Jeraha katika mwili wa Castor Sote Yawamba ambapo risasi ilipenya na kisha kutokea mgongoni hadi kusababisha umauti wake.
Marehemu Castor Sote (Kushoto) enzi za uhai wake, akiwa na Babu yake Laiti Yawamba.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitulo wakilia baada ya kuuona mwili wa mwalimu wao marehemu Castor Sote Yawamba.
Mama wa Marehemu Castor (Mwenye kitambaa chekundu kichwani) akilia mwili ulipokuwa nyumbani kwake eneo la Mbalizi Mbeya Vijijini.
Jeneza la mwili wa marehemu likibebwa ili kuingizwa kwenye gari tayari kwa safari ya kwenda kijijini Jojo Kata ya Santilya Mbeya Vijijini kwa mazishi.
Waombolezaji wakishiriki katika mazishi ya marehemu, mwalimu Castor Sote Yawamba
Mwili wa Marehemu, Castor Sote Yawamba ukiingizwa kaburini
Ibada ya Mazishi ikiendelea
Msemaji wa jeshi la polisi ambaye ni mkaguzi wa polisi wilaya ya Makete, Frank Chimale akitoa taarifa mbele ya waombolezaji juu ya kifo cha Castor Sote Yawamba na aliyeshika kinasa sauti ni mtangazaji wa Redio Kitulo ya Makete.
Hili ndilo kaburi la marehemu, Mwalimu Castor Sote Yawamba ambamo atapumnzika milele baada ya kuuawa kwa risasi.
Kesi ya askari, PC Joseph Gervas Konas mwenye namba G 9790, anayetuhumiwa kwa kosa la kummuua kwa risasi mwalimu Castor Sote Yawamba aliyetoka kuchukua hela katika Benki ya NMB tawi la Makete itatajwa kesho katika Mahakama ya Wilaya ya Makete.
Habari hizi ni kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zilizowafikia ndugu wa Marehemu Castor Sote Yawamba, zilizodai kuwa kesi hii itatajwa siku ya Ijumaa tarehe 05/04/2013 lakini haitasikilizwa kwa vile Mahakama ya Wilaya haina mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi za mauaji ambazo kimsingi husikilizwa na Mahakama Kuu.
Aidha, habari zilisema zaidi kuwa mnamo tarehe 09/03/2013, Joseph Gervas Konas alifutwa rasmi kazi ya uaskari katika Jeshi la polisi kwa kosa la kulifedhehesha jeshi la polisi baada ya kufanya kosa la kuua kinyume na maadili ya kazi yake.
Baada ya kufutwa kazi, mtuhumiwa Konas alifikishwa mahakamani tarehe 11/03/2013 ambapo kesi yake ilitajwa na kisha akarudishwa mahabusu.
Mwalimu Castor Sote Yawamba aliuawa mnamo tarehe 27/02/2013 majira ya saa 12.45 jioni kwa kupigwa risasi na askari Joseph Gervas Konas aliyekuwa akilinda benki baada ya askari Konas kumtuhumu Marehemu Castor kuwa hakuvaa kofia maalumu wakati anaendesha pikipiki.
Awali kamanda wa mkoa wa Njombe, Kamishina Msaidizi wa polisi, Fulgency Ngonyani alisema askari hupelekwa kulinda benki ili kuzuia matukio yanayohatarisha usalama wa benki kwa kutovaa kofia maalumu wakati wa kuendesha pikipiki ni kosa lakini lilikuwa halihatarishi usalama wa benki.
Aidha, uchunguzi ulibaini kuwa kulikuwa na tabia ya askari kuwadai fedha wateja wanaochukua fedha zao ATM, benki ya NMB Tawi la Makete hali ambayo ilielezwa kusababisha usumbufu kwa wateja.
Akizungumzia suala hili Kamanda Ngonyani alikiri kupata taarifa hizi na kusema walipata taarifa kwa kuchelewa.
"Tumepata taarifa hizi ingawa tatizo la wananchi ni kuamua kusema wakati mambo yameshaharibika", alisema Kamanda Ngonyani.
Mwalimu Castor Sote Yawamba alikuwa anafundisha katika shule ya Sekondari Kitulo iliyopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.
Inawezekana umefika wakati sasa kwa jeshi la polisi kuona kama kuna haja ya kuanzisha vitengo maalumu vya saikolojia na sosholojia, kama havipo au
kuboresha vitengo hivi kama vipo ili jeshi liweze kuwabaini askari
wenye matatizo binafsi ya kisaikolojia na hata wawapo katika makundi
kisha kuyatafutia ufumbuzi kabla hayajasababisha madhara makubwa kwa jamii.
Post a Comment