Loading...

Ruvuma: wanafunzi zaidi ya 500 wanasomea katika vibanda vya nyasi

          Chanzo: fikrapevu.com
    WANAFUNZI wa shule tatu za msingi zaidi ya 500 katika kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanasomea kwenye madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi.
    Uchunguzi uliofanywa katika shule tatu kati ya saba zilizopo kwenye kata hiyo ambayo ipo mjini Namtumbo umebaini kuwa  katika shule ya msingi Rwinga wanafunzi  296  wanasomea kwenye vibanda vya miti vilivyoezekwa kwa nyasi .
    Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Onesmo Mbawala alisema idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo wanasomea katika vibanda vya nyasi kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa vyumba 12 vya kusomea ambapo vyumba vilivyopo ni vinne tu na kwamba shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975 ina jumla ya wanafunzi 592.
wanafunzi-rwinga-school
Wanafunzi wa darasa la awali wapatao 92 shule ya msingi Rwinga wilayani Namtumbo wakiwa darasani na mwalimu wao

Katika shule ya msingi Selous jumla ya wanafunzi 108 wa madarasa ya tano na sita wanasoma kwenye vibanda vya nyasi hali ambayo walimu wanasema inachangia kushusha taaluma kwa wanafunzi.
wanafunzi-selous-school
Wanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Selous wilayani Namtumbo wakiwa darasani
Mwalimu  wa taaluma katika shule hiyo Sheweji Simba  alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ina jumla ya wanafunzi 477 huku ikiwa na vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba nane hali ambayo imesababisha baadhi ya wanafunzi kusomea kwenye vibanda vya nyasi .
Katika shule ya msingi Mkapa ambayo imepewa jina la aliyewahi kuwa kiongozi mkuu wa nchi  Rais mstaafu Benjamin Mkapa pia kuna wanafunzi  wanaosomea kwenye vibanda viwili vya nyasi  kwa kuwa shule hiyo ina vyumba vinne tu kati ya mahitaji ya vyumba nane.
wanafunzi-mkapa-school
Wanafunzi wa shule ya msingi Mkapa wilayani Namtumbo wakiwa darasani na mwalimu wao
Mkuu wa shule hiyo Hans Mwailima alisema shule hiyo yenye wanafunzi 306 madarasa matatu yanasomea katika chumba kimoja  ambapo kuanzia darasa la tatu hadi la sita  wanasomea kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu.
“Unajua wanafunzi wana tabia ya kutaniana hivyo endapo darasa moja wakisoma kwenye vibanda vya nyasi kila siku wenzao wanawatania hivyo kukata tamaa na wengine kuwa watoro hivyo tumeamua wote wawe wanasoma kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu ili kujenga mvuto wa mazingira ya kusomea’’, alisema.
Mratibu elimu kata ya Rwinga Thomas Komba amekiri shule  tatu kati ya saba katika kata yake ambazo ni Rwinga, Mkapa na Selous wanafunzi kusomea katika vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi na kusisitiza kuwa shule za Minazini, Kidagulo, Migelegele na Mandepwende ndizo shule pekee katika kata hiyo ambazo hazina vyumba vya madarasa vilivyoezekwa kwa nyasi.
“Shule zangu  tatu za Rwinga,Mkapa na Selous katika kata yangu zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa hali ni mbaya tunafanya jitihada za kuhamasisha jamii ili waweze kujitolea kufyatua tofali kuzichoma kwa kushirikiana na serikali  ili kupata vyumba zaidi na kumaliza kero hii ya aibu’’, alisisitiza.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Kasimu Ntara alidai kuwa kuwa kuwepo kwa madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi katika wilaya hiyo kunatokana na kuanzishwa shule nyingi za msingi.
“Mpango wa uboreshaji wa elimu ya msingi MEM nchini ulisababisha kuanzishwa kwa shule nyingi hivyo  baada ya kuondoka kwa MMEM serikali imeshindwa kumudu ujenzi wa vyumba vya madarasa jitihada zinaendelea kufanyika kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa’’, alisisitiza.
Habari hii imeandikwa na Albano Midelo, FikraPevu – RuvumaPost a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top