Na Gideon Mwakanosya-
Songea
Mjumbe
wa Halmashauri kuu ya Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Edson Mbogolo, amewamwagia sifa wabunge watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
kuwa ndio wawakilishi wazuri na ni wakweli kwa wananchi Bungeni kwani hoja zao
wanazozitoa zimekuwa zikileta tija kwa jamii wakiwemo wapiga kura wao.
Hayo
yalisemwa juzi (Jumapili) kwenye viwanja vya shule ya msingi Matalawe katika
Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na
CHADEMA ambao ulihudhuriwa na mamia ya wakazi wa Manispaa hiyo akiwemo
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe.
Mbogolo
aliwataja wabunge ambao alidai kuwa ndio watetezi wazuri wa wapiga kura wao
kuwa ni Deo Filikunjombe mbunge wa jimbo la Ludewa mkoa wa Njombe, Kangi Lugola
Mbunge wa jimbo la Mwibala mkoa wa Mara na Ally Kessy Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini Mkoani Rukwa.
Alisema
kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiwashangaa wabunge wengi wa CCM ambao wamekuwa
wakitoka kwenye majimbo yao kwenda Bungeni bila kubeba hoja za wapiga kura wao
badala yake wamekuwa wakitumia muda mwingi kukejeli na kubeza hoja zinazotolewa
na wabunge wa upinzani ndani ya Bunge jambo ambalo wanaona ni kitu cha kawaida.
Amewaomba
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali itikadi za
vyama vyao vya kisiasa ni vyema wawe wanaona ni muhimu kuwa na hoja
zitakazoleta manufaa kwa wapiga kura wao na taifa kwa ujumla na si vinginevyo.
Alieleza
kuwa inashangaza sana kuona serikali inaacha kuwabana wabunge wanawaobeza
wabunge wenzao wanapotoa hoja zenye tija kwa taifa na badala yake serikali hiyo
imekuwa ikitengeneza mazingira ya kuwabana wabunge wa vyama vya upinzani na
baadhi ya wabunge wa CCM pale wanapotoa hoja Bungeni walizotumwa kutoka kwenye
majimbo yao lakini inaanza mikakati ya kuwabana ili wasiendelee kusema ukweli
kwa manufaa ya Taifa.
“Ndugu
wananchi ninashangazwa kuona kwamba serikali kupitia ofisi ya Bunge ilifikia
uamuzi wa kutaka kuwa mijadala inayotolewa Bungeni isirushwe kwenye luninga
jambo ambalo linaonesha wazi kuwa serikali haina nia nzuri ya kuhakikisha kuwa
wananchi wanaona kinachofanyika Bungeni”. Alisema Mbogolo.
Naye
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime akimkaribisha Mwenyekiti wa
CHADEMA Taifa Freeman Mbowe ili aweze kuongea na wananchi kwenye mkutano huo wa
hadhara alisema kuwa CHADEMA mkoa wa Ruvuma kwa sasa hivi imejipanga kikamilifu
kuhakikisha kuwa mwaka 2015 majimbo yote ya Mkoa wa Ruvuma yatashikwa na
wabunge kutoka CHADEMA na alidai kuwa jitihada zinafanywa zaidi kuhakikisha
kuwa jimbo la Songea Mjini, linaloshikiliwa na DK. Emmanuel Nchimbi kwa sasa,
ni lazima ushindi wa kishindo upatikane.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, akiongea na wananchi wa Songea
alisema kuwa Watanzania wana haki za msingi kuchagua chama cha siasa
wanachokipenda ambacho wao wanaona kuwa ndicho kitakachoweza kuwakomboa na si
vinginevyo.
Alisema
kuwa Tanzania ina makundi mawili ya uongozi ambapo alilitaja kundi la kwanza
kuwa ni la viongozi wanaochaguliwa na wananchi wenyewe ambalo linapaswa kuwa na
mamlaka na kundi la pili akalitaja kuwa ni la viongozi wanaoteuliwa na Rais
ambalo ndilo linaloonekana kusikilizwa zaidi na kuwa na maamuzi makubwa kutoka
serikalini hivyo amewataka wananchi waone umuhimu kwa sasa hivi kuwa viongozi wote wanaoteuliwa
na Rais kama vile wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa wanachaguliwa na wananchi
na jambo hili liingizwe kwenye katiba mpya.
Alifafanua
zaidi kuwa wnanchi katika kila wilaya au mkoa wananchi ni vyema wachague wakuu
wa wilaya na wakuu wa mikoa kutoka katika
maeneo yao kupitia kwenye vyama vyao vya siasa badala ya ilivyo sasa
hivi ambapo wanateuliwa na Rais kutoka katika maeneo tofauti na wanayoongoza.
Aliwataka
Watanzania kutambua kuwa mfumo wa siasa wa vyama vingi sio wa ugonvi wala sio
wa kuwekeana chuki badala yake vyama vya upinzani ndivyo vinavyoweka bayana
changamoto zilizopo kwa serikali inayoongozwa na chama tawala ambayo inapaswa
kuzifanyika kazi changamoto hizo.
Post a Comment