WAKUU wa Wilaya wapya wametakiwa kufanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa ili kuweza kuleta matumaini mapya kwa wananchi ambao wanahangaika na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu katika viwanja vya ikulu wakati wa kuwaapisha wakuu wa Wilaya wapya wa tano walioteuliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kuongoza wilaya tano zilizopo mkoani Ruvuma ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Abdula Lutavi, na Mkuu wa Wilaya Mpya ya Nyasa Erenest Kahindi
Mwambungu alisema kuwa wananchi wengi wamekata tamaa kutokana na kupanda kwa gharama za maisha kunakosababishwa na mambo mbalimbali na kufanya familia nyingi zikose furaha stahiki
Alisema kuwa muda umefika sasa kwa viongozi kujishusha na kufanya kazi kwa ushirikiano na wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika jamii zao ili kuweza kuleta matumaini na nuru mpya
“ Mmeapa kwa nguvu kubwa kupitia vitabu vitakatifu hivyo ni vema mkatekeleza majukumu yenu bila kupokea rushwa, upendeleo, chuki na vitendo vingine ambavyo havimpendezi mungu na vimekatazwa katika sheria, kanuni, taratibu na maadili ya kazi” alisema Mwambungu
Alieleza kuwa kuapa kwenu leo ni kukubali dhamana mliyopewa hivyo mnapaswa kwenda kwenye wilaya zenu mkawe karibu na wananchi ambao wanazifahamu kero zinazowakabili ambazo wanataka zitatuliwe kwa ukamilifu
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma Dkt Matenus Kapinga alisema kuwa amewataka wakuu hao wapya kuheshimu wananchi wanaowaongoza na kufanya kazi zenye tija na kuacha kujifanya miungu watu kwa kutenda mambo ya ubabe
Naye shehe wa Mkoa wa Ruvuma Abdalah Hasan Amir Mkoyogole alisema kuwa wakuu wa Wilaya wamechaguliwa na Mungu hivyo wanapaswa kwenda kufanya kazi kwenye wilaya zao walizopangiwa na kupunguza kufanya siasa na kuepukana na makundi ambayo yana athiri amani na utulivu.
Post a Comment