Loading...

MAHAKAMA YAPELEKA KILIO KWENYE FAMILIA

Na Steven Augustino, Tunduru
MAHAKAMA kuu Tanzania Kanda ya Songea imepeleka kilio katika familia ya Shaibu Zuberi Kipande baada ya kumhukumu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika kosa la kuua kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002.

Kipande alihukumiwa adhabu hiyo baada ya Mahakama hiyo kumtia hatiani katika kosa kubwa la kuua kwa kukusudia, shauri Namba 7/2012 lililofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Songea na kusikilizwa katika kikao cha Mahakama Kuu kilichofanyika katika Mahakama ya Wilaya ya Tunduru. Bwana Kipande alishtakiwa kwa kosa la kumuua Hamisi Henyeka kwa kumnyonga na kumvunja shingo tukio lililotokea katika kijiji cha Nakapanya Wilayani Tunduru Januari 28/2010 na kwamba kutokana na mazingira hayo alistahili kupata adhabu hiyo kutokana na unyama alioufanya.

Sambamba na familia hiyo kuonja makali kutokana na machungu hayo ya kutenganishwa na ndugu yao huyo ambaye hata kaburi lake hawataliona,familia mbili ambazo ndugu zao walikuwa katika hamaki kutokana na kusubilia kutolewa kwa amri na Mahakama hiyo kutokana na tuhuma za aina hiyo Adhabu iliyotolewa ikawafuta machozi ya kutengana na ndugu zao muda mrefu baada ya Mahakama hiyo kuwaona hawana hatia na kuwaachia huru taarifa ambayo ililishitua Jeshi la polisi kutokana na vijana hao kudaiwa kuifahamu vyema yazi hiyo wawapo mitaani.

Aidha katika Mahakama hiyo pia familia nyingine tano (5) za wafungwa waliokuwa wakitumikia vifungo tofauti baada ya kupatikana na hatia katika makosa ya wizi wa kutumia silaha nazo zikanufaika na Rufaa walizokata baada ya mahakama hiyo kutengua adhabu za vifungo hivyo huku mahakama hiyo ikibainisha kuwa sababu za kuachiliwa huru kwao kunatokana na kilichodaiwa kuwa ni udhaifu wa ushahidi pamoja na kutozingatiwa kwa vifungu sahihi wakati wa kufungua mashtaka.

Akifafanua adhabu hizo Hakimu Mkuu Mwenye mamlaka ya Ki JAJI Mhesh. Wilifred Peter Dyansobera alisema kuwa mahakama hiyo imetoa adhabu ya kunyogwa hadi kufa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne waliongozwa kutoa ushahidi wao mahakamni na Mwanasheria mwandamizi wa Serikali Mkoani Ruvuma Maurice
Mwamwenda.

Alisema mbali na kuzingatia rai ya upande wa utetezi iliyotolewa na Wakili Msomi wa kujitegemea Dickson Ndunguru alitoa maoni kuwa adhabu anayostahili mstakiwa ni kunyongwa na kwa kuwa hakuna adhabu mbadala kwa mujibu wa kosa la mauaji ya makusudi aliomba Mahakama iandae nyaraka zinazostahili ili mshtakiwa aweze kukata rufaa.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na mwanasheria wa Serikari Wilbroad Ndunguru alihitimisha kwa kutoa maoni kwa kuiomba Mahakama hiyo izingatie kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 juzuu ya 2002 katika kutoa adhabu kwa mshtakiwa.

Aidha Hakimu Mkuu mwenye mamlaka ya Jaji,Mhesh. Dyansobera baada ya kumtia hatiani mshtakiwa na kutoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa alihitimisha hukumu hiyo kwa kuutalifu upande wa utetezi kuwa njia ipo wazi endapo watahitaji kukata Rufaa na kuongeza kuwa Mahakama yake ipo tayari kutoa nakala ya hati ya hukumu na mwenendo wa shauri hilo mapema iwezekanavyo baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.

Kwa mujibu wa adhabu zilizotolewa na Mahakama hiyo walionufaika kwa kuachiwa huru kutokana na udhaifu wa ushahidi wa tuhuma zilizo kuwa zikiwakabili ni pamoja na Salum Rashid Chibama aliyekuwa anatuhumiwa kwa tuhuma za mauaji ya bila kukusudia katika shauri la mauaji namba 6/2012 ambapo alidaiwa kuchoma nyumba moto na kusababisha kifo cha Mtoto Shadrack Hasani ambalo kiini chake ni tukio la fumanizi lililotokea katika
kijiji cha Muhuwesi Januari 4/2011.

Aidha Gotad Rufunda aliyekuwa anatuhumiwa katika Shauli la mauaji namba 4/2012 la tuhuma za kumuua marehemu Emmanuel Nyoni, Katika tukio lililo tokea Wilayani Namtumbo Tarehe 28/06/2008 aliachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kumwunganisha na
shtaka la mauaji.

Walionufaika na Rufaa zao kwa kuachiwa huru ni pamoja na Hasan Rajabu ,Kiwembe Kampose na Hamad Wajika Jamshid waliokuwa wanatumikia kifungo cha miaka 30 kila mmoja baaya ya Mahakama ya Wilaya ya Tunduru kuwatia hatiani kwa kosa la Wizi wa kutumia Silaha kinyume cha sheria namba 294 (A) kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002 ambapo ilidaiwa kuwa kwa pamoja waliiba kwa kutumia silaha na baada ya kuiba walimtishia kumchoma Kisu askari (mstaafu) wa Jeshi la wananchi Abbas Husein katika tukio lililotokea February 13/2011.

Kesi nyingine iliyotolewa maamuzi ya aina hiyo ni ya Rufaa namba 4A/2012 wakata rufaa wakiwa ni Alex Steven Chipasula, Lazack Ally Jaza na Rashid Kamwana walikuwa wanatumikia kifungo cha miaka 11 kila mmoja wao baada ya Mahakama ya Wilaya hiyo kuwatia hatiani katika makosa mawili likiwemo la kuvunja na kuiba Seti ya TV na deki vyote
vikiwa na thamani ya Shilingi 900,000 mali ya Afisa utumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo Christina Kumwenda katika tukio lililo tokea usiku wa manane agosti 19/2011.

Rufaa ya mwisho iliyotolewa maamuzi hayo na Mahakama hiyo ni Namba 7/2011 iliyokatwa na Said Hamidu Manyiru ambaye alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 6 na Mahakama ya Wilaya baada ya kumtia hatiani kwa kosa la wizi wa pikipiki yenye namba za Usajiri T 772 EAD
mali ya Erasmo Damian iliyokuwa ameegeshwa katika yadi ya Idara ya Ujenzi Wilayani humo ambapo maelezo ya shauri hilo yalidai kuwa, Manyiru alibambwa na walinzi wa idara hiyo akitaka kuondoka na Pikipiki hiyo Mei 16/2011.

Wakizungumzia adhabu hizo Mwanasheria msomi wa Serikali Wilbroad Ndunguru mbali na kukiri Jamhuri kufanya vibaya katika kesi hizo alisema kuwa kuanguka huko kumetokana na mapungufu ya kiushahidi ulioandaliwa na kutolewa Mahakamani huku Wakili wa kujitegemea .
Dickson Ndunguru alidai kutoridhishwa na adhabu ya kunyogwa hadi kufa
iliyotolewa dhidi ya mteja wake nikubwa mno na akaahidi kukata rufaa.

Upande wa Zuberi Kipande ambaye ni Baba mzazi wa mtuhumiwa aliyehukumiwa adhabu ya Kifo cha kunyongwa alipotakiwa kuzungumzia adhabu hiyo aliongea kwa uchungu kuwa kitendo cha kutenganishwa na mpendwa wao huku wakiwa hawajui mwili wake utazikwa wapi baada ya adhabu hiyo kutekelezwa kimewauma sana.



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top