Loading...

Walemavu Ruvuma Watoa Maoni Katiba Mpya

WATU wenye ulemavu mkoani Ruvuma wamependekeza madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vyema yapunguzwe kwani kwa muda mwingi inaonekana Rais amekuwa akielemewa na kazi nyingi sana ambazo zingeweza kufanywa na waziri mkuu wa nchi.

Watu hao wenye ulemavu walitoa mapendekezo yao  kwenye semina iliyoendeshwa kwa muda wa siku mbili chini ya mradi wa kuhamasisha  watu wenye ulemavu katika mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya uliofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la “Foundation for Civil Society” la jijini Dar es Salaam iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa SACCOS ya wafanyakazi wa Halmashauri ya manispaa ya Songea.

Mjumbe wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) mkoani Ruvuma Henry Chaima alisema kuwa katiba mpya ni lazima iweke bayana kuona kazi anazozifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aweze kupunguziwa madaraka ambayo yatamwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo amekuwa akielemewa na kazi nyingi sana.

Alipendekeza kuwa Rais awe na madaraka ambayo hayamsababishii usumbufu zaidi mfano, uteuzi wa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Maspaa na Majiji ufanywe na Waziri Mkuu ambaye ni mtendaji mkuu wa serikali na kwamba mawaziri wasiwe wabunge.

Asia Abdallah ambaye ni katibu wa CHAVITA mkoa wa Ruvuma ameomba katiba mpya iweke bayana lugha kwa watu wenye ulemavu wa kutosikia kwani lugha ya wasiosikia ni ngumu kuielewa hasa kwa watu wenye ulemavu wa kutosikia kutokana na uhaba wa shule maalumu kwa watu wasiosikia.

Naye Kelvin Vicent ambaye ni Mwenyekiti wa CHAVITA mkoa wa Ruvuma amependekeza kuwa kwenye katiba mpya ijayo kuoneshe wazi uwepo wa mgombea binafsi wa nafasi ya urais kwani kuna watu wengine ambao ni watanzania wenye sifa nzuri za kuiongoza nchi lakini si wanachama wa chama chochote cha siasa jambo linalowafanya wakose sifa ya kugombea.

Amebanisha zaidi kuwa vilevile mikataba ya nchi iwe wazi kwa wananchi mfano ardhi na mikataba ya biashara mbalimbali ya kimataifa na pale inapogundulika kuwa mahali fulani pana madini wananchi wa maeneo hayo ni vema wakashirikishwa ili kujua namna zoezi la uchimbaji wa madini hayo litavyondeshwa na wao wakafahamu faida watakayoipata kutokana na uchimbaji huo.

Aidha, wameitaka katiba mpya iseme wazi juu ya miundombinu ya walemavu wa aina zote na kwamba vyama vya walemevu vipatiwe ruzuku na kuwepo na uwakilishi mzuri Bungeni kwa asilimia therathini kama inavyofanywa kwenye jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Vijana, uwakilishi wa vyuo vikuu na wabunge wa viti maalumu.

Wamesema muungano wa nchi ya Tanzania uvunjwe na badala yake uwe wa serikali tatu yaani serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano kwani kwa muungano tulionao kwa hivi sasa watanzania wengi bado hawajauelewa kinachoshangaza Zanzibar wana serikali yao yenye  maamuzi kamili tofauti na serikali ya Muungano.

Iko haja kwa sasa katiba mpya itamke kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asitokane na chama chochote cha siasa na badala yake nafasi hiyo itangazwe ili watu wagombee kama wanavyogombea ubunge kuondoa utata unaojitokeza kwenye vikao vya Bunge.Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top