Loading...

CHADEMA YASHINDA UDIWANI MANISPAA YA SONGEA



Na Stephano Mango,Songea.

MGOMBEA Udiwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kata ya Lizaboni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kwenye Uchaguzi mdogo ameshinda kwa kupata kura 1712 wakati Mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika Kata hiyo George Oddo Mbunda alipata kura 1579.

Akitangaza matokeo hayo mara tu baada ya kumaliza zoezi la uchaguzi lililoanza majira ya saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kata ya Lizaboni Mussa Chiwango alimtangaza Alanus Mlongo wa Chadema kuwa ndiye aliyeshinda katika Uchaguzi huo.

Chiwango ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata hiyo alisema kuwa kwenye orodha ya daftari ya kupigia kura inaonyesha kuwa Wananchi waliojiandikisha ni 7825 lakini waliopiga kura ni 3315 jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa wakazi wengi wa Kata hiyo hawakuweza kujitokeza kupiga kura.

Kwa upande wake Diwani Mteule wa Kata ya Lizaboni Mlongo mara tuu baada ya kutangazwa kuwa ni mshindi alieleza kuwa nafasi hiyo amepewa na Mwenyezi Mungu hivyo anawajibu mkubwa wa kuangalia changamoto zilizopo kwenye Kata hiyo ambazo zinahitajika zifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.

Alieleza zaidi kuwa mara tu baada ya kuapishwa kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha kuwa ana ubana uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ili kumaliza tatizo kubwa lililopo la Miundo mbinu ya barabara,maji na Ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye Shule za Sekondari za Londoni na Mjimwema.

Naye Katibu wa Jimbo la Songea la Chama hicho Masumbuko Paul Masumbuko aliiambia www.stephanomango.blogspot.com kuwa ushindi walioupata kwenye uchaguzi mdogo kwenye Kata ya Lizaboni ni endiketa kwa CCM kwamba kila Uchaguzi utakapofanyika kuanzia sasa Chadema lazima washinde kwani mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina Kata 21 ambapo kati ya hizo Kata sita zina ongozwa na Madiwani wa Chadema.

Alibainisha zaidi kuwa mbinu zilizotumika ambazo zimefanikisha ushindi kwenye Kata ya Lizaboni ndizo mbinu zinazotarajia kufanyika kwenye Kata nyingine ya Mletele ambayo iko wazi tangu Diwani wa Kata hiyo alipofariki dunia miezi 2 iliyopita.

Aidha Masumbuko alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wafuasi wa CCM ambao walikwenda kwenye maeneo ya kupigia kura huku wakiwa na vitisho lakini kwa vile wafuasi wa Chadema nao walijipanga walifanikisha kukamata gari la kigogo mmoja wa CCM likiwa limesheheni fimbo ambazo zinahofiwa kuwa zilikuwa zinatakiwa kutumika kwaajili ya kuwapigia wafuasi wa Chadema jambo ambalo liliufanya uongozi wa Chama cha Chadema kumtafuta mmiliki wa hilo gari ambaye hakutaka kutaja jina ili aweze kueleza ni kwanini aliamua kuchukua fimbo kwenye gari lake na kupeleka kwenye eneo la kupigia kura.

Alisema kuwa licha ya mmiliki wa gari hilo kutoa sababu ambazo ni dhaifu kuwa alikuwa amemtuma dereva wake kwenda kijijini kutafuta fito ambazo zingemsaidia kujengea zizi la mbuzi askari Polisi waliokuwa kwenye doria waliikamata gari hiyo na kuiondoa kwenye eneo hilo na kufanikisha mpaka uchaguzi unakwisha usalama kwa wapiga kura unakuwepo jambo ambalo amelieleza kuwa jeshi hilo la Polisi linastahili pongezi tofauti na walivyokusudia.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alipoulizwa www.stephanomango.blogspot.com kuwa katika zoezi zima la uchaguzi mdogo wa Kata ya Lizaboni kama kulikuwepo na tofauti yeyote alisema kuwa Jeshi lake lilijipanga katika maeneo yote ya Kata hiyo kwa kuhakikisha kuwa Vituo vyote vya kupigia kura vinalindwa bila kuwepo vurugu ya aina yeyote na aliongeza kuwa suala la gari kukamatwa likiwa limebeba fimbo Ofisini kwake lilikuwa bado halijamfikia na alidai kuwa inawezekana lilimalizwa na askari wake wa chini ambao waliona hakuna sababu ya msingi ya kuendelea kulishikilia gari.

Mgombea wa Udiwani wa Chama cha Mapinduzi Mbunda alipoulizwa na www.stephanomango.blogspot.com kuhusiana na zoezi zima la uchaguzi alisema kuwa kubwa zaidi anawashukuru Wakazi wa Lizaboni ambao walionyesha nia ya kutaka awe Diwani wao lakini kwa bahati mbaya kura hazikutosha hivyo amewaomba wawe na subira hadi hapo mambo ya uchaguzi yatakapojitokeza tena.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Wilaya ya Songea Mjini Victor Ngonyani amesema kuwa kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi hivyo kushindwa kwa Ccm kwenye uchaguzi mdogo huo wa Udiwani ni changamoto kubwa ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Chama cha Mapinduzi ili changamoto kama hizo zisijirudie tena na kwa kuto kuoneana haya kwa Wanachama ambao wanaonekana kuwa ndiyo waliosababisha Ccm kupigwa na Chadema



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright 2025 songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US