Loading...

Picha na habari: Yaliyotokea kijijini Msimbati, Mtwara

Ya awali ni maelezo ya Mhariri wa blogu ya ‘Kusini’ na inayofuatia ni ya bwana Samli, wote wapo Mtwara, wanaripoti kuhusu taarifa za gari linalosadikiwa kuwa lilikuwa limeandaliwa kwenda kumchukua Bibi Somoye Issa (90) ambaye ni Mkuu wa Kaya aliyetoa kauli kuwa gesi ikisafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, itageuka kuwa maji, kuchomwa moto usiku wa jana huko kijijini Msimbati, Mtwara. Kijiji cha Msimbati ndicho ambacho miradi ya kuvuna gesi asilia imesimikwa.Pichani juu ni Mhariri wa blog ya Kusini akitizama mabaki ya gari lililochomwa moto huko Msimbati.                                                 Pichani juu Bibi Somoye Issa (90).

Kwa mujibu wa wanakijiji hao, Mtu huyo ambaye ana asili ya kijiji hicho waliyemtambua kwa jina la Seleman Babu aliwasili kijijini hapo jana saa 10 jioni akiwa na gari ndogo aina ya Mark II na kwenda nyumbani kwa shangazi yake.

Habari zinadai kuwa saa 2 usiku Babu, alikwenda nyumbani kwa Bibi Mtiti akiwa na gari pamoja na shangazi yake aliyetajwa kwa jina la Fatuma Saidi Tom.

Mkazi wa kijiji hicho, Juma Ayoub alisema: “Unajua yule bibi tunamlinda, sasa ilipoonekana ile gari usiku pale, watu wakaanza kujiuliza linafanya nini? Wakaanza kusogea, kadiri muda ulivyokwenda ndivyo watu walivyozidi kuongezeka.”

Asha Hamisi, mtoto wa pili wa Bibi Mtiti, akihadithia juu ya tukio hilo alisema yapata saa 2 usiku wakiwa wanakula chakula alipokea wageni wawili ambao baada ya kumaliza kula waliomba kuongea na Mkuu huyo wa Kaya. “Alikuja kijana na mama wakaniomba kuongea na bibi... Alimuliza bibi kama ana uwezo wa kwenda Mtwara, bibi akajibu hawezi... Wakaniuliza mimi kama naweza kwenda badala yake nikawaambia siwezi... Akasema ametumwa na Rais Jakaya Kikwete na Hawa Ghasia wamjie bibi wakazungumze naye mambo ya gesi... Alisema kama bibi yupo tayari Jumanne ijayo watamfuata kwa gari, mimi nikasema sitaki, nilipochungulia nje nikaona watu wengi wamezunguka.”

Manzi Mohamedi Faki mtoto wa tano wa Bibi Mtiti anasimulia: “Kwa kuwa tunamfahamu tulimwambia aondoke mpango aliojia haufai, akawa anabisha, tukaendelea kumsihi, wakati huo watu wanazidi kuongezeka, alipotoka akakosea njia, alipopita hakukuwa na njia, watu walimfuata wakaanza kumrushia mawe, aliacha gari akakimbia, ndipo wananchi walipoliteketeza gari kwa moto.”

Fatuma Tom ambaye ni shangazi wa Babu amethibitisha kumpokea mwanae huyo na kumsindikiza kwa Bibi Mtiti na ambako alimuomba mkuu huyo wa kaya akubali kuondoka nae kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ametumwa na viongozi wake wa juu: “Ni mwanangu mtoto wa kaka yangu, alikuja akaniomba nimepeleke kwa bibi akamsalimie tuliondoka saa 2 usiku…watu walituzingira na hali ilipokuwa mbaya niliondoka na kumwacha mwanangu pale, nae alikimbia na ndipo walipochoma moto gari.... Huyu mwanangu anaishi Dar es Salaam, anafanya kazi usalama wa Taifa…nadhani alirudi jana hiyohiyo Mtwara.”

Mwenyekiti wa kijiji cha Msimbati, Salum Tostao alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ofisi yake haikupokea mgeni yeyote kutoka serikalini kwa siku hiyo: “Ni kweli gari imechomwa lenye namba za usajili T 609 BXG mali ya Mussa Babu…taarifa hii ni kwa mujibu wa nyaraka tulizookota kutoka ndani ya gari hilo.”

Selemani Babu alikanusha madai ya yeye kwenda kijijini hapo jana na alisema: “Hapana, hapana labda umekosea…na... na... na... umekosea… sijakwenda Msimbati jana… kwanini asiwe Mussa, umekosea sio mimi kwaheri.”

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki alisema hana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa mhusika hajaenda polisi kulalamika.Pichani juu ni Aisha Hamisi ni mtoto wa pili wa Bibi MtitiWananchi wakitizama mabaki ya gari lililochomwa moto

Baada ya majibizano ya hapa na pale kuendelea kwa muda mrefu baina ya Serikali, Wanaharakati na Wananchi wa Mikoa ya Kusini sasa inaonekana mgogoro huo kukua zaidi siku hadi siku. Ililipotiwa hapo kabla kuhusu Naibu Waziri wa Nishati kwenda usiku huko Msimbati na kufukuzwa, ingawaje Serikali kwa upande wake ilikanusha habari hiyo na kudai ni maneno ya kizushi na udanganyifu wa watu kujitafutia umaarufu.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni hatari, asubuhi ya leo tumepata taarifa kwamba gari lililoenda kwa ajili ya kumbeba Bibi kwenda naye kusikojulikana limechomwa moto. Taarifa zinasema, watu kadhaa akiwemo kijana mmoja mwenye asili ya ukaazi wa kijiji hicho walikamatwa jana usiku na wanakijiji cha Msimbati wakidai wameagizwa kuja kumchukua Bibi huyo ili wakafanye maongezi na Wakubwa ambao pia hawakuweza kuwekwa bayana ni Wakubwa gani hao. Kinachoelezwa ni kwamba, baada ya mtafaruku huo, watu hao walichoropoka na kukimbia kitu kilichowapa hasira wananchi na kuamua kuchoma gali hilo ambalo walikuja nalo.

Wananchi hao wamesema wako tayari kumlinda Bibi huyo usiku na mchana kwa kuhofia kurubuniwa na Serikali ili abadili msimamo wake.

Ni hatari, kwa sababu mbali na propaganda za viongozi wetu wa Kitaifa kwamba suala la gesi ni la Wanamtwara Mjini tu; Kwamba wenyewe wa Msimbati na Mtwara Vijijini kwa ujumla wako tayari gesi hiyo kupelekwa Dar es salaam, si kweli. Leo hii, wale wanaodaiwa kuwa tayari kuruhusu gesi hiyo wameteketeza gari, je wale wasio tayari kwa hilo kesho watafanya nini?

Serikali isidharau wananchi na wale wenye matakwa mema na nchi hii, kwani mbali na mamlaka ambayo serikali imepewa katika kusimamia rasilimali za nchi, bado uhalali wa wamiliki asilia wa rasilimali hizo ambao ni wananchi hauwezi kuporwa. Wananchi wanaozungukwa rasilimali husika ndio wamiliki halali wa rasilimali hizo kabla ya Serikali na jamii zingine za nchi. Hivyo wanufaika wa kwanza wa rasilimali husika ni lazima wawe ni wale wenye uhalali wa Ki-asili na si vinginevyo.

Tuache dharau!

Leo gari limechomwa, kama hii hali itaendelea kuwa hivi, tusishangae kuambiwa kuna mtu pia kachomwa au kapoteza maisha kwa sababu hizi hizi zinazofanyiwa masihara na viongozi wetu.

Tuweni wazalendo, tutetee maendeleo ya nchi na watu wake kwa vitendo, tuache porojo.


Chanzo:  http://www.jamiiforums.comPost a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top