Loading...

ALAT RUVUMA YAWEKA AZIMIO LA KILIMO CHA MAZAO MBADALA

Na Steven Agustino,Tunduru
KIKAO cha jumuiya za serikali za mitaa (ALAT) mkoa wa Ruvuma kimeazimia kuanzisha na kuendeleza kilimo cha mazao mbadala katika mkoa wa Ruvuma ambayo ni pamoja na korosho,karanga,mihogo na kahawa badala ya kuendeleza zaidi kilimo cha mahindi pekee.
Azimio hilo limepitishwa na wajumbe wa jumuiya hiyo katika mkutano mkuu uliofanyika wilayani Tunduru ambao ulitanguliwa na ziara ya mafunzo kwa wajumbe kutembelea kituo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara zikiwa ni juhudi za wajumbe hao kupata ufahamu zaidi wa shughuli za uzalishaji bora wa zao la korosho.

Aidha wakiwa katika ziara hiyo ya mafunzo katika kituo hicho wajumbe hao pamoja na kujifunza namna ya uzalishaji bora wa korosho pia walielimishwa namna ya kulima kilimo bora cha karanga,Ufuta, na muhogo mazao ambayo yanastawi pia mkoani Ruvuma ambako kunalimwa mahindi kwa kiasi kikubwa na kahawa ambalo ni zao la biashara linalolimwa zaidi katika wilaya ya Mbinga nalo limewekewa mikakati zaidi ya kuhakikisha wilaya zote za mkoa wa Ruvuma zinalima.

Akizungumza wakati akitoa mafunzo hayo kwa wajumbe Afisa utafiti wa kilimo wa kituo cha Naliendele Ramadhan Bashiru alisema kuwa uamuzi wa wajumbe hao kutoka mkoani Ruvuma kufika katika kituo hicho kwa ajili ya kujifunza ni ishara kuwa wamedhamiria kuinua kiwango cha wakulima wa mkoa wa Ruvuma kwani watalima kilimo bora chenye tija kwao na taifa kwa ujumla.

 Bashiru aliwaeleza wajumbe hao kuwa mbali na kituo hicho kufanya utafiti wa mazao mbali mbali pia kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wakulima kulingana na mahitaji yao ingawa wananchi wanaokizunguka kituo hicho bado hawajaonyesha mwamko chanya wa kutaka kujifunza kilimo bora na uzalishaji bora wa mazao mbali mbali ambayo ni rahisi kwa wakulima wadogo wadogo.

Aidha Bashiru alitoa wito kwa mikoa mingine kuiga mfano wa mkoa wa Ruvuma kufika kwenye kituo hicho kwa ajili ya kujifunza na kupata mbegu bora za mazao mbali mbali ili kutekeleza kauli mbiu ya kilimo kwa vitendo kwa sababu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa.

Awali akifungua mkutano huo  Mkuu wa Wilaya ya Tunduru  Bakari Nalicho pamoja na kutoa hamasa kwa viongozi wa Jumuiya hiyo kuhamasisha uzalishaji wa mazao hayo kwa wakulima wao pia aliwaomba viongozi wa Bodi ya Korosho na Mfuko unaosimamia uzalishaji wa zao hilo kuhakikisha wanatafuta soko la uhakika na kuuza korosho zilizo kwama katika maghala ya vyama vya ushirika Wilayani humo pamoja na kujenga tabia ya kupeleka madawa ya kupulizi mikorosho ya wakulima kwa wakati.

Aidha DC, Nalicho aliwahamasisha wajumbe hao kupia halmashauri zao kuhamasisha wananchi kukopa matrekta yaliyoletwa Mkoani humo, kutoa elimu  juu ya ukusanyaji wa kodi kutoka kwa wafanyabiashara, kubuni mbinu mpya za ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyazo visivyo wa kwaza wananchi na akatumia nafasi hiyo kuwakumbusha watendaji katika halmashauri hizo kusimamia mapato hayo ili yatumike katika uboreshaji wa maisha ya wananchi kupitia huduma muhimu za Maji,Afya, Elimu,Kilimo kwa maana ya Pembejeo na miradi ya ufugaji.

Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho aliwataka wajumbe waliofika kwenye kituo hicho kuwa mabalozi kwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwatumia wataalamu wa kilimo waliopo katika halmashauri zao ili kuufanya mkoa wa Ruvuma kuwa na mazao mbali mbali ya biashara na chakula.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama alisema kuwa ziara hiyo ya wajumbe kwenye kituo hicho ni chachu kubwa ya kuufanya mkoa wa Ruvuma kuwa kioo cha uzalishaji wa mazao hayo ambayo yakizalishwa kwa kuzingatia utaalamu yatainua uchumi wa mkulima na taifa kwa ujumla.



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top