h
KESI inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeibua mambo mapya, Tanzania Daima Jumatano, limebaini.
Habari kutoka ndani ya idara ya mahakama na polisi, zimelieleza gazeti hili kuwa jeshi la polisi limeandika barua kuiomba mahakama ya hakimu mkazi Kisutu itoe amri kwa mtuhumiwa namba mbili katika kesi ya jinai namba 6 ya mwaka 2013, Ludovick Joseph, atolewe gerezani na akae na makachero wa polisi kwa siku mbili ili waweze kumfanyia mahojiano upya.
Hatua hiyo ambayo duru za kisheria zimeelezea kama ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, imekuja wakati tayari Ludovick na Lwakatare wameshafikishwa mahakamani.
Habari zinasema kuwa tayari mtuhumiwa huyo ambaye tangu kesi yao ilipoahirishwa alirejeshwa mahabusu katika gereza la Segerea; sasa hivi yuko mikononi mwa polisi akifanyiwa mahojiano.
Msemaji wa jeshi la polisi nchini, Advera Senso, alilithibitishia gazeti hili jana kwa njia ya simu kwamba Ludovick yuko katika mikono ya polisi.
“Ludovick yuko mikononi mwa polisi, kazi ya upelelezi bado inaendelea, liacheni jeshi la polisi lifanye kazi yake,” alisema Senso.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umebaini kuwa kitendo cha kumchukua Ludovick kilifanyika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla faili la kesi hiyo kupelekwa mahakamani kama ilivyokuwa imeamriwa na Mahakama Kuu.
Kitendo cha kumchukua Ludovick pekee akae na polisi wakati suala hilo lilishafikishwa mahakamani limeibua maswali mengi kwa wadau mbalimbli wakiwemo wanasheria walioeleza kushangazwa na kitendo cha mahakama kushirikiana na polisi kumtoa Ludovick nje bila kuwepo waendesha mashtaka wa serikali na mawakili wa watuhumiwa hao kwani kesi inayowakabili inasikilizwa wazi hivyo ni lazima pande zote ziwepo kuafikiana kila jambo au kila hatua kadiri kesi inavyoendelea.
Wakili mmoja mzoefu nchini ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema hatua kesi ilipofikia, kitendo cha kumchukua Ludovick pekee kinaweza kuathiri mwenendo wa kesi kwani haijulikani polisi wanataka kumwambia nini au kumpa nini ili aweze kubadili maelezo aliyotoa awali.
Aidha wakili huyo ameishangaa pia mahakama kuruhusu iingiliwe na polisi na kutekeleza amri za polisi katika kesi hiyo bila kuwepo waendesha mashtaka wa serikali na mawakili wa upande wa utetezi.
“Sielewi kwa nini mahakama inafanya mambo haya kinyemela wakati inapaswa kuyafanya kwa uwazi kila upande ukiwepo na kuridhika na sababu zinazotolewa na upande mwingine katika kila maombi yanayoletwa mahakamani.”
Wakili huyo alikumbusha kuwa siku watuhumiwa hao walipofikishwa mahakamani na kuachiwa kwa muda, kisha kufunguliwa mashtaka tena, mawakili wa utetezi walitaka kutoa maombi lakini mahakama ilikataa kwa kusema kuwa mambo yote yangefanyika Aprili 04.
“Suala hilo lilipofikishwa mahakamani mara ya pili halikujadiliwa baada ya Hakimu Katemana kusema kwamba hakuwa na muda wa kulisikiliza kwani alikuwa anawahi kesi nyingine. Kesi hiyo sasa iliahirishwa hadi Aprili 4 na mawakili wa pande zote mbili waliafikiana.
“Kama waliona hawajakamilisha upelelezi kwa mshtakiwa wa pili, hawakuwa na sababu ya kukimbilia kumfikisha kortini halafu leo wanakuja kumchukua tena akiwa mahabusu, hii haiwezekani,” alisema wakili huyo.
Hii ni mara ya pili kwa mahakama kutoa maamuzi yenye utata kuhusu kesi hiyo inayovuta hisia za wengi.
Machi 20, 2013 Ludovick na Lwakatare walifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka manne mbele ya Hakimu Emilius Mchauru.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, wakili wa serikali, Prudence Rweyongeza, aliwasilisha hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akiiomba mahakama kuwaachia chini ya kifungu cha 91 (1). Kifungu hicho ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi huyo wa Mashtaka kufuta mashtaka pale anapoona hana sababu ya kuendeleza mashtaka ya mtuhumiwa bila hata ya kutoa sababu zilizosababisha kufanya hivyo.
Mchauru alikubaliana na hati hiyo na kuwafutia mashtaka washtakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi namba 37 ya mwaka 2013, iliyokuwa na mashtaka manne yanayohusu vitendo vya ugaidi.
Hata hivyo, baada ya washtakiwa hao kuachiwa huru na Mchauru, walipotoka nje ya chumba cha mahakama, askari ambao walikuwa wamevaa sare na nguo za kiraia, waliwakamata tena.
Baada ya kukamatwa upya, Lwakatare na mwenzake, walipandishwa tena kizimbani, safari hii mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, na kusomewa kesi mpya namba 96, yenye mashtaka manne yanayofanana na yale ya awali ya ugaidi.
Ludovick na Lwakatare kwa mujibu wa Wakili Mkuu wa Serikali, Prudence Rweyongeza, wanakabiliwa na mashtaka manne, yakiwemo ya kula njama ya kumdhuru kwa sumu na kumteka Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, Desemba 28, 2012 katika eneo la Stop Over Kimara.
Shtaka la pili, kwa washtakiwa wote, limefunguliwa chini ya kifungu cha sheria namba 24 (2) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002; watuhumiwa wanadaiwa walikula njama ya kumteka Denis Msacky kinyume cha sheria namba 4 (2) (C) (iii) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.
Shtaka la tatu, linawakabili washtakiwa wote pia, wanadaiwa kinyume cha kifungu namba 5(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, kwa pamoja walifanya mkutano wa kufanya vitendo vya kigaidi, walipanga na kushiriki mkutano huo wenye lengo la kupanga kitendo cha ugaidi kwa kumteka nyara Msacky.
Shtaka la nne ni la kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
source:
Post a Comment