chanzo: Mwananchi Sunday, 01 July 2012 09:54 |
SIRI zaidi za ufisadi katika mchakato wa kumiliki mgodi wa makaa ya mawe Kiwira mkoani Mbeya, zimedizi kuibuliwa baada ya kubainika kwamba sehemu ya mgodi huo ilimilikishwa kinyemela kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona. Yona kupitia Kampuni yake ya Tan-Power Resources Ltd (TPR) anadaiwa kujimilikisha mgodi huo kwa kutoa leseni ya umiliki Desemba 19, 2005, ambayo ni siku ya mwisho ya kuwapo ofisini kwake akiwa Waziri wa Nishati na Madini na siku moja kabla ya kuapishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kushika nafasi ya urais. Kikwete aliapishwa kuwa Rais katika awamu yake ya kwanza ya uongozi, Desemba 20, 2005 katika Uwanja wa Uhuru (zamani Uwanja wa Taifa) jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona, Yona anadaiwa kujipa mgodi huo kwa leseni maalumu namba SML 235/2005 ambayo iliiwezesha TPR kuwa mmiliki wa mgodi wa Kabulo ambao ni sehemu ya mgodi wa Kiwira. Utafiti wa awali katika eneo la Kiwira (Kiwira Complex), ulifanywa na Serikali kupitia Shirika lake la Madini (Stamico) na kubaini kuwapo kwa mashapo ya makaa ya mawe ambayo yanafikia futi za ujazo tani milioni 139 katika milima mitatu iliyopo eneo hilo. Nyaraka zinabainisha kuwa, milima hiyo ni Kabulo wenye mashapo yenye futi za ujazo tani milioni 50.9, Kiwira tani milioni 35.4 na mlima wa mwisho ni Ilema wenye futi za ujazo tani 280,000. Utafiti huo ulifanywa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB), kiasi cha dola za Marekani milioni 6.3 karibu Sh10 bilioni kwa mujibu wa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambavyo ni wastani wa Sh1,576.75 kwa dola moja ya Marekani. Imebainika kuwa, Serikali baada ya kufanya utafiti huo wa awali, Stamico ilipewa leseni ya umiliki wa mashapo ya Kiwira na Ilema ambayo jumla yake ni futi za ujazo tani milioni 35.7 kiasi ambacho hakifikii mashapo yaliyopo kwenye mlima wa Kabulo. Mlima wa Kabulo ndiyo eneo ambalo Yona anadaiwa kujimilikisha akiwa Waziri wa Nishati na Madini na wakati huohuo akiwa mbia katika kampuni ya Tan Power Resources Ltd. Alijimilikisha kwa hati maalumu, japokuwa hakuna taarifa zozote zinazothibitisha iwapo alilipa fedha za kufidia gharama za utafiti uliofanywa na Serikali kwa mkopo wa Benki ya Dunia au la. Mmoja wa maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema kwa mujibu wa sheria, TPR hawakupaswa kupewa leseni maalumu (special mining licence) kwani kampuni inayopewa leseni ya aina hiyo lazima iwe imefanya utafiti (exploration) husika katika eneo husika. Ngeleja aliidhinisha Kabulo kuuzwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, wiki iliyopita wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali bungeni, alifichua kwamba mgodi wa Kabulo wenye hazina kubwa ya makaa ya mawe sasa umeuzwa kwa bei ya kutupa kwa Kampuni ya Intra Energy ya Australia. Mkono alisema, Kabulo ambayo ni sehemu ya mgodi wa Kiwira mkoani Mbeya, umeuzwa kwa kiasi cha Dola za Marekani 700,000 wakati thamani yake ni matrilioni ya Shilingi, hivyo kupendekeza kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwenda kuchunguza ufisadi katika mgodi huo. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini pia kwamba Ngeleja akiwa waziri mwenye dhamana ya nishati na madini, ndiye aliyetoa idhini ya kuuzwa kwa mgodi huo kwa kampuni iitwayo Tanzacoal East Africa Ltd ambayo ni sehemu ya Kampuni ya Intra Energy ya Australia. Mwananchi limefanikiwa kuona kibali hicho kilichosainiwa na Ngeleja na kikihamisha leseni maalumu iliyotolewa na Yona mwaka 2005 kwenda Tanzacoal. Sehemu ya kibali hicho inasomeka: “Mimi Waziri wa Nishati na Madini kwa mamlaka niliyopewa chini ya sehemu ya 9(2) ya Sheria ya madini ya namba 14 ya 2010, natoa idhini ya kuhamisha jina, haki na majukumu yaliyopo chini ya leseni maalumu namba 235/2005 kutoka kampuni ya Tan Power Resources Ltd kwenda Tanzacoal East Africa Mining Ltd.” Idhini ya kuuzwa kwa mgodi huo iliyotolewa na Ngeleja, ilitanguliwa na ushauri uliotolewa kwake na aliyekuwa Kamishna wa Madini, Dk Dalaly Kafumu ambaye sasa ni mbunge wa Igunga (CCM). Kafumu katika ushauri wake wa maandishi kwenda kwa Ngeleja alioutoa Agosti 24 (siku mbili kabla ya idhini ya waziri huyo) unasomeka: “Transfer hii imepitiwa na kuonekana haina matatizo ya kisheria, nashauri usaini transfer hii.” Wakati Dk Kafumu akitoa ushauri huo kwa Ngeleja, tayari alikuwa ameshinda kura za maoni za kuwania ubunge wa Igunga zilizopigwa Agosti 19, 2011 na baadaye aliteuliwa rasmi na Kamati Kuu ya CCM kupeperusha bendera ya chama hicho, siku tano tangu atoe ushauri kwa Ngeleja, Agosti 29, 2011. Ngeleja aliliambia gazeti hili kwamba hakukuwa na kosa kwake kusaini hati ya kuhamisha kazi za kampuni hiyo kwani, leseni ya umiliki wa mgodi wa Kabulo ni tofauti na leseni ya kumiliki migodi mingine katika eneo la Kiwira. “Sitaki kusema sana maana mimi siko serikalini sasa, ila watu wengi hawafahamu kwamba ule mgodi wa Kabulo umiliki wake ni wa leseni tofauti kabisa na ile migodi mingine,”alisema Ngeleja. Kauli ya Serikali Hivi karibuni akijibu hoja za wabunge kuhusu mgodi huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema wameitisha mkutano wa wahusika wote wa suala hilo katika mkutano ambao unalenga kufahamu ukweli wa sakata la mgodi huo. Profesa Muhongo alisema suala la mgodi huo limegubikwa na mambo mengi ambayo yanahitaji kuwekwa wazi na kuahidi kutoa taarifa ya kina wakati atakapowasilisha hotuba yake bungeni Julai 24 mwaka huu. Waziri huyo pia alizungumzia mpango wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutaka kununua mgodi huo kwamba ulishindikana kutokana na kampuni ya City Energy Transfer ya Dubai ambayo walitaka kushirikiana nayo kubainika kwamba haikuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo. Kauli ya Yona Alipotafutwa na gazeti hili wiki hii, kuzungumzia nafasi yake katika kujipa mgodi wa Kabulo, Yona alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu suala hilo, badala yake alitaka aulizwe Mkurugenzi wa Kiwira aliyemtaja kwa jina la Francis Tabaru. “Kwa kweli siwezi kuzungumza chochote, yupo mtu anayefahamu kila kitu kuhusu suala hilo naye ni Mkurugenzi wa Kiwira Coal Mine. Anaitwa Tabaru Francis. Huyo ndiye mtu sahihi, anafahamu kila kitu,” alisema Yona. Hata pale alipoambiwa kwamba suala hilo linamuhusu yeye alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini, Yona alisisitiza kwamba mambo yote aulizwe Tabaru. Kwa upande wake Tabaru alipopigiwa simu yake ya kiganjani alisema: “Mimi kweli nadhani mnanionea. Ninachoweza kukushauri ni kwamba hebu nenda kwa Kamishna wa Madini, yeye anafahamu kila kitu na nitashangaa asipokupa taarifa maana zipo. Mimi naweza nisiwe na taarifa sahihi sana, lakini ukienda huko nadhani unaweza kupata taarifa za uhakika.” TPR mgodini Kiwira Wakati Yona alipojipa leseni hiyo maalumu ya kumiliki Kabulo, tayari kampuni yake ya Tan Power Resources Ltd ilikuwa ikimiliki sehemu nyingine ya mgodi wa Kiwira kutokana na ubia iliyoingia na Serikali Juni mwaka huo wa 2005. Ubia wa pande hizo uliziwezesha kuunda Kampuni ya Kiwira Coal & Power Limited (KCPL), ikiwa na malengo ya kufufua uendeshaji wa mgodi huo na kuuwezesha kuzalisha umeme ambao ulitarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Hata hivyo, KCPL ambayo pia ilikuwa ikiendeshwa na Tan Power Resources licha ya kwamba kampuni hiyo ilikuwa mbia mwenye hisa asilimia 70, ilishindwa kutekeleza makusudio yake hivyo kuilazimisha Serikali kuurejesha mgodi huo mikononi mwake. Wakati wa mjadala wa bajeti bungeni Dodoma, suala hilo pia liliibuka, mara hii wabunge wakitaka Serikali itoe maelezo ya sababu za kutengwa kiasi cha Sh40 bilioni kwa ajili ya Kiwira. Chini ya uongozi wa menejimenti ya TPR, KCPL ilipata hasara ya Sh61 bilioni na hadi kufikia Desemba 31, 2010 ilikuwa imelimbikiza hasara ya zaidi Sh61 bilioni wakati madeni yake yalikuwa yakifikia Sh56 bilioni. Kulingana na ukaguzi uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Hesabu ya PKF, madeni hayo yanatokana na mikopo kutoka benki na taasisi za fedha ambazo jumla yake ni Sh32.19 kutoka Benki ya CRDB inayodai kiasi cha Sh4.65 bilioni, Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), Sh11.09 bilioni na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sh16.5 bilioni. Kadhalika taarifa hizo za hesabu zinathibitisha kwamba, Sh23.81 bilioni ni madeni yanayohusiana na wafanyakazi na wadai wengine. Kutokana na hali hiyo, nyaraka mbalimbali ambazo Mwananchi limeziona zinathibitisha kuwa Serikali ilishauriwa na timu ya wataalamu kutoilipa kampuni hiyo kiasi chochote baada ya kufanyika kwa uamuzi wa kurejeshwa kwake serikalini baada ya kushindwa kutekeleza kazi zake. |
Loading...
Post a Comment