VIONGOZI na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walifanya maandamano na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara uliofanyika Temeke, jijini Dar es Salaam ambako chama hicho kilitangaza nia ya kuandaa hoja ya kuwang’oa viongozi wa Bunge.
Hoja hiyo itawasilishwa katika mkutano ujao wa
Bunge kwa ajili ya kuwapigia kura za kutokuwa na imani na Spika wa
Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kwa madai ya kukwamisha
mijadala yenye masilahi ya wananchi bungeni.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Uwanja wa Temeke Mwisho, Dar es Salaam, wabunge wa chama hicho
wakiwa na uongozi wa juu, waliwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo
kujiandaa na maandamano ya kuwang’oa spika hao.Kana kwamba hiyo
haitoshi, wabunge hao walitangaza namba za simu za viongozi hao wa Bunge
ili wananchi wazitumie kuwashinikiza wang’oke.
Akihutubia katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe alisema Spika Makinda ameshindwa
kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha
nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu
(Epa).
Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto aliyekuwa
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti
ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia masilahi ya wananchi.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi
waliohudhuria mkutano huo, Zitto alitaja mbinu za kumng’oa Spika Makinda
akisema kuwa hoja hiyo imeshakamilika.
“Kuna njia za kumng’oa Spika Makinda, kwanza kwa
kupeleka hoja ya kutokuwa na imani naye na nimeambiwa hapa kwamba
imeshakamilika. Au tuandamane hadi pale Shule ya Msingi Bunge… au
tutumie namba zake kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…”
alisema Zitto na kumruhusu Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kutaja
namba za Spika Makinda na Naibu wake.
Baada ya kutaja namba hizo wananchi walionekana wakizipiga na wengine kutuma ujumbe wa simu.
Mwananchi lilipompigia simu Spika Makinda, simu yake ilikuwa inaita, kisha inakatika bila kupokewa.
Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto alisema:
“Kamati hii iliundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Spika
Samuel Sitta kwa ushauri wa kina Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu
Chadema), waliona kuwa haiwezekani nchi yenye zaidi ya mashirika 200
yenye thamani ya zaidi ya Sh10 trilioni yasidhibitiwe na Bunge…Lakini
Serikali ya CCM ikaona upinzani umepata sehemu ya kuzungumzia, sasa
wameifuta,” alisema Zitto.
Alitaja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni
utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni
kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo
Kikuu cha Arusha.
“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni
msimamizi tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Makinda
lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” alisema Zitto.
Mnyika alia na Maghembe
Katika mkutano huo, Mnyika alitoa wiki mbili kwa
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuwa ameshughulikia matatizo ya
maji kwa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema kutokana na hoja aliyoiwasilisha katika
kikao kilichomalizika mwishoni mwa wiki bungeni kuondolewa, analitaka
Bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la
Dar es Salaam.
“Natoa wiki mbili kuanzia leo (jana) Waziri wa
Maji (Maghembe) awe ameeleza hatua anazochukua kuhakikisha hali ya
upatikanaji wa maji kwa Dar es Salaam,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Asipofanya hivyo tutaandamana kwenda wizarani kwake kumshinikiza kutekeleza yale ambayo alisema yanaendelea,” alisema.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa chama hicho, Dk
Slaa alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
kueleza hatua ambazo amefikia katika ufuatiliaji wa mabilioni
yaliyofichwa nchini Uswiss.
Alisema watuhumiwa wa fedha hizo ndiyo vigogo
katika Serikali, ndiyo maana hakuna jitihada zozote zinazofanyika
kuhakikisha fedha hizo zinarudi.
Ahadi ya Mbowe
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema kuwa ule mtindo wa wabunge wa chama hicho kususia
vikao vya Bunge hautakuwepo tena badala yake wataendelea kupiga kelele
ndani ya Ukumbi wa Bunge ili mikutano iahirishwe.
“Tulikuwa tunatoka nje ya Bunge, watu wakawa
wanasema kuwa hatukuwachagua ili mkatoke nje, kwanza ni sawa na
kumwachia nguruwe shamba la mahindi…Sasa hatutoki, tutakuwa tunakomaa na
kupiga kelele hadi hoja zetu zisikilizwe… kama noma na iwe nomaa… kama
noma na iwe nomaaa…” alisema Mbowe huku akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande mwingine Mbowe aliilaumu Serikali kwa kukusanya kodi nyingi kila mwaka lakini haijali mahitaji ya wananchi.
“Kwa kipindi cha Desemba 2011 hadi Desemba 2012 Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete imekusanya kodi ya Sh900 bilioni. Zote wanapeleka
hazina, kisha wanakaa vikao Dodoma na kula na kustarehe. Watoto wetu
wanashindwa kwenda shule…” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kwa upande wa madini, asilimia 60 sawa na Sh256
bilioni iliyokusanywa kama kodi inatokana na wachimbaji wadogo kama ‘Pay
as you earn’ (kwenye mishahara), wakati kampuni kubwa zimelipa Sh56,000
bilioni za kodi. Hivi wananchi mnasubiri nini? Mapambano haya hayatoshi
bungeni tu, ndiyo maana tumekuja kwa wananchi hadi kieleweke.”
Mapokezi ya wabunge
Wabunge wa Chadema wakiongozwa na Mbowe
walipokelewa majira ya saa nne asubuhi ambapo magari ya chama hicho na
idadi kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam walijikusanya kwa ajili ya
kujiunga na msafara ulioanzia maeneo ya Riverside, Ubungo mpaka Uwanja
wa Temeke Mwisho.
Shamrashamra za kuwapokea viongozi hao,
zilifanyika mpaka majira ya saa 7.00 mchana baada ya kuwasili katika
eneo hilo tayari kwa msafara wa kuelekea kwenye uwanja huo.
Magari zaidi ya 70 yaliyokuwa kwenye msafara huo
yaliyokuwa yamefurika katika Barabara ya Mandela kwa takriban saa tatu
huku magari ya John Mnyika, Tundu Lissu, Zitto Kabwe na Godbless Lema
yakivamiwa kwa furaha na wakazi hao katika kona ya kuingia Tandika.
Post a Comment