WAKATI mjadala wa kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi
wa kidato cha nne ukiendelea nchini, Waziri Mkuu mstaafu, Edward
Lowassa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume kuchunguza na kutoa
mapendekezo ya mfumo bora wa elimu nchini.
Alisema kwa hali ilivyo sasa mtu mmoja hawezi kujifungia ofisini peke
yake na kuja na mfumo wa kuboresha sekta ya elimu utakaokidhi matakwa ya
jamii.
Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.
Ingawa hakutaka kuzungumzia hoja ya mbunge wa kuteuliwa na Rais, James
Mbatia (NCCR- Mageuzi), aliyetaka Bunge liunde kamati kuchunguza
udhaifu katika sekta ya elimu na hoja hiyo kutupwa, Lowassa alisema
hakuna sababu ya kubishana kama tuna mitaala au la, lakini jambo la
msingi ni kuhakikisha tunapata sababu za matokeo mabaya ya wanafunzi wa
kidato cha nne.
“Sitaki kuzungumzia mjadala wa bungeni huyo anasema hatuna mitaala,
serikali inasema tunayo, hoja ya msingi zaidi ni kuangalia hii mitaala
ni sahihi, inatufaa? Mfumo wetu wa elimu ni mzuri?” alisema Lowassa na
kuongeza kuwa tume itakuja na majibu kama mitaala yetu ni sahihi na kama
inatufaa au la.
Akitolea mfano, Lowassa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, Waziri
wa Elimu wakati huo, marehemu Jakson Makweta, aliunda tume kuchunguza
mfumo wa elimu na ilikuja na majibu mazuri yaliyofaa kwa wakati ule na
sasa tunahitaji tume nyingine kuja na majibu ya wakati uliopo.
“Miaka ya nyuma, Rais Reagan wa Marekani wakati huo, aliunda tume
kuchunguza ubora wa elimu inayotolewa nchini mwake na tume hiyo ilikuja
na majibu yaliyofanyiwa kazi na leo hii Marekani ina mfumo mzuri na bora
wa elimu,” alisema Lowassa.
Alisema matokeo ya kidato cha nne mwaka huu, yanasikitisha na kama
taifa lazima tupate sababu za hali hiyo na kutafuta ufumbuzi.
Alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kuwa ni
pamoja na kuangalia namna gani serikali inawaangalia walimu kwa maana ya
mishahara na mazingira yao ya kuishi wawapo kazini.
“Matokeo ya kidato cha nne yamenisikitisha sana maana asilimia 60 ya
wanafunzi kupata ziro ni jambo la hatari. Na napenda kumsihii Rais
Kikwete kwamba amefanikiwa sana katika sekta nyingine kama barabara,
aunde tume kuchunguza sababu za wanafunzi kufeli, lakini kubwa kuliko
zote tume hiyo ije na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha mfumo wetu
wa elimu,” alisema Lowassa.
Alisisitiza kuwa hoja ya kutaka serikali iunde tume kuboresha mfumo wa
elimu, alipata kuitoa mara kadhaa kwani anaamini Elimu Kabla, Kilimo
Kwanza.
“Kila Mtanzania anasema lake, wengine wanasema ni hujuma, wengine
wanadai kuna mgomo baridi wa elimu, malalamiko na sababu ni nyingi na
njia pekee ya kujua ukweli ni kupitia tume,” alisema Lowassa.
Akizungumzia shule za kata alizoziasisi nchini nzima, alisema
anajivunia uwepo wa shule hizo hasa kutokana na mwitikio ambao wananchi
waliuonyesha wakati anazianzisha.
Alisema matatizo na changamoto zinazozikabili shule hizo ni bora zikatafutiwa ufumbuzi kupitia tume anayopendekeza ianzishwe.
Alisema shule hizo ni mkombozi kwa wananchi wanyonge na zimeleta usawa
na ni jambo la kujivunia kwamba ziko kwenye kila kata nchini.
“Hata hivyo kasi ya kuzihudumia shule hizo hatua kwa hatua imepungua
na sitaki kumlalamikia mtu, lakini ni bora zikaendelezwa kwa kukabiliana
na changamoto zake.
Mbali ya kuzungumzia anguko la elimu, Lowassa pia alizungumzia vurugu
za kidini zinazoendelea nchini, hususan kuuawa na kujeruhiwa kwa
viongozi wa kidini visiwani Zanzibar.
Aliwasihi Watanzania kutambua kuwa amani iliyopo ina maana kubwa kwani
zikianzishwa vurugu za kidini hakuna atakayebaki salama na hakutakuwa
na mshindi.
Wakati huohuo, Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), limeitaka serikali kutangaza matokeo ya mitihani ya kidato
cha nne yaliyotoka hivi karibuni kuwa janga la kitaifa kwa lengo la
kuliepusha taifa na fedheha ya kuzalisha kizazi cha watu wasiosoma.
Mbali na kutaka matokeo hayo kutangazwa kuwa janga la kitaifa, pia
baraza hilo limesema limeshaanza kuwasiliana na vijana waliofeli kutoka
maeneo mbali mbali ya nchi kwa ajili ya kuandaa maandamano ya kumtaka
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Katibu
Mtendaji wa Baraza la Mitihani Taifa (NECTA), Dk Joyce Ndalichako, na
Mkaguzi wa Elimu ya Sekondari nchini, waachie nafasi zao kwa madai kuwa
wameshindwa kusimamia majukumu yao.
Kauli hiyo iltolewa jana jijini Dar es Salaam, na Katibu Mkuu BAVICHA,
Deogratius Mushi, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea
kusikitishwa kwao na matokeo ya mitihani hiyo yanayoonyesha asilimia 60
ya wanafunzi, wamepata ziro.
Mushi alisema sababu kuu ya matokeo mabaya ni udhaifu wa serikali
kushindwa kusimamia majukumu yake na kuchukulia kila jambo kwa wepesi.
“Hii serikali dhaifu ya CCM, mwaka 2006 ilisema lengo ni kufikia
ufaulu wa asilimia 70 wakati huo tukiwa katika asilima 34 leo hata hiyo
haipo sasa tunakwenda wapi na jeshi hili kubwa ambalo litakuwa
haliajiriki tena kwa kukosa hata sifa ya kuwa na vyeti vya sekondari!?”
alisema Mushi.
Katika hatua nyingine kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi waliofeli kutasababisha shule na vyuo vingi kukosa wanafunzi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kuzungumza na wataalamu wa
elimu unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanafunzi watashindwa kujiunga na
masomo ya juu pamoja na vyuo.
VIA
http://freemedia.co.tz
Post a Comment