BAADHI
ya wateja wa shirika la umeme Tanzania (Tanesco) wa halmashauri ya Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma wamelalamikia kutopata huduma ya umeme kwa zaidi ya
wiki moja jambo ambalo limesababisha baadhi ya maeneo kwa nyakati za usiku
kuwa giza totoro.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari wakazi hao walieleza adha
wanayoipata baada ya Tanesco kushindwa kutoa huduma ya umeme kwenye maeneo
wanayoishi ambapo walidai kuwa kuanzia mwanzoni mwa wiki iliyopita hadi sasa
umeme haupatikani kabisa hasa katika maeneo ya F.F.U
Mahenge,Makambi,Seedfam,Mji mwema na Matogoro.
Akizungumza
kwa jazba Ally Said Mkazi wa Makambi alisema kuwa tatizo la kutokuwepo kwa
umeme kunawakwamisha kufanya shughuli zao za kila siku za maendeleo kwani
yeye anategemea kupata kipato chake kupitia biashara yake ya saluni
hivyo ameliomba shirika hilo lichukuwe hatua za haraka kurudisha huduma hiyo
kwenye eneo la Makam
Alphonsi Kapinga alisema kuwa shirika la
Tanesco ni vyema linapotokea tatizo wakawatangazia wananchi ili waweze kujuwa
tatizo kuliko kukaa kimya wananchi wanashindwa kujuwa tatizo ni nini jambo
ambalo linawafanya wakose imani na shirika hilo.
Aidha
hiyo pia imewakuta akina mama na watoto ambao walikuwa wanaangaika kutafuta
huduma ya kusaga nafaka kwenye mashine zinazotumia umeme jambo ambalo
limewalazimu kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo na shughuli
zingingine za nyumbani kukwama .
Amina ally mkazi wa F.F.U Mahenge alisema
kuwa bajeti ya nyumbani kwake imeongezaka kutokana na kununua baadhi ya
mahitaji kama unga ambao ananunua kilo moja sh.1500na mchele kilo moja
sh.2500 wakati nyumbani kwake anayo magunia ya mahindi na mpunga ambavyo
anashindwa kwenda kusaga kutokana na kukosekana kwa umeme.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti alipohojiwa na waandishi wa
habari kwa njia ya simu amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kutokana na baadhi ya
mashine kuharibika na mtaalamu wa kutengeneza mashine hizo muhandisi Steven
Manda ambaye pia ni kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma yupo nje ya mkoa
kwa shughuli za kikazi.
Hata
hivyo waandishi wa habari walipowasiliana kwa njia ya simu na kaimu Meneja wa
Tanesco Ruvuma Mhandisi manada kufuatia kuwepo kwa kero kubwa kwa baadhi ya
maeneo mjini Songea alisema kuwa pamoja na kujitokeza kwa tatizo hilo la
kutopatikana kwa umeme lakini alidai kuwa yeye si msemaji na badala yake
alieleza kuwa msemaji wa shirika yupo makao makuu ya Tanesco jijini Dar es
salaam.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alipohojiwa kwa njia ya simu
na mwandishi wa gazeti hili alisema kuwa kweli kuna tatizo la kiufundi kubwa
ambalo limejitokeza kwenye mashine za kufua umeme hivyo wamewasiliana na
Tanesco makao makuu na tayari wameshatuma mafundi kuja kutengeneza mashine
hizo na zitachukuwa siku nne hadi kuja kukaa sawa
Aidha
hivi karibuni serikali ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na Wilaya zake ilitangaza
mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) ndani ya miaka
saba kuwa imeweza kuboresha huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo miundo
mbinu ya barabara, afya,maji,kilimo ,elimu pamoja na umeme ambao katika
manispaa ya Songea ulikuwa sio wa uhakika kwa sababu ya ubovu wa mitambo ya
kufulia umeme.
Post a Comment