Loading...

Vyandarua vyatumika kuanikia dagaa ziwa Nyasa



Na Gideon Mwakanosya -Mbambay

Baadi ya wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyoko kandokando ya ziwa Nyasa katika wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma wamewalalamikia baadhi ya wananchi wakiwemo wavuvi wa samaki kwa tabia yao ya kutumia vibaya vyandarua tofauti na makusudio yake ambapo serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  kwa muda mrefu imekuwa ikigawa vyandarua bure lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia kuvulia samaki huku wengine wakitumia kuanikia dagaa kwenye vichanja.


Wakizungumza na NIPASHE, kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Mbaha na Lundu wananchi hao ambao waliomba majina yao yafadhiwe walisema kuwa serikali imekuwa ikigawa vyandarua kwa kila kaya kwa lengo la kupunguza malaria lakini ni jambo la kushangaza baadhi ya wavuvi na wakazi wengine wamekuwa wakitumia vyandaraua hivyo tofauti na ilivyokusudiwa.


Walisema kuwa katika vijiji vingi vilivyoko kandokando ya ziwa Nyasa kumekuwa na tabia hiyo mbaya ambayo inaweza kuhatarisha maisha kwa wakazi wa maeneo hayo ya kuchukua vyandarua kwenye majumba na kupeleka ziwani kuvulia samaki huku wengine wakanikia dagaa wakati wanajua kwamba vyandarua hivyo vimewekwa dawa za viuatilifu.


Wameiomba serikali ya wilaya hiyo kuona umhimu wa kuwazuia au kuwapiga marufuku kuvulia na kuanikia samaki vyandarua na badala yake wananchi wahimizwe kuvitumia vyandarua kama ilivyokusudiwa na serikali na sio vinginevyo. 


Hata hivyo mratibu wa malaria wa mkoa wa Ruvuma, Kibua Amani Kakolwa, alisema kuwa kampeni ya ugawaji vyandarua sehemu za malazi ilifanyika mwaka 2010 ambapo jumla ya vyandarua 706219 viligawiwa kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma wakti vyandarua  236375 viligawiwa katika wilaya ya Mbinga kabla kabla wilaya hiyo haijagawanywa.


Kibua alisema kuwa lengo kuu ni kuwa wananchi wanapaswa kuvitumia kila siku ili waweze kujikinga na mbu waenezao malaria na uwezo wa vyandarua hivyo ni miaka mitatu hadi mitano kama vinatunzwa vizuri hivyo watu  wanaoamua kuanikia au kuvulia dagaa wanakwenda tofauti na malengo ya serikali.


Aliongeza kuwa faida ya vyandarua itaonekana katika kupunguza malaria endapo kila mwananchi atatumia chandarua chake kwa usahihi na amezishauri mamlaka za halmashauri za wilaya zitumie sheria ndogo walizo nazo kuhakikisha kuwa wananchi hawatumii vyandarua kwa shughuli ambazo hazikukusudiwa na serikali.


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Nyasa, Ernest Kahindi, aliiambia NIPASHE kuwa ofisi yake ilishapokea malalamiko hayo na kwamba kwa hivi sasa amewaagiza viongozi wote wa serikali wakiwemo maafisa watendaji wa vijiji na kata kuwa mwananchi yeyote atakayepatikana kuainikia dagaa  au kuvulia samaki akamatwe na achukuliwe hatua haraka iwezekanavyo na maafisa wa idara ya maliasili tayari wameshaanza kufanya msako kijiji hadi kijiji kandokando ya Ziwa Nyasa ili kuwabaini waharibifu wa vyandarua. 


Mwisho      



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top