MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ametoa siku 14 kwa wazazi wenye watoto waliochaguliwa kujiunga na masomo ya
kidato cha kwanza Januari mwaka huu katika shule za sekondari ambao mpaka sasa
hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa
na wahakikishe kuwa wanawapeleka shuleni watoto hao haraka iwezekanavyo.
Mwambungu amelitoa agizo hilo jana mchana ofisini kwake
wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara aliyoifanya
kwenye baadhi ya shule za sekondari kila Wilaya mkoani humo ambako amegunduwa
kuwa nusu ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mkoani humo
mpaka jana hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.
Alisema kuwa jumla ya
wanafunzi 16,578 walichaguliwa kuanza masomo ya sekondari Januari mwaka huu
lakini kati ya hao walioripoti ambao hivi sasa wanaendelea na masomo 9,388 na
wanafunzi 7190 ambayo sawa na asilimia 56.6 hawajaripoti kwenye shule
walizopangiwa.
Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa katika ziara ya kushtukiza
aliyoifanya kwenye baadhi ya shule amegunduwa kuwa idadi ndogo ya wananfunzi
ambao wapo madarasani wanaendelea na masomo na wanafunzi wengine hawajulikani
wapo wapi jambo amblo limepelekea kuwepo na hofu kubwa kwa wazazi wa wenye
watoto kutoona umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shuleni.
Alitoa mfano wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa
na kujiunga na masomo ya sekondari mwaka katika shule ya Sekondari ya
Barabarani iliyopo Wilaya ya Songea vijijini ambapo wanafunzi 20 walipangwa
kuripoti lakini hadi jana ni wanafunzi wawili tu ambao wameripoti shuleni hapo
hali ambayo imemtisha mkuu huyo wa Mkoa.
Amezitaja shule zingine za sekondari ambazo wanafunzi
hawajaripoti kwa kiwango kinachostahili ni pamoja na sekondari ya serikali
ya kutwa ya Mtutura iliyopo wilayani
Tunduru kuwa walipangwa wanafunzi 159 kati ya hao walioripoti ni wanafunzi 22
na kwamba 137 hawajaripoti na hawajulikani walipo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo iliyojitokeza amewaagiza
wakuu wa Wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za Wilaya na
Manispaa,wenye viti wa halmashauri pamoja na maafisa elimu wa sekondari
wahakikishe kuwa wanafuatilia kwa karibu wazazi wa watoto waliochaguliwa
kujiunga na masomo ya sekondari mwaka huu na amewataka Hadi ifikapo Machi moja
mwaka huu wawe wameshafika kuripoti kwenye shule walizopangiwa na kuanza masomo
mara moja.
Amewaonya wakuu wa shule za sekondari za serikali kuacha
mara moja tabia ya kuwarudisha watoto nyumbani kwa madai kuwa wameshindwa
kulipa ada na michango na kwamba watakao bainika watachukuliwa hatua mara moja
na si vinginevyo pia wazazi wa wanafunzi ambao watoto wao watashindwa kuripoti
kwenye shule walizopangiwa watakamatwa na kufikishwa mahakamani mara moja .
Hata hivyo Mwambungu amewaonya baadhi ya watu wenye tabia
chafu ya kufanya mapenzi na wanafunzi wa kike na kuwasababishia washindwe
kuendelea na masomo kwa mfano shule ya sekondari Nasuri iliyopo wilayani
Namtumbo wanafunzi 14 wamekatishwa masomo kutokana na kupata ujauzito pamoja na
shule ya sekondari ya serekali ya kutwa ya Lukara iliyopo Songea vijijini
wanafunzi 12 wamebainika kuwa ni wajawazito.
Post a Comment