Waziri wa Elimu na mafunzo ya Ufundi Mh. Dk. Shukuru Kawambwa |
Na Betty Kandonga.
MOJA ya habari iliyoandikwa na gazeti dada la Tanzania Daima Jumapili
wiki hii ilifichua ‘madudu’ yaliyofanyika kupanga washindi wa matokeo
ya darasa la saba, hatua hiyo itaongeza idadi ya wajinga nchini.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alitangaza
kuwa ufaulu umeongezeka, kwa wanafunzi hao kwa mwaka 2012 kwa asilimia
8.8 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2011.
Alisema kuwa alama ya juu ya ufaulu kwa wanafunzi wote ni 234 kati ya
alama 250 ambapo wasichana wamefaulu kwa wingi zaidi kuliko wavulana
kutoka kwenye idadi hiyo ya 865,827 waliofanya mtihani huo.
Hata hivyo, baadhi ya walimu na wazazi wa wanafunzi hao, hawakubaliani
na maelezo ya Kawambwa ya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wakati
alama zilizotumika kuwachagua washindi zilikuwa chini ya kiwango.
Nimeshitushwa na taarifa iliyotolewa na makundi hayo hasa ukizingatia
kuwa vigezo vya utungaji wa mitihani kwa mwaka huu uliibua maswali
lukuki kutoka kwa wadau mbalimbali kwa kuwa somo la hisabati lilionekana
kuwa limewekwa katika mtindo wa kuchagua majibu. Ni wazi kuwa kuna baadhi ya viongozi nchini hawana nia njema na elimu
ya hapa wapo tayari kuona watoto wa maskini wakiendelea kuwa mbumbumbu
huku watoto wao wakipata elimu bora katika shule za kimataifa.
Iwapo serikali imeweka chini alama za viwango vya ufaulu taifa
linalokwenda kuzalishwa ni lile ambalo alitatakiwa kuhoji, kudadisi na
kuchambua masuala mbalimbali yanayofanywa na baadhi ya viongozi wasio
waaminifu. Hawa ni wale wanaofanya ufisadi kupitia mikataba mbalimbali ambayo
haina tija kwa taifa. Kuna mchezo wa kuigiza unaoendelea katika elimu
hapa nchini. Nasema mchezo wa kuigiza kwa kuwa haiwezekani kama kweli wapo
waliofaulu ambao wanaonekana kuwa ni wadanganyifu na kulazimika kupimwa
upya.
Kwanini jahazi letu la elimu linazama kwa kasi? Kwanini serikali
inashusha viwango vya ufaulu, kuna nini nyuma ya suala hili? Je,
serikali haipo tayari kupandisha viwango vya ufaulu ili walau wanafunzi
wengi waweze kujituma na kufanya vizuri? Au tunalazimika kutengeneza takwimu ili mradi tuonekane tunasonga mbele
na tunafanya vizuri katika sekta hiyo? Ni muhimu wadau wa elimu wakakaa
na kulichambua suala hilo kwa kina.
La sivyo tukubali kuongozwa kama bata, wasiwepo wa kuhoji wala
kudadisi jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu. Tukifikia
hatua ya kushindwa kuhoji kutokana na kupewa elimu isiyo na mashiko ni
ishara mbaya kwa kizazi kijacho na itakuwa furaha kwa walio madarakani.
Kwa kuwa wataweza kufanya mambo yao kwa uwazi ikiwa ni pamoja na
kuficha fedha zetu Uswisi wakijua kuwa hakuna atakayeweza kudadisi.
Fedha ambazo zingewekezwa hapa nchini si ajabu zingesaidia kuongeza
vitanda katika hospitali zetu, kuongeza maabara katika shule zote za
kata na hata kusaidia kuwapa mikopo kwa wakati wanafunzi wote wa elimu
ya juu.
Kuna ishara za wazi kuwa walimu wanafahamu mambo yanayoendelea katika
elimu yetu, lakini hawapo tayari kuchukua hatua kwa kuwa serikali
imekuwa ikiwadhalilisha hasa pale wanapodai haki yao ya msingi ikiwa ni
pamoja na malipo ya likizo, uhamisho na hata nyongeza ya mishahara.
Wameamua kukubaliana na hali hiyo wakiamini ndiyo adhabu inayostahili
kupewa Serikali kwani kuna dalili zote zinaashiria kuwa elimu yetu
inachezewa bila sababu za msingi. Kuanzia ngazi ya elimu ya msingi,
sekondari hadi vyuoni mtindo ni huo.
Serikali inajisifu kwa ongezeko la takwimu hawapo tayari kutatua
ongezeko la mbumbumbu ambapo tunaelezwa kuwa pamoja na ufaulu kuongezeka
kuna idadi kubwa ya wasiojua kusoma na kuandika.
Hii ni wazi kuwa elimu yetu inazidi kuporomoka na hakuna aliye
tayari kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo. nini kifanyike sasa?
Hatuna haja ya kuiachia serikali bali tunatakiwa kupigana na adui
ujinga ili kulikomboa taifa letu. Kama wazee wetu waliweza kusimama na
kupigana ili kulikomboa taifa hili, basi sasa ni lazima tuchukue hatua
kwa kila Mtanzania ambaye anaguswa na suala hilo ili kupata taifa lililo
bora. Tusikubaliane na kundi la viongozi wachache wanaotaka kuzalisha ubovu
katika elimu yetu, ambao wanajua wazi kuwa watu wajinga hawana uwezo wa
kuhoji juu ya malipo yanayotakiwa kulipwa Dowans.
Tupate taifa ambalo litahoji juu ya rasilimali za nchi zinazonufaisha
watu wachache, kama ilivyotokea kwa wananchi wa Mtwara ambao walihitaji
kuona gesi yao ikiwanufaisha, ikiwa ni pamoja na kujengewa kiwanda na
vijiji pamoja na maeneo yote ya jirani yakipata umeme kutokana na
rasilimali hiyo. Si kujengwa kwa bomba la gesi ambalo halina tija kwao kwa kuwa wajenzi
wenyewe ni Wachina na wala si Watanzania ambao wanashindwa kufaidika na
ajira ya moja kwa moja.
Wapo wapi wananchi wa Kinyerezi ambao kutwa kucha wanahangaikia fidia
za maeneo yao yaliyotwaliwa kwa ajili ya kupisha mradi huo? Hawa nao
siku moja watakuja kuamka wakisema kuwa bomba hilo liishie sehemu fulani
kwa kuwa wamenyimwa fedha za maeneo yao.
Sitaki kuwashawishi bali ninaiona hatari ya jambo hilo linapoelekea,
kuna hatua za haraka zinazohitaji kuchukuliwa katika suala hilo. Maana
kizazi hicho kinayafanya hayo yote kutokana na elimu bora waliyopata.
Kupatikana kwa elimu bora kutazalisha wataalamu walio na ufahamu wa
kutosha na tutaepukana na ‘vihiyo’, nina hakika viongozi wanajua kile
ambacho wanakipanda katika taifa hili kupitia elimu inayolalamikiwa kuwa
ipo chini ya viwango.
Hata mara moja tusitegemee kuwa tukipanda bangi lazima tutavuna bangi,
huwezi kuvuna mpunga wala miwa. Tunachopanda katika kupitia elimu yetu
wapo wanaokijua hivyo taifa lisitegemee kuzalisha vipaji na wala
tusitarajie makubwa kwa hali yetu ya baadaye.
Inasikitisha kwamba tunafanya mzaha na elimu yetu wakati ambapo tupo
katika ushirikiano wa Afrika Mashariki. Tutakuwa na watoto raia wa aina
gani katika shirikisho hilo iwapo serikali inashindwa kuandaa elimu
bora? Ni wazi kuwa tutakuwa wasindikizaji siku zote.
Hatupaswi kuridhika na hoja hafifu za ujenzi wa madarasa lukuki ya
shule za kata au kuandikishwa kwa idadi kubwa ya watoto katika shule
zetu. Cha muhimu ni kuangalia aina ya elimu inayotolewa katika shule
zetu kuliko vyote. Hii ndiyo rasilimali ya pekee wanayorithi
Post a Comment