Loading...

Lwakatare aumiza vichwa polisi • Wakwama kumfikisha kortini, mawakili wachachamaa




                    Wilfred Lwakatare

JESHI la Polisi nchini limekwama kumfikisha mahakamani Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuendelea na uchunguzi.
Kukwama kwa jeshi hilo ambalo jana lilitangaza kumfikisha Lwakatare katika Mahakama ya Kisutu, kumezua tafrani kutoka kwa mawakili wake wakidai kuwa hatua hiyo ni kinyume na sheria, ni unyanyasaji na ukandamizaji wa haki za binadamu.
Mmoja wa mawakili wake, Nyaronyo Kicheere alisema pamoja na polisi kumshikilia Lwakatare, wamemuweka katika mahabusu isiyokidhi hali ya afya ya kiongozi huyo, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
“Hali ya Lwakatare ni mbaya, anaumwa kisukari, anahitaji chakula kila baada ya saa nne, na kupata huduma ya haja ndogo mara kwa mara, lakini amewekwa katika chumba ambacho hakina huduma ya choo ingawa vinapatikana pale polisi.
“Ni kinyume cha sheria kumweka mtu polisi saa zote hizo, na wanafanya vile utadhani huyu wameshampata na hatia. Hatuwezi kuhamishia familia yake pale ili wampatie chakula kila mara,” alisema.
Aliongeza kuwa juzi alipotolewa kutoka katika chumba alipohifadhiwa alikuwa na hali mbaya kiasi cha kushindwa kuongea au kusimama kwa kuwa alikuwa hajala kwa muda mrefu kulingana na hali ya ugonjwa wake.
“Mtu wa aina hii sio wa kuwekwa mahabusu muda mrefu, kwanza Lwakatare sio mtu wa kutoroka, ukiachilia mbali suala la kisheria linalowalazimisha polisi kumpeleka mahakamani ndani ya saa 24,” alisema Kicheere.
Akizungumza kwa niaba ya mawakili wanaomtetea Lwakatare nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kiongozi wa jopo hilo, Tundu Lissu alisema kitendo cha polisi kutomfikisha mkurugenzi huyo mahakamani kama ilivyopangwa mapema jana ni ukatili.
“Kama wanaendelea na upelelezi wangemfungulia mashtaka hata ya kuokoteza tu ili apate dhamana ya mahakama kuliko kumtesa hivi,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa polisi wameendelea kujichanganya na kutupiana mpira kuhusiana na sakata hilo, jambo linalowafanya wajiulize kulikoni.
Alifafanua kuwa alipoongea na mtu aliyeambiwa ndiye anayekaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Hezron Kigondo, alikana kutohusika na jambo hilo.
“Mimi nilipomuuliza alisema ahusiki kabisa na suala la kumshikilia Lwakatare isipokuwa anasimamia upelelezi wa suala lake tu, hivyo nimuulize Isaya Mungulu,” alisema Lissu.
Kwamba alipozungumza na Mungulu naye alisema yuko Mtwara, na kwamba hajui kabisa jambo hilo, akaomba ampigie tena baada ya nusu saa.
Lissu anasema alipompigia tena Mungulu alisema “Jeshi la Polisi litamshikilia Lwakatare hadi siku ya Jumatatu ndio watamfikisha mahakamani” kauli iliyozusha zogo kubwa kwa mawakili hao.
Mawakili hao walisema majibu ya maofisa hao wa polisi yanadhihirisha namna walivyoshindwa kubaini kosa linalomkabili Lwakatare.
Walisema huo ni ushahidi mwingine kuwa Jeshi la Polisi linajifanya liko juu ya sheria na kwamba lina uwezo wa kunyanyasa watu kadiri linavyotaka.
Lissu alisema ikifika Jumatatu polisi hawajamfikisha Lwakatare mahakamani, basi wataongea na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, na baada ya hapo watapeleka ujumbe kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi halifuati sheria.
Mbali na Lissu na Nyaronyo, wakili mwingine Professa Abdallah Safari alimtaka IGP Mwema aache kujiaibisha, kwani na yeye ni mwanasheria, ni wakili kama wao, hivyo anajua kuwa ni kinyume na sheria kumshikilia mtuhumiwa kwa muda unaozidi saa 24.
Lwakatare anatetewa na jopo la mawakili wanne; Lissu, Prof. Abdallah Safari, Kicheere na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Peter Kibatala.
Wabunge waliofika mahakamani jana kumwekea dhamana Lwakatare ni Israel Natse (Karatu), Suzan Kiwanga na Naomi Kaihula (viti maalumu), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa mjini) na Ezekiah Wenje (Nyamagana).
Utata wa video
Katika hatua nyingine, wakili Kicheere amezungumzia kile alichokiita utata wa video iliyokamatwa na Jeshi la Polisi akisema ina walakini mwingi.
Kicheere alisema video hiyo ambayo mteja wake alioneshwa ina kasoro nyingi na tofauti na ile iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.
“Mkanda uliopo polisi kuna sehemu sauti inaongea, lakini picha imefunga mdomo, na kuna sehemu midomo inafunguliwa hakuna sauti inayosikika. Huo mkanda ni wa kutengeneza kabisa,” alisema.
Alidai kushangazwa na habari zilizotolewa na gazeti moja la kila siku zikidai kuwa Lwakatare katika video hiyo amemtaja mhariri mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msaky, jambo alilosema ni uzushi.
“Katika mkanda huo, ulioko polisi hakuna sehemu hata moja alipotajwa Msaky, sasa kama sio kuandaa mazingira ya kuhalalisha ajenda zao ni nini?
“Sisi tunawasubiri wamlete Lwakatare mahakamani ili tujue waliohusika kuutengeneza mkanda huo,” alisema.
Kupekuliwa Bukoba
Wakati hayo yakijiri, taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zimesema kuwa kuna mpango wa kumpeleka kiongozi huyo nyumbani kwake mjini Bukoba kwa upekuzi zaidi, baada ya kufanya hivyo mara mbili katika makazi yake Kimara King’ongo jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alipohojiwa ikiwa hawaoni kama wanavunja sheria kwa kutomfikisha Lwakatare mahakamani alisema; “sisi bado tunaendelea na utaratibu wa upepelezi, hatujavunja sheria, tukikamilisha upelelezi tutamfikisha mahakamani haraka, siwezi kuzungumza mengi maana nitakuwa navujisha upelelezi.”
Kurekodi sauti bandia
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za wanasayansi, kuna uwezekano wa kurekodi sauti bandia, huku video za mara kwa mara zilizorekodi sauti za viongozi kadhaa maarufu duniani, akiwemo Osama bin Laden zikitolewa mfano.
Wanasema sauti isiyokuwa na ubora pamoja na kuwepo kwa mabadiliko mbalimbali ya sauti zisizohitajika ni dhahiri kuwa kanda za aina hiyo ni feki.
“Nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikigundua teknolojia ambazo zinaweza kubadilisha sauti kwa haraka sana,” anasema mwanasaikolojia Jan van Santen.
Mwanasaikolojia huyo anasema kutokana na sababu kuwa teknolojia ya kubadilisha sauti imekuwa ikiongezeka na kukua kwa kasi sana, ni vigumu kugundua kama sauti zinazorekodiwa ni halisi ama ni bandia.
Anaeleza kuwa njia mojawapo inayotumika kwa sasa kuweza kugundua uhalisi wa sauti hiyo ni kwa kuangalia alama maalumu zilizopo kwenye vyombo vya kurekodia ambazo nazo pia hutegemea ni njia gani ya ubadilishwaji wa sauti imetumika.
Dk. Alexander Kain ambaye ni miongoni mwa watafiti kutoka katika shule ya OGI, kituo kinachoshughulikia uelewa wa lugha ya matamshi, amegundua Mimics kuwa ni njia mojawapo inayoweza kuiga sauti halisi kwa kutumia kigezo cha sifa pekee iliyoko kwenye koromeo, njia ya matamshi pamoja na muziki maalumu na ‘biti’ yake.
Anaeleza kuwa wanasayansi wengi wamegundua njia mbalimbali za kubadilisha sauti ambazo ni rahisi sana kutumia na vinapatikana kirahisi kwa kila mmoja kupitia vitabu pamoja na mtandao wa Internet.
Ili kutumia na kufanikisha Mimic ni lazima sauti halisi iliyorekodiwa ya mtu husika itambuliwe kwanza na baadaye atafutwe mtu wa tofauti mwenye sauti sawa na mtu wa kwanza ambaye atasoma ama kusema maneno yaleyale aliyosema mtu huyo bila kukosea.
Anasema kuwa ni lazima mtu huyo afanye kazi hiyo kwa uhakika kiasi kwamba ni vigumu kwa mtu yeyote kutambua ama kutofautisha kama sauti hiyo ni ya watu wawili tofauti.

VIA: http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=46773



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top