Loading...

mwanaume auwawa akitokea msikitini kuswali

MHAMEDI Mwanyali (65) maarufu kwa jina la Fereji mkazi wa kijiji cha Namwinyu kilichopo katika wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma amekutwa kichakani akiwa amevuliwa nguo huku akiwa na jeraha kichwani baada ya kuuwawa na watu wasiofahamika.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Desdedit Msimeki ameongea leo mchana ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tano usiku huko katika eneo kati ya vjijiji vya Namwinyu na Darajambili wilayani Tunduru ambako inadaiwa mwili wa Mwanyali uligunduliwa na wanavijiji hivyo ambao walikuwa wakimtafuta baada ya kutoonekana nyumbani kwake tangu alipoaga kuwa anaenda msikitini kuswali majira ya saa tano asubuhi.

Alisema kuwa inadaiwa wanavijiji hao waliukuta mwili wa Mwanyali ukiwa umetelekezwa kwenye eneo la kichaka baada ya kuuwawa na watu wasiofahamika katika eneo pamoja na eneo lisilojulikana ambako mauaji hayo yalifanyika.

Alifafanua zaidi kuwa Mwanyali alikutwa na jeraha kubwa kichwani linaloonesha wazi kuwa alikatwa na kitu chenye ncha kali na alikuwa amevaa shati na sehemu zingine za mwili akiwa uchi wa mnyama na kwamba nguo alizokuwa amevaa wakati anaondoka nyumbani kwake kuelekea msikitini haijafahamika mahali zilipo mpaka sasa.

Kamanda Msimeki alibainisha zaidi kuwa katika uchunguzi wa awali wa polisi imebainika kuwa Mwanyali aliondoka nyumbani kwake juzi majira ya saa tano asubuhi kwenda msikiti wa darajambili kuswali kama kawaida yake kila siku kwenda msikitini akiwa amevaa shati, suruali, kanzu na kandambili.

Alieleza kuwa inadaiwa kuwa Mwanyali alikuwa hana kawaida ya kuchelewa kurudi nyumbani kwake mara baada ya ibada lakini siku hiyo hakuonekana nyumbani kwake hadi ilipofika majira ya saa mbili usiku ndipo mke wake aliposhtuka na kuwatuma watoto wake wamfuate msikitini huko katika kijiji cha Darajambili ambacho kipo umbali wa kilomita tatu toka nyumbani kwake.

Alisema kuwa watoto hao walipofika kwenye kijiji hicho, wakaenda moja kwa moja msikitini kumwuulizia ambapo walimkosa kisha walitoa taarifa kuwa Mwanyali hajaonekana nyumbani tangu majira ya asubuhi pindi alipoaga anakwenda msikitini na juhudi za kumtafuata zilianza kwa kushirikiana na uongozi wa serikali za vijiji vya Namwinyu na Darajambili na kufanikiwa kuukuta mwili wa marehemu ukiwa kwenye kichaka ambacho kipo katikati ya vijiji hivyo.

Hata hivyo kamanda Msimeki alieleza kuwa chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na kwamba hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na polisi inaendelea kufanya upelelezi wa kina ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top