Na Stephano Mango,Songea.
MGOMBEA Udiwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
katika Kata ya Lizaboni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani
Ruvuma kwenye Uchaguzi mdogo ameshinda kwa kupata kura 1712 wakati
Mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika Kata hiyo George Oddo Mbunda
alipata kura 1579.
Akitangaza matokeo hayo mara tu baada ya
kumaliza zoezi la uchaguzi lililoanza majira ya saa 1 asubuhi hadi saa
10 jioni Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kata ya Lizaboni Mussa
Chiwango alimtangaza Alanus Mlongo wa Chadema kuwa ndiye aliyeshinda
katika Uchaguzi huo.
Chiwango ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa
Kata hiyo alisema kuwa kwenye orodha ya daftari ya kupigia kura
inaonyesha kuwa Wananchi waliojiandikisha ni 7825 lakini waliopiga kura
ni 3315 jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa wakazi wengi wa Kata hiyo
hawakuweza kujitokeza kupiga kura.
Kwa upande wake Diwani
Mteule wa Kata ya Lizaboni Mlongo mara tuu baada ya kutangazwa kuwa ni
mshindi alieleza kuwa nafasi hiyo amepewa na Mwenyezi Mungu hivyo
anawajibu mkubwa wa kuangalia changamoto zilizopo kwenye Kata hiyo
ambazo zinahitajika zifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.
Alieleza zaidi kuwa mara tu baada ya kuapishwa kazi yake ya kwanza
itakuwa ni kuhakikisha kuwa ana ubana uongozi wa Halmashauri ya Manispaa
ili kumaliza tatizo kubwa lililopo la Miundo mbinu ya barabara,maji na
Ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye Shule za Sekondari za Londoni na
Mjimwema.
Naye Katibu wa Jimbo la Songea la Chama hicho Masumbuko Paul Masumbuko aliiambia www.stephanomango.blogspot.com
kuwa ushindi walioupata kwenye uchaguzi mdogo kwenye Kata ya Lizaboni
ni endiketa kwa CCM kwamba kila Uchaguzi utakapofanyika kuanzia sasa
Chadema lazima washinde kwani mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya
Songea ina Kata 21 ambapo kati ya hizo Kata sita zina ongozwa na
Madiwani wa Chadema.
Alibainisha zaidi kuwa mbinu zilizotumika
ambazo zimefanikisha ushindi kwenye Kata ya Lizaboni ndizo mbinu
zinazotarajia kufanyika kwenye Kata nyingine ya Mletele ambayo iko wazi
tangu Diwani wa Kata hiyo alipofariki dunia miezi 2 iliyopita.
Aidha
Masumbuko alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wafuasi wa CCM ambao
walikwenda kwenye maeneo ya kupigia kura huku wakiwa na vitisho lakini
kwa vile wafuasi wa Chadema nao walijipanga walifanikisha kukamata gari
la kigogo mmoja wa CCM likiwa limesheheni fimbo ambazo zinahofiwa kuwa
zilikuwa zinatakiwa kutumika kwaajili ya kuwapigia wafuasi wa Chadema
jambo ambalo liliufanya uongozi wa Chama cha Chadema kumtafuta mmiliki
wa hilo gari ambaye hakutaka kutaja jina ili aweze kueleza ni kwanini
aliamua kuchukua fimbo kwenye gari lake na kupeleka kwenye eneo la
kupigia kura.
Alisema kuwa licha ya mmiliki wa gari hilo kutoa
sababu ambazo ni dhaifu kuwa alikuwa amemtuma dereva wake kwenda
kijijini kutafuta fito ambazo zingemsaidia kujengea zizi la mbuzi askari
Polisi waliokuwa kwenye doria waliikamata gari hiyo na kuiondoa kwenye
eneo hilo na kufanikisha mpaka uchaguzi unakwisha usalama kwa wapiga
kura unakuwepo jambo ambalo amelieleza kuwa jeshi hilo la Polisi
linastahili pongezi tofauti na walivyokusudia.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alipoulizwa www.stephanomango.blogspot.com
kuwa katika zoezi zima la uchaguzi mdogo wa Kata ya Lizaboni kama
kulikuwepo na tofauti yeyote alisema kuwa Jeshi lake lilijipanga katika
maeneo yote ya Kata hiyo kwa kuhakikisha kuwa Vituo vyote vya kupigia
kura vinalindwa bila kuwepo vurugu ya aina yeyote na aliongeza kuwa
suala la gari kukamatwa likiwa limebeba fimbo Ofisini kwake lilikuwa
bado halijamfikia na alidai kuwa inawezekana lilimalizwa na askari wake
wa chini ambao waliona hakuna sababu ya msingi ya kuendelea kulishikilia
gari.
Mgombea wa Udiwani wa Chama cha Mapinduzi Mbunda alipoulizwa na www.stephanomango.blogspot.com
kuhusiana na zoezi zima la uchaguzi alisema kuwa kubwa zaidi
anawashukuru Wakazi wa Lizaboni ambao walionyesha nia ya kutaka awe
Diwani wao lakini kwa bahati mbaya kura hazikutosha hivyo amewaomba
wawe na subira hadi hapo mambo ya uchaguzi yatakapojitokeza tena.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Wilaya ya Songea Mjini
Victor Ngonyani amesema kuwa kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi hivyo
kushindwa kwa Ccm kwenye uchaguzi mdogo huo wa Udiwani ni changamoto
kubwa ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Chama cha Mapinduzi ili
changamoto kama hizo zisijirudie tena na kwa kuto kuoneana haya kwa
Wanachama ambao wanaonekana kuwa ndiyo waliosababisha Ccm kupigwa na
Chadema
Monday, April 2, 2012
Post a Comment