MADIWANI kumi kati ya madiwani
ishirini na nane (28) wa halmashauri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
wamemwandikia barua mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa hiyo ya kumtaka
aitishe kikao cha baraza chenye madhumuni ya kutokuwa na imani na mstahiki meya
wa manispaa hiyo Charles Mhagama kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kuchukua gari
la halmashauri lenye namba za usajili
SM 3863 aina ya Toyota Cruiser
alilokabidhiwa kutokana na nafasi yake na kwenda nalo Mbinga kwenye shughuli
zake binafsi ambako gari hilo liliharibika na kuisababishia halmashauri hiyo
kugharimia fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo.
Akizungumza mjini
Songea diwani wa kata ya matarawe (CCM) James Makene alisema kuwa tayari
madiwani kumi wamejiorodhesha majina yao na kuambatanisha barua kwa mkurugenzi
wa manispaa hiyo yenye kumbukumbu namba MD/SO/013 ya tarehe 15.03.2013 ya
kumuomba aandae mkutano maalumu wenye madhumuni ya kutokuwa na imani na meya wa
manispaa hiyo.
Alisema kuwa sababu zilizowafanya
baadhi ya madiwani waone umuhimu wa kuomba mkutano maalumu ni kwamba mstahiki meya
Charles Mhagama inadaiwa kwa muda wote kutumia nafasi yake vibaya kinyume na
kanuni za serikali za mitaa (Mamlaka za miji- Maadili ya Madiwani za mwaka
2000)
Alifafanua kuwa tuhuma zingine
zinazomkabili mstahiki meya Mhagama ni kwamba alilidanganya baraza la madiwani
lililofanyika Oktoba 30 mwaka jana kuwa kuna waraka unaozuia kamati ya maadili
ya taarifa inayomhusu kutojadiliwa kwenye baraza la madiwani huku akijua kuwa
hakuna waraka kama huo.
Alieleza zaidi kuwa mstahiki meya
Mhagama ambaye pia ni diwani wa kata ya Matogoro anatuhumiwa kushiriki vitendo
vya rushwa kwa kuchukua fedha kutoka kwa kila mkandarasi anayeomba nafasi ya
kutaka kufanya kazi kwenye manispaa hiyo.
Alisema kuwa inadaiwa kuwa
alichua rushwa kutoka kwa mfanyabiashara mmoja ambaye hakutaka kumtaja jina na
kumruhusu ajenge kibada cha biashara kwenye eneo lisiloruhusiwa na idara ya
mipango miji jambo ambalo ambalo linaonekana kuleta utata mkubwa na anadaiwa
kuvuruga michoro ya kituo kipya cha mabasi cha msamala iliyochorwa mwaka 2005
ambayo ilionyesha kuwa na vibanda vya maduka thelathini, 27 vibanda vya kukatia
tiketi za mabasi lakini hivi sasa vibanda vilivyopo vinafikia tisini na nane na
kwamba zoezi zima la ugawaji wa vibanda hivyo ulisimamiwa nay eye mwenyewe na
kujipatia fedha kutoka kwa waombaji mbalimbali.
Alisema kutokana na hali hiyo,
madiwani kumi wanapinga vikali matendo yote aliyoyafanya mstahiki meya Charles
Mhagama na kuamua kujiorodhesha majina ya madiwani na kutia saini kwa kila
diwani na kwamba lengo kubwa ni kutaka manispaa hiyo inafanya kazi kwa misingi
ya utawala bora.
Kwa upande wake mkurugenzi wa
halmashauri ya manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alikiri kupokea barua ya
madiwani kumi ya kuomba mkutano maalumu wenye lengo la kutokuwa na imani na
mstahiki meya Charles Mhagama ambayo alidai kuwa kwa hivi sasa inafanyiwa kazi
kwa kuangalia kanuni na sheria kama zitaruhusu kuitisha kikao cha baraza
wanachokihitaji madiwani hao.
Hata hivyo ,kurugenzi wa manispaa
hiyo Zakaria alisema kuwa madiwani hao walioomba kuitisha kikao cha kutokuwa na
imani na meya ni theluthi moja ambayo kisheria haiwezi kutengua nafasi ya meya
ila halmashauri inaweza kumwondoa meya madarakani ni theluthi mbili na siyo
theluthi moja kwani manispaa ya Songea ina jumla ya madiwani ishirini na nane,
na madiwani kumi ndo wamehitaji kikao cha baraza jambo ambalo linaonekana kuwa
kinyume na utaratibu lakini bado anaangalia kama kutakuwa na uwezekano wa
kuwepo hicho kikao.
Mstahiki meya Charles Mhagama
alipohojiwa kwa njia ya simu alisema kuwa mpaka jana alikuwa
hajakabidhiwa barua inayomtuhumu kutaka ajiengue katika nafasi aliyonayo
kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabiri licha ya kuwa alidai kuna habari
alizozisikia kuwa kuna baadhi ya madiwani wamejipanga kumg’oa katika nafasi
hiyo lakini alieleza kuwa ni vyema wafuate sheria na kanuni za kumwondoa
madarakani na pia wawe na ushahidi wa kutosha dhidi ya tuhuma wanazozisema
kwani endapo barua barua atakabidhiwa atapaswa apewe nafasi ya kuzijibu tuhuma
kabla ya kikao cha baraza wanachokihitaji kifanyike na si vinginevyo.
Post a Comment