Hatua hiyo ya Rais Banda ambayo tunaweza kuiita ya kukurupuka siyo tu imeishtua Tanzania, bali pia Afrika na dunia nzima kutokana na ukweli kwamba mazungumzo kuhusu mgogoro huo yalikuwa yakiendelea vizuri chini ya usuluhishi wa jopo la marais wa zamani barani Afrika chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano.
Lakini waliokuwa wakifuatilia mgogoro huo kwa karibu watakubaliana nasi kwamba nchi hiyo tangu mwanzo haikuwa na dhamira ya kumaliza mgogoro huo kwa mazungumzo au usuluhishi. Mara zote zilisikika kauli na sauti za viongozi katika serikali hiyo zikibeza juhudi hizo kwamba ni kupoteza muda tu. Tangu mwanzo mkakati wa serikali hiyo ulikuwa kupeleka mgogoro huo katika mahakama za kimataifa.
Ni jambo la kushangaza Rais Banda anaposema hatua ya nchi yake kujitoa katika mazungumzo ya usuluhishi imetokana na kuhujumiwa na katibu wa jopo la usuluhishi ambaye ni raia wa Tanzania, ambaye nchi hiyo inadai alivujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo. Kama kweli Malawi ilikuwa na ushahidi wa hujuma hizo kwa nini haikulifikisha suala hilo kwa mamlaka husika, ikiwamo kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya katibu huyo?
Mgogoro huo wa mpaka ni wa muda mrefu na unatokana na mikataba yenye utata iliyoachwa na wakoloni. Kwa kutambua hilo marais waliotangulia, hasa Bakili Muluzi na Bingu wa Mutharika wa Malawi na wenzao Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wa Tanzania, waliendeleza mazungumzo, kwani walitambua kwamba Ziwa Nyasa ni urithi wa wananchi wote wanaoishi katika nchi tatu za Msumbiji, Tanzania na Malawi na kwamba mazungumzo ndio suluhisho pekee la tatizo la mpaka.
Lakini kujitokeza kwa dalili za kuwapo mafuta katika Ziwa Nyasa na baadaye Rais Joyce Banda akaingia madarakani ndiko kulikosababisha Malawi isione tena umuhimu wa kuendelea na mazungumzo. Kwa maneno mengine, suala la mafuta ghafla liliichanganya na kuipofusha Serikali ya Malawi ambayo haikuona tena umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa masuala ya ujirani mwema.
Serikali ya Rais Joyce Banda bila kushauriana na Tanzania ilitoa leseni kwa makampuni mawili ya kigeni kutafuta mafuta katika eneo la Ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Hilo ndilo chimbuko la mgogoro uliopo hivi sasa ambao umechukua sura mpya baada ya upande mmoja wa mgogoro huo kupata ndoto za kuneemeka na mafuta.
Post a Comment