MBUNGE wa Jimbo la Peramiho Wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma
Jenista Mhagama ametoa msaada wa vitanda sita na magodoro sita wenye
thamani ya sh.milioni 1.7 kwaajiri ya akina mama wajawazito katika
zahanati ya kijiji cha Nambendo ambacho kiko mpakani mwa Tanzania na
Msumbiji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi ya mwenyekiti
wa halmashauri ya Wilaya ya Songea Diwani wa kata ya Ndingosi Visenti
Komba alisema kuwa mbunge wa jimbo hilo ametekeleza ahadi yake aliyokuwa
ameitoa kwa wananchi wa kijiji hicho wakati alipokuwa amewatembelea
ambako aliahidi kuhakikisha kuwa anawasaidia akina mama wajawazito.
Alisema kuwa Mbunge huyo ametoa msaada wa vitanda sita vyenye
thamani ya sh. milioni 1.5 pamoja na magodoro sita yenye thamani ya
sh.210,000 na kwamba msaada huo umewafurahisha kwa kiasi kikubwa wakina
mama wajawazito ambao wamekuwa wakienda kusubiri kujifungua kwenye
zahanati hiyo ambayo hapo awali ilikuwa na vitanda viwili tu.
Diwani Komba alieleza kuwa pamoja na kupokea msaada huo kutoka kwa
mbunge bado zahanati hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madawa pamoja
na vifaa tiba na vitendea kazi jambo ambalo linawalazimu kutembea umbali
wa kilomita 43 kwenda kupata huduma hiyo katika kijiji cha ndongosi
ambako kuna zahanati inayomilikiwa na kanisa katoliki jimbo kuu la
Songea.
Alieleza kuwa tayari wananchi wa kijiji hicho walishajenga wodi
mbili kwaajiri ya kujitazamia akina mama wajawazito wakati wanatarajia
kujifungua hivyo wanaiomba serikali kupitia fedha za wafadhili (busket
fund) kuelekeza kwenye ujenzi wa wodi hizo ili ziweze kuboresha zaidi
miundo mbinu ya zahanati hiyo.
Hata hivyo Diwani wa kata hiyo Komba amemshukuru mbunge Jenista kwa
msaada mkubwa alioutoa kwa wananchi wa kijiji cha Nambendo ambacho kipo
mpakani mwa Tanzania na Msumbiji na kipo mbali na kituo cha afya cha
Muhukuru.
Kwa Upande wake wananchi wa kijiji hicho wamempongeza mbunge
Jenista kwa kuona umuhimu wa kuwaletea vitanda pamoja na magodoro kwani
wanawake wengi wamepoteza maisha kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba
na vitendea kazi katika zahanati hiyo.
Post a Comment