Loading...

SONGEA YAGEUKA UWANJA WA MAPAMBANO

VURUGU ZASABABISHA WATU WATATU KUFARIKI SONGEA
Na Gideon Mwakanosya,Songea.
 
WATU watatu wamefariki dunia na idadi kubwa ya watu wanadaiwa kujeruhiwa kutokana na hali tete iliyozuka katika mji wa Songea mkoani Ruvuma, baada ya mamia ya wananchi na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la yeboyebo, kuandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi na ofisi ya mkuu wa mkoa huo, wakipinga mauaji ya raia ambayo yameshamiri katika mji huo.
 
Kufuatia maandamano hayo kushika kasi katika mji huo, jeshi la polisi lililazimika kuingilia kati kwa kuanza kupiga mabomu ya machozi na risasi za moto hewani ikiwa ni lengo la kuwatawanya raia hao wasiendelee kuleta vurugu.  
 
Wakati mabomu na risasi hizo zikipigwa, ghasia za hapa na pale zilianza kujitokeza baadhi ya wananchi wakirusha mawe kuelekea kituo kikuu cha polisi na wengine wakipaza sauti wakielekeza lawama kwa jeshi hilo kwamba limeshindwa kudhibiti mauaji hayo.
Vurugu hizo zimesababisha ofisi za serikali na taasisi binafsi mkoani Ruvuma kufungwa kwa muda yakiwemo maduka na huduma za kifedha katika mabenki zimesimama kwa muda.
 
Huduma za usafiri katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani nazo zimesimama huku madereva wa mabasi na abiria wakikimbia kujificha kwa lengo la kuepukana na mabomu ya machozi na risasi za moto zilizokuwa zikipigwa hewani.
 
 Matukio ya mauaji katika mji wa songea yalianza kujitokeza mapema mwezi Novemba mwaka jana yakiendelea hadi sasa, ambapo kila baada ya siku kadhaa watu walikuwa wanauawa katika mazingira ya kutatanisha huku miili ya marehemu ikikutwa imejeruhiwa vibaya.
 

Watu tisa wameuawa katika mji huo tokea matukio ya mauaji yaanze kujitokeza katika mji wa Songea na kwamba watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanashikiliwa na polisi.
Watuhumiwa wanaoshikiliwa na jeshi la polisi ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa mtaa wa Lizaboni mjini Songea.
 
Pamoja na mambo mengine mpaka habari hizi zinaingia mitamboni Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma hawakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo huku simu zake zikiwa zimefungwa na askari polisi mjini hapa wakiendelea kupiga mabomu ya machozi, kwa lengo la kutawanya watu.Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top