Loading...

BAADHI YA WABUNGE WAMEENDELEA KUJADILI KESI INAYOMKABILI WILFRED LWAKATARE LICHA YA KESI HIYO KUWA MAHAKAMANI

makinda
Bila kujali kwamba kesi ya Ugaidi na kula njama ya kutenda kosa la jinai inayomkabili Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), WILFRED LWAKATARE na mwenzake LUDOVICK RWEZAURA kuwa mahakamani, baadhi ya Wabunge wameendelea kulijadili suala hilo na kubainisha mkakati huo ulivyopangwa.

MWIGULU NCHEMBA Mbunge wa Iramba Magharibi ndiye aliyefungua pazia la malumbano hayo akidai kujibu Hotuba ya Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayomtaka akamatwe kwa ugaidi na kusema anao ushahidi wa kutosha na yuko tayari kwenda popote kuthibitisha jambo hilo.

Kambi ya Upinzani ikiwakilishwa na Mbunge wa Mbulu MUSTAPHA AKUNAI inaoneshwa kuchukizwa na kauli hiyo na kupelekea kuomba muongozo wa Spika ili hoja hiyo isijadiliwe Bungeni.

Hata hivyo kwa kutoridhishwa na kauli hiyo ya kiti cha Spika, Mbunge wa Singida Mashariki TUNDU LISSU anairudisha tena hoja hiyo iliyopo mahakamani kwa madai kwamba mkakati mzima umepangwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara MWIGULU NCHEMBA.

Baadae Mbunge wa Viti Maalum ANNA ABDALAH nae akaingilia kati na kuomba muongozo hali inayompelekea Spika MAKINDA kuwataka wabunge kuachana na jambo hilo ili wajadili masula yanayowahusu wananchi kwa ujumla.

Mbali na hayo bunge limeendelea na majadiliano ya Makadirio na Matumizi ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Matumizi ya Bunge na kuahirishwa hadi Juni 15 saa tatu asubuhi mwaka huu.




Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top