BAADHI ya wanafunzi wa shule ya
sekondari ya De Paul inayomilikwa na kanisa la katoliki jimbo kuu la Mbinga
mkoani Ruvuma wamekumbwa na ugonjwa unaodaiwa kuwa ni wa ajabu ambao umekuwa
ukiwasababibishia kuweweseka na baadhi ya viungo vya miili yao kupooza.
Habari zilizopatikana kutoka
kwenye shule hiyo ambayo ipo umbali wa kilometa 15 kutoka Mbinga mjini zimesema
kuwa siku tatu zilizopita dalili zilianza kuonekana kwa baadhi ya wanafunzi
ambao baadae hali zao ziliendelea kuwa mbaya na uongozi wa shule ulilazimika
kuwakimbiza kwenye hospitali ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya kupata matibabu
ambapo wanafunzi tisa kwa mara ya kwanza walikumbwa na ugonjwa huo wa
kuweweseka na kupooza baadhi ya viungo vya miili yao.
Habari zaidi ambazo zimeelezwa na
baadhi ya wanafunzi na walimu ambao wameomba majina yao yahifadhiwe zilisema
kuwa siku ya pili wanafunzi wengine saba walibainika kuwa na tatizo hilo nao
walipelekwa katika hospitali ya serikali ya wilaya kwa matibabu ambako kati yao
walilazwa na wengine waliruhisiwa kurudi kwa nyumbani kwa wazazi wao.
Hata hivyo jitihada za kuupata
uongozi wa shule hiyo ziligonga mwamba baada ya kutopatikana kwa simu zao za
mikononi ambapo jitihada zilifanywa za kumpata mganga mkuu wa wilaya ya Mbinga
Dr. Damas Kayela ambaye alikiri kuwapokea wanafunzi kumi na sita ambao
waliletwa wakiwa wanaumwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Dr. Kayela alifafanua zaidi kuwa
baada ya kuwapokea wagonjwa hao jopo la madaktari lilianza kuwahudumia kwa
kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na matatizo yaliyokuwa yanawakabiri lakini
baadae jopo la madaktari lililazimika kwenda kwenye eneo la shule ya De Paul
ambapo walipofika waliwakuta wanafunzi wengine sita wakiwa wanasumbuliwa na
tatizo hilo kasha walitoa huduma kwa kuwasaidia na baadaye iligundulika kuwa
tatizo lililowakumba wanafunzi hao ni la ugonjwa wa kuchanganyikiwa na kulegea
mwili.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya
Mbinga Senyi Ngaga alipohojiwa kuhusiana na tatizo hilo lililotokea kwenye shule
ya sekondari ya De Paul ambayo ipo katika kijiji cha Mbangamawe alithibitisha
kuwa wanafunzi ishirini na mbili wa shule hiyo waligungulika kuwa na ugonjwa wa
kuchanganyikiwa na kulegea mwili na kwamba kwa sasa hivi wataalamu wa afya
wakiwemo madaktari walishakwenda kwenye shule hiyo kutoa ushauri zaidi kwa
wanafunzi na uongozi wa shule hiyo.
Ngaga alifafanua zaidi kuwa
tatizo la wanafunzi kukumbwa na ugonjwa huo tayari ofisi yake imeshaweka mikakati
ya kuhakikisha kuwa linakwisha na vile vile ameiagiza timu hiyo ya wataalamu
kufanya utafiti zaidi na ikiwezekana hata kwa shule zingine za sekondari za
wilaya hiyo ziepukane na kukumbwa na ugonjwa huo ambao unawanyemelea zaidi
wanfunzi wa kike.
Post a Comment