MWANAFUNZI wa kidato cha sita
katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea mkoani Ruvuma amekutwa amekufa
baada ya kujinyonga kwenye mti uliopo kandokando ya njia kwenye eneo la milima
ya matogoro ya hifadhi ya msitu ya taifa nje kidogo ya manispaa ya Songea.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa
wa Ruvuma mrakibu mwandamizi wa polisi George Chiposi alisema kuwa tukio hilo lilitokea januari 21 mwaka
huu majira ya 12.30 asubuhi huko katika eneo la milima ya matogoro
Kaimu kamanda Chiposi alimtaja
mwanafunzi huyo aliyekutwa amekufa baada ya kujinyonga kuwa ni Ahabu Richard Ng’ondya
(21) wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea ambapo
alidai kuwa siku hiyo ya tukio watoto wawili ambao walikuwa wakipita njiani
majira ya saa za asubuhi ghafla waliona kama kuna mtu ananing’inia kwenye mti
mrefu ambao upo kandokando ya njia hiyo.
Watoto hao baada ya kuona hali hiyo
walikimbia na kukutana na mtu aliyejulikana kwa jina la Osward Kahongo
walimwonyesha tukio hilo ambaye nae pia aliwasiliana na polisi ambao walifika
kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari.
Alisema baada ya polisi kufanya
uchunguzi ulibaini kuwa alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana
ya Songea ambaye anadaiwa aliondoka kwenye eneo la shule katika mazingira ya
kutoroka siku chache kabla ya kutokea tukio hilo.
Alibainisha zaidi kuwa upelelezi
wa awali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha kujinyonga kwa mwanafunzi huyo ni
kwamba alikuwa amefukuzwa shule na uongozi wa shule baada ya kutofanya mitihani
ya majaribio hivyo uongozi uongozi wa shule ulimtaka arudi nyumbani kwao Matamba
Uwanji wilaya ya Makete mkoani Njombe ili akamlete mzazi wake.
Alieleza zaidi kuwa baada ya
kuambiwa hivyo mwanafunzi huyo alitoeka kwenye eneo la shule na kwenda
kusikojulikana hadi hapo alipokutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga, hata hivyo
alieleza kuwa mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Matamba Uwanji nyumbani
kwa wazazi wake kwa ajili ya mazishi.
1 comments:
Ni habari ya kusikitisha kwa kweli..pole wazazi na wanandugu wote ...
ReplyPost a Comment