JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
DODOMA
ALHAMISI DESEMBA 14, 2012.
Wakazi wa Dodoma wametakiwa
kuondokana na dhana potofu inayoenezwa na kundi la kundi la lamba lamba ya
kuwaaminisha wananchi hususani wa vijijini kuwa wanauwezo wa kuondoa na kufichua
uchawi na washirikina ambao wanadai wanavuta mali za watu wengine kwao na kuwafanya
matajiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Bw. David Misime ameeleza hayo
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ya kutangaza vita dhidi ya kundi la
matapeli la lamba lamba lililovamia na kufanya shughuli zake mjini humo.
Akizungumzia kundi hilo
Kamanda David Misime alisema kuwa ni kundi la matapeli ambalo limeundwa na
wahalifu kwa lengo la kujihusisha na uhalifu wa
utapeli na ulaghai kwa wananchi hususani wa vijijini, ili kujipatia
mali, fedha na mifugo ya aina mbalimbali toka kwa wanavijiji.
“Kundi hili ni mkusanyiko
wa watu wa jamii tofauti ambao wanatoka maeneo ya Rufiji, Pwani, Tanga na
Morogoro ambao wamekuja kuivamia jamii ya watu Dodoma ambayo nayo ina mila na
desturi zake katika mambo ya jadi.” Alielezea Bw. David Misime
Alisema kwamba kundi hilo
limekuwa likitumia mtindo wa kujifanya kuwa wao ni waganga wa tiba za jadi
kwamba wana uwezo wa kutoa vitu vya kichawi
katika majumba ya watu, sehemu za biashara na pia kufichua wachawi, vitu ambavyo hawana uwezo navyo.
Kamanda Misime alieleza
kuwa ili mtu akubalike kuwa ni mganga wa tiba za jadi ni lazima afahamike
katika eneo analofanyia shughuli zake hizo kuanzia uongozi wa ngazi ya chini hadi wa juu wa serikali na awe na
kibali cha kuendesha tiba hizo kisheria kitu ambacho kundi la lamba lamba
hawakidhi matakwa hayo.
Aliongeza kuwa Mganga wa jadi kwa asili yake hatakiwi kufanya
kazi zake kwa kuita watu ni wachawi bali
anapaswa kutoa tiba na kinga kwa kutumia miti shamba kulingana na uwezo wake,
na sio wanachofanya hao wanaojiita lambalamba.
Kamanda Misime alisema
kundi la lambalamba kwa kushirikiana na
washirika wao, huwa wanapandikiza vitu kwenye nyumba, mashamba au sehemu za biashara
za walengwa nyakati za usiku na baada ya kufanya hivyo ndipo wanaondoka na
kundi la watu na kwenda kutoa vitu ambavyo walishavipandikiza kabla.
Alieleza kwamba madhara
yanabaki kwa anayefanyiwa hivyo kwa kudhalilika yeye na familia yake kuwa ni mchawi na kibaya zaidi hulazimishwa kutoa
kiasi cha fedha na mifugo kama adhabu na
kutishiwa wasithubutu kwenda kutoa taarifa Polisi.
“Hili ni kosa la jinai na
ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu, hatuwezi kuvumilia na kuwaacha wananchi wenzetu
kuendelea kupoteza fedha na mali zao kwa kuwanufaisha hao matapeli.” Alisistiza
Bw. David Misime
Aidha aliongeza kwamba zipo
taarifa kuwa lambalamba hao wanapofika vijijini hutafutiwa wanawake wa
kuwapikia na kisha kuwastarehesha kitu ambacho ni unyanyasaji wa kijinsia na
jambo la hatari ambalo linachangia kuenea kwa magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Bw. David Misime alisema
hayo yanayofanyika ni utapeli mkubwa uliobuniwa na watu hao wa kujipatia fedha
na ni jambo linalodhalilisha, linalojenga chuki, na uchochezi ndani ya
jamii na
kuhatarisha usalama, utulivu na
amani pamoja na kuathiri afya za
wanawake na jamii nzima kwa ujumla.
Kamanda
David Misime ametoa
wito kwa wananchi kwa kupitia
mkakati wa Polisi Jamii na dhana ya utii wa sheria kwa hiari kushirikiana
kwa pamoja na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za watu hao ili kuutokomeza uhalifu huu ili jamii
iendelee kubaki salama na inayoweza kufanya
shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
MWISHO:
CONTACT:
POLISI
MKOA WA DODOMA
DAWATI
LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone: 0715 006523, Luppy Kung’alo – Mrakibu
msaidizi wa Polisi (ASP)
Phone: 0712
360203, Silyvester Onesmo – Police
Konstebo (PC)
Post a Comment