwa siku hiyo ya tukio watu waliokuwa wakipita njiani walimwona mtu huyo akiwa amelala kandokando ya barabara na walipomwangalia alionekana ameungua moto mwili mzima ndipo walipotoa taarifa kituo kikuu cha polisi cha mjini Songea.
Alisema kuwa askari polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walifika mara moja kwenye eneo la tukio ambako waliukuta umati mkubwa wa watu waliofika kushuhudia wakiwawa wameongozana na daktari ambaye baada ya kumfanyia uchunguzi ilibainika kuwa mtu huyo alikuwa amekwisha fariki kutokana na kuchomwa moto sehemu mbalimbali za mwili.

Alieleza zaidi kuwa afisa upelelezi wa makosa ya jinai wa wilaya ya Songea ambaye alikuwa ameongozana  na askari polisi wakiwa kwenye eneo la tukio walimkuta mtu huyo amelazwa kifudifudi huku akiwa amevishwa taili la gari ambalo lilikuwa likiendelea kuwaka moto na wakati huo alikuwa anefungwa kamba miguuni.

Hata hivyo kamanda Msimeki alisema kuwa katika tukio hilo hakuna mtu yoyote anayeshikiliwa na polisi na uchunguzi unaendelea kufanywa kuhusiana na tukio hilo la kinyama na amewaonya wananchi kutojichukulia sheria mkononi mara wanapohisi kuwa kuna mtu amevunja sheria na badala yake watoe taarifa kwenye kituo cha polisi kilicho jirani.
Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top