Loading...
WALALAMIKIA UBOVU WA MIUNDOMBINU YA STENDI SONGEA
Na Gideon Mwakanosya, Songea
BAADHI ya wakazi wa Halmashauri ya manispaa ya songea wakiwemo abiria wameulalamikia uongozi wa manispaa hiyo kwa kushindwa kukarabati miundombinu ya kituo kikuu cha mabasi cha mjini Songea na kusababisha adha kubwa abilia na baadhi ya magari kukwama hasa wakati wa kipindi cha masika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana abiria hao wameeleza kuwa hali ya kituo cha mabasi cha Songea kwa muda mrefu kina hali mbaya ambapo kwa kipindi cha mvua kunakuwa na mashimo ambayo hujaa maji na kusababisha magari ya kubeba abiria kukwama katikati ya kituo hicho
Wameeleza zaidi kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakiulalamikia uongozi wa halmashauri hiyo kuhusu kuwepo miundombinu mibovu kwenye kituo hicho bila kuwepo mafanikio jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa songea wakiwemo abiria .
Mmoja kati ya wananchi hao John Komba mkazi wa Mbinga alisema kuwa hali ya kituo hicho ni mbaya sana hasa kwa wakati huu wa kiangazi ambapo kumekuwepo na vumbi ambalo limeonekana kuwa ni kero kwa watu wanaoingia na kutoka kwenye kituo hicho kwa miguu hivyo ameuomba uongozi wa Halmashauri kuona umuhimu wa kumwagia maji kwa lengo la kupunguza kero ya vumbi lililokithiri
Naye Sebastian Nombo mkazi wa kijiji cha Kihangimauka kilichopo wilayani Mbinga alisema kuwa ipo aja kwa uongozi wa Halmashauri ya manispaa ya Songea wakiwemo madiwani kuona umuhimu kwenda kujifunza jinsi mbinu wanazozitumia kuboresha miundombinu mbalimbali ya barabara za halmashauri ya wilaya ya mbinga pamoja na mikakati waliyonayo ya kukijenga kituo kipya cha kisasa cha mabasi cha mjini mbinga.
Nombo alieleza zaidi kuwa inasikitishwa sana kuona hali mbaya ya miundombinu ya kituo kikuu cha mabasi cha mjini songea ambacho kipo makao makuu ya mkoa wa Ruvuma hivyo ni vyema uongozi wa halmashauri hiyo ukachukua hatua za haraka kukifanyia ukarabati kituo hicho cha mabasi ambacho kinaonekana kuwa ni kero kwa wakazi wa Songea.
Mmoja wa wamiliki wa magari wa kusafirisha abiria kati ya Songea na Dar es salaam ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema kuwa ushuru wa magari yakiwemo mabasi yanayoingia kwenye kituo kikuu cha mabasi cha manispaa hiyo umekuwa ukitolewa kila siku lakini Halmashauri hiyo imeshindwa kukifanyia matengenezo jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kwa abiria hasa wakati mvua zinaponyesha kunakuwa na madimbwi ya maji ambayo husababisha magari kupita kwa taabu katika kituo hicho.
Mmoja wa wafanyakazi wa mabasi ya SAJDA yanayosafirisha abiria kutoka songea kwenda Mbinga Oddo Nchimbi alisema kuwa magari madogo yanayoingia kwenye kituo hicho (TAXI) Halmashauri hiyo imekuwa ikiwatoza shilingi 500 kila siku wakati magari yenye uzito wa tan 1 nusu hadi tani 7 kila anapoingia kwenye kituo hicho hutozwa shilingi 1000 kila siku na magari makubwa yakiwemo ya kusafirisha abiria kuanzia tani saba na kuendelea kila yanapoingia hutozwa shilingi 2000 kila siku lakini hali ya kituo hicho cha mabasi ni mbaya.
Alisema kuwa abiria wanayoijua stendi hiyo hasa wakati wa masika wamekuwa hawapandii mabasi ndani ya kituo na badala yake wamekuwa wanapandia nje ya kituo kwa kukwepa adha ya tope .
Kwa upande wake kaimu wa mkurugenzi wa manispaa hiyo Naftari Saiyori alipoulizwa kuhusiana na kero hiyo alikiri hali ya kituo cha mabasi ni mbaya lakini alieleza kuwa halmashauri yake inampango kabambe wa kujenga kituo kikuu cha mabasi cha kisasa huko katika eneo la msamala ambapo alidai kuwa mpango huo uko katika hatua ya upembuzi yakinifu na kwamba kwa hivi sasa kutakuwa na gari la maji litakuwa linapita kwa wiki mara tatu kwa lengo ya kupunguza kero ya vumbi iliypo kwenye kituo hicho.
1 comments:
Nimeguswa na habari hii maana hali hii imekuwa kwa muda mrefu sana. Kama mwandishi na wachache hapo juu walivyosema ni kituo kikuu cha mji wa Songea na ni ndipo usafiri unapoanzia na kuishia. Kujenga kituo msamala haitakkuwa nzuri kwa vile kituo cha basi kinatakiwa kiwe mjini ili iwe rahisi kwa wengi...
ReplyPost a Comment