Loading...

KWA WALIMU WOTE

SHAIRI HILI LINAITWA "KWA WALIMU WOTE" LIMEANDIKWA NA PROFESA KEZILAHABI MWALIMU NA RAFIKI YANGU.

sikilizeni wimbo huu:
nilipokuwa mtoto niliitwa
Chacha

kwa matamshi yangu ya sasa
nilipokuwa kijana niliitwa Chaupele
nilipokuwa mtu mzima niliitwa manywele
nilipokuwa mwalimu niliitwa BURE.

Huu utakuwa wimbo wako
utakapostaafu urudipo nyumbani
umelewa kangara na nyayo zako
zikishindwa kulenga njia nyembamba vijijini.
utakuwa kichekesho kwa watoto
watapokuita, ticha! popote upitapo.

kumbuka mwalimu utakapostaafu.
mijusi watataga mayai ndani ya viatu
vyako vilivyokwisha visigino
na ndani ya sidiria chakavu
zilizoshikizwa kamba kwa pini.
mende watazaliana ndani ya chupa tupu
za marashi na za bia.

na manyigu yatajenga ndani ya kofia
zilizosahaulika kutani.
utakapokufa nge watazaliana
chini ya jiwe juu ya kaburi lako,
na mlevi fulani akipita atapenga
na kupangusa vidole kwenye jiwe pweke.
mwanzo na mwisho wako ndio huo.

lakini wakati ungali hai
unaweza kubadili mkondo wa maji.
lakini kwanza tuzungumze. wewe na mimi.
acha mioyo yetu izungumze.
baada ya kunyanyaswa
na kisha nusu mshahara,

utafundisha tena nyimbo za kusifu viongozi?
utafundisha tena ngonjera?
utapeleka tena wanafunzi asubuhi
wakajipange barabarani kusubiri
mgeni afikaye saa kumi, an apitapo
apunga tu mkono kuwatia kichaa cha shangwe
na huku nyuma mwasambaa na njaa?

tazama rundo la daftari mezani
utalimaliza kwa mshahara wa mkia wa mbuzi?
tuzungumze. ninyi na mimi.
acha mioyo yetu izungumze.
mkiwa waoga na kujikunya kama jongoo
mtawekwa kwenye kijiti na kutupwa
nje ya ua, na ndani mtawaacha
wacheza ngoma wakitunga nyimbo mpya.

sikilizeni walimu.
anzeni kufundisha hesabu mpya:
mjinga mmoja kujumlisha wezi ishirini
ni sawa na sifuri.
fundisheni historia mpya:
hapo zamani za sasa
hapakuwa na serikali.

sikilizeni kwa makini.
umoja hatuna:
twasambaratika kama nyumbu.
tulichonacho ni woga,
na kinachotuangusha ni unafiki.
lakini tusikate tamaa kama mbuni.
tukiupata umoja bado tunayo silaha.
KURA.
SHAIRI HILI LINAPATIKANA KATIKA KITABU CHA "DHIFA"



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top