Loading...

AHUKUMIWA JELA MIAKA 15

JOSEPH KOMBA (20) mkazi wa eneo la Madizini kata ya Lizaboni manispaa ya Songea mkoa wa Ruvuma amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kuvunja nyumba na kuiba mali mbalimbali zenye thamani ya shilingi 2,914,000 (milioni mbili laki tisa na elfu kumi na nne) mali ya Happiness Yaunde mkazi wa majengo Songea.

Akisoma hukumu hiyo ambayo ilisomwa zaidi ya dakika arobaini na tano, hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Ruvuma Kasmilly Mwalunyungu alisema kuwa mahakama imeridhika kabisa na ushahidi uliotelewa na upande wa mashtaka ambao ulithibitisha kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo huku akijua anavunja sheria.

Mwalunyungu alifafanua zaidi kuwa mshitakiwa Joseph Komba bila halali alitenda makosa hayo akiwa na lengo la kuiba hivyo mahakama imemtia hatiani na kumpa nafasi ya kujitetea ambapo mshitakiwa Komba aliiomba mahakama imfikirie kumpa adhabu ndogo kwa vile kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa lingine, pia ana mke mmoja na mtoto mmoja ambao wote wanamtegemea.

Hata hivyo mwendesha mashtaka wakili wa serikali wa ofisi ya mwanasheria wa serikali kanda ya Songea  Tulibake Juntwa kabla ya utetezi wa mshitakiwa aliiomba mahakama impe adhabu kali mshitakiwa kwakuwa anaonekana kuwa ni mzoefu wa uhalifu.

Kwa upande wake hakimu mkazo wa mahakama hiyo Mwalunyungu alisema kuwa mahakama imeona kuwa mshitakiwa anamakosa hivyo inahukumu kifungo cha miaka 10 kwa kosa la kwanza na kosa la pili mshitakiwa anahukumiwa kwenda jela miaka 5, ambapo adhabu zote zinakwenda pamoja.

Awali mwendesha mashitaka ambaye ni wakili wa serikali Tulibake Juntwa alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Joseph Komba mnamo februeri 19 mwaka jana majira ya saa za usiku huko katika eneo la Majengo Songea Mjini bila halali na huku akijua anavunja sheria alivunja nyumba na kuingia kwenye chumba anachoishi Happiness Yaunde na baada ya kuingia alifanikiwa kuiba Tevisheni moja aina ya Panasonic, radio kaseti moja aina ya Panasonic, godoro, begi, deki moja, shuka mbili, CD za muziki, pasi moja, suruali moja, zulia na mapazia mawili mawili. Mali yote ina thamani ya 2914000/=
Hata hivyo mshitakiwa alikana mashitaka.
MWISHO



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top