Na Alexander Joseph
NIUNGANE na Watanzania wote wenye mapenzi mema kuwapa pole ndugu zetu wa mkoani Ruvuma hususan mji wa Songea, ambao ama wamepoteza ndugu zao kutokana na vurugu hizi, wamejeruhiwa au wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Waliofikishwa katika vyombo vya sheria sina wasiwasi nao sana maana najua sheria ni msumeno unaokata nyuma na mbele.
Baada ya vurugu zilizotokea Februari 22, mwaka huu siku ya Jumatano mjini Songea na kusababisha vifo vya watu wanne waliokuwa wakiandamana kupinga mauaji ya hovyo hovyo yanayofanywa na watu wasiojulikana yakihusishwa na imani za kishirikina, kumekuwa na lawama nyingi dhidi ya polisi, bila hata watu kuangalia upande mwingine wa shilingi kwa kuwa tu, walitumia risasi za moto na kusababisha vifo. Watu sasa wanaangalia na kushughulikia walipoangukia, badala ya kushughulikia walipojikwaa.
Hao sasa, ni marehemu waliokufa kwa mtutu wa bunduki ambao pesa yao ya kodi ndiyo iliyoununua na pesa hiyo hiyo, ndiyo inayowalipa mshahara waliowafyatulia risasi; askari polisi wa mkooa wa Ruvuma. Nashukuru kusikia kwamba, walau askari wanne wanashikiliwa kutokana na tukio hilo huku uchunguzi ukiwa unaendelea.
Jumatano hiyo ya Februari 22, mwaka huu, wananchi wa Songea walipoupata mwili wa mtu mwingine anayesadikiwa kuuawa kwa imani za kishirikina, ndipo mioyo ikawalipuka. Wakasema “tumechoka.” Hapo hapo, wakapanga na kuanzisha maandamano ya ghafla kupeleka kilio chao kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Si wanawake, si wanaume; si vijana, si wazee; si waenda kwa miguu, si wapanda pikipiki maarufu mkoani humo kama yeboyebo; ari inazidi kupanda na kuanza kukimbia huku na huko wakiimba na kila mmoja akisema lake.
Haya ni maandamano yaliyolipuka ghafla, hayana kiongozi (msemaji) maalumu, hayakutolewa taarifa mahali popote wala kupata kibali na hasahasa ulinzi wa polisi; wanakimbia kimbia mamia kwa mamia mara ofisi za polisi mara ofisi za RC.
Wananchi hao wanataka haki yao ya kusikilizwa iheshimiwe na kuzingatiwa. Hata hivyo, nani msemaji au watesema wote kama nyimbo za walevi; au mwenye sauti kubwa na kali ndiye anasikika? Katika mazingira kama hayo matokeo ni nini?
Ingawa nawapongeza kwa uamuzi wa kufanya maandamano kufikisha kilio cha kero hii, na ingawa nawapongeza wote waliotoa “kauli” zao mintarafu suala hili, bado najiona kudaiwa kusema ukweli maana, dawa ya deni ni kulipa.
Ninasema hivi nikiamini kabisa kuwa Wanasongea waliamua kufanya maandamano ambayo ni haki yao kwa sababu isingewezekana waendelee kuuawa, huku wamekaa kimya, lakini si siri walisahau kuwa haki siku zote huenda sambamba na wajibu.
Kwa mujibu wa taratibu nijuavyo mimi, mikusanyiko na hasahasa maandamano, siku zote huhitaji umakini na hasa hasa usalama na amani kwa wote waandamanaji na hata wasio waandamanaji hivyo, wajibu wa kuvijulisha vyombo vya usalama kama polisi ni wenye umuhimu usiopimika.
Nasema hivyo kwani imebainika kuwa, waandamanaji hawakuwa wametoa taarifa polisi, wala kupata kibali chochote ili kupata ulinzi. Hii ni kwa kuwa maandamano yale hayakuwa yameandaliwa kwa misingi ya utulivu na umakini, bali yaliibuka kwa jazba baada ya kubaini kuwapo mwili wa mtu mwingine aliyeuawa usiku wa kuamkia siku hiyo na viungo vyake kunyofolewa.
Kwa mantiki hiyo, naamini yeyote mwenye busara na umakini wa kutosha, kama yeye ndiye angekuwa amepewa jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, asingeruhusu maandamano ya mfumo huo yaendelee na hasa ikizingatiwa kuwa mara nyingi penye msafara wa mamba, kenge hawakosekani.
Hii ni kwa kuwa penye wengi, pana mengi na mara nyingi hata wanasaikolojia wanasema, watu huenenda tofauti na kawaida yao wanapokuwa katika kundi la watu na kwamba mtu unayemheshimu kwa busara zake, anaweza kukengeuka na kufanya mambo ambayo katu asingeweza kuyafanya akiwa nyumbani kwake, kazini kwake au akiwa peke yake.
Kwa msingi huo, suala hili la maandamano ya Songea na matokeo yake, ninaamini kwamba wananchi walihitaji kuwa na ulinzi wa polisi. Hili lilikuwa ni suala la muhimu na la kipekee na hii ni kutokana na ukweli kuwa, katika mazingira hayo ya imani za kishirikina, mazingira ya mauaji, usishangae watu wakaanza kutuhumiana wenyewe kwa wenyewe na kushikana uchawi, jambo linaloweza kuzua machafuko au mauaji zaidi.
Hivi hapo hakuna haja ya kuwa na ulinzi wa polisi? Katika hali hiyo, ndiyo maana kwa mang’amuzi yangu, suala la vurugu za Songea Watanzania wasilichukue kwa mtindo wa ushabiki wala kufuata mkumbo; lazima liangaliwe kwa mapana na marefu yake.
Ifahamike kuwa, sheria za nchi zinalenga kumfanya kila mmoja apate haki yake, lakini pia atimize wajibu wake wa kutovuruga haki za wengine.
Hivyo, ingawa naungana nao kwani hata siku moja siwezi kufurahia wala kubariki mtu yeyote kuuawa, niseme wazi tu kwamba, waandamanaji wa Songea hawakutimiza wajibu wa kutoa taarifa ili kuimarisha usalama wakati wa maandamano kwa kuwa hayakuwa yameandaliwa na kwamba, yaliibuka tu, kama nyuki jambo ambalo kama lingeachwa, lingeweza “kumwaga damu nyingi” ya waliomo na hata wasiokuwamo.
Kwa msingi huo kisingekuwa kitendo cha busara kusikia kuwa madhara fulani yametokea kwa kuwa polisi wameacha maandamano yasiyo na uongozi wala kibali, eti tu kwa sababu yameibuka kwa kile wasomi wakiitacho mob psychology; kwamba wamewaachia mamia kwa mamia ya wananchi; kila mmoja na wazo au tatizo lake kichwani, waandamane wanavyotaka na tena bila kiongozi au msemaji anayefahamika.
Eti waachiwe waandamane kwa hali ile bila ulinzi wala uangalizi kwamba wakimaliza kufanya kila mmoja alilokusudia watatawanyika wenyewe! Nani anayejua kuwa ndani ya dhamira ya kila mwandamanaji kulikuwa na ajenda gani?
Si siri, endapio polisi wangepumbazika na kuachia maandamano hayo yasiyo na kiongozi, msemaji wala mwelekeo maalumu, bali kukimbia kimbia huku na huko huku wengine wakionesha mbwembwe za kuendesha pikipiki (yeboyebo) ni wazi hapa kila mmoja hata mtoto angelilaumu Jeshi la Polisi na kuliona kama Mfalme Juha na hivyo, Jeshi la Polisi lingepaswa kuwajibika.
Kama hivyo ndivyo, kwanini polisi wasiingilie kutawanya maandamano na mkusanyiko huo usiokuwa na “definition” yaani maelezo ili wananchi wafuate kwanza taratibu za kisheria na kiusalama ili kwamba, hata wapewe ulinzi?
Kwanini mara kadhaa polisi wakitimiza wajibu wao, wanawekewa vikwazo na wasipofanya hivyo wanalaumiwa? Kuna ajenda gani inayosukwa dhidi ya polisi au ndiyo tabia iliyojengeka katika jamii hasa kujifanya tunajua na kukosoa kila kitu bila kupima uzito na madhara yake?
Mbona polisi wetu badala ya kuwatia moyo tunawakatisha tamaa kwa kuwawekea vikwazo, ikiwa ni pamoja na kuwashambulia kwa silaha mbalimbali za jadi hususan mawe? Wengine wanabeza mawe; mawe, nani alisema jiwe sio silaha inayoweza kuua au kudhuru? Tumewafanya askari polisi mithili ya ubwabwa, juu moto chini moto; kwamba wakifanya, kosa, wasipofanya kosa!
Sheria na kanuni zinazoliongoza Jeshi la Polisi zinamruhusu askari polisi katika mazingira fulani, atumie silaha kali ili kujilinda na hata kulinda wengine sambamba na kulinda mali. Ndiyo maana ningependa tugeuze lawama na kuelekeza nguvu zetu katika kutoa elimu kwa jamii, ili kila mmoja atambue haki na wajibu wake katika kuzuia matumizi ya nguvu dhidi yake katika kumshurutisha atii sheria tulizojiwekea zituongoze.
Kama tunataka nchi yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani na usalama, tunapaswa kuwa mstari wa mbele kufundishana njia za kuwasilisha kero ambazo hazituingizi katika kuvunja sheria, amani na usalama wa jamii nzima. Kwangu mimi, kuendelea kuwalaumu Polisi waliotimiza wajibu wao baada ya wahusika kujiandalia mazingira ya taratibu za kisheria ili nguvu itumike dhidi yao ni sawa kusaka panya vichakani, wakati kabatini wamo.
Ipo haja ya jeshi hilo kuendesha uchunguzi na kuweka mitego ya kina na ya muda mrefu dhidi ya wachochezi wanaosababisha mihemko katika jamii inayosababisha hasara na madhara kwa watu.
Wachochezi wapo na matamko yao yanajulikana, wafuasi wao katika ngazi ya chini wanatumika sana kuchochea uasi hata katika mambo madogo madogo, ambayo yangemalizwa katika ngazi ya awali ya mamlaka za kiserikali lakini yanakuzwa hadi kusababisha hasara kubwa.
Nijuavyo mimi, katika matukio kama hayo, polisi hawafiki tu, na kuanza kupiga, bali hutoa maonyo kadhaa ya wazi tena kwa ishara za wazi na sauti kubwa. Kama hivyo ndivyo, kwa nini onyo la kwanza lipuuzwe; onyo la pili lipuuzwe;… huku ni kulichokoza jeshi letu wenyewe na kujaribu kuliwekea vidole machoni na haya, ni matunda ya mob psychology yanayopandikizwa na wanasiasa wanaotamani uongozi wa juu wa nchi. Je, hao watawezaje kuongoza kwa amani wakati wameingia kwa kuvuruga amani na usalama wa jamii?
Kadhalika, wananchi yaani raia, wafike mahali sasa watambue umuhimu wa kujenga urafiki na majeshi yetu; na hivyo, raia na majeshi kama polisi, wasionane wabaya wala maadui, bali wadau wa amani na usalama wetu sote. Jamii itambue kuwa, Tanzania ni yetu sote na hivyo, hatuna budi kushirikiana kuijenga katika nyanja za amani, usalama na maendeleo mengine yakiwamo ya kiuchumi.
Ifahamike kuwa, bila taarifa sahihi za raia wema, polisi hawawezi kufanya kazi zao sawia kwa kuwa kwanza, ni wachache na pia, wao si malaika wa kujua kila kitu na kumjua kila mtu; mwema au mwovu. Kadhalika, bila polisi kufanya kazi zao sawia, raia wema watasita kutoa taarifa za kuzuia uhalifu na kuwakamata wahalifu na hivyo, uhalifu utazidi kutanda.
Ikumbukwe pia kuwa kwa nchi kama Tanzania yetu, jukumu la ulinzi wa nchi ni la kila mmoja na hasa mzalendo wa kweli. Jukumu hili, linapaswa kuanzia kwa mtu mwenyewe katika eneo lake kwa KUTAFUTA na KUBAINI vyanzo vya uhalifu na wahalifu wenyewe na kisha, kutoa taarifa sahihi kwa polisi ili hatua za kisheria zifuate.
Hili, ndilo jukumu la wote; kujenga utamaduni wa kila raia; mwananchi na mzalendo kutafuta taarifa za uhalifu yakiwamo mauaji hayo yanayokera Songea, kabla haujatendeka, badala ya kusubiri matukio yatokee.
Ni muhimu wakaepuka kutumia matukio ya kihalifu na maafa kama fursa ya uwekezaji na mtaji wa kujipatia umaarufu wa kisiasa na mambo ya kitaalamu na kiutendaji, wawaachie wataalamu na watendaji wao, ili wao wajikite katika kutunga sera safi zinazotekelezeka.
CHANZO TANZANIA DAIMA LA FEBRUARI 29,2,2012
Habari hii nimeitoa facebook bofya hapa
Post a Comment