Loading...

WAZIRI MKUU AAHIDI TREKTA KWA VIJANA ILUNDE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI  


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kutoa trekta moja kwa ajili ya kikundi cha vijana katika kata ya Ilunde ili waweze kuondokana na kilimo cha jembe la mkono na waboreshe uchumi wa eneo hilo.

Ametoa ahadi hiyo leo (Ijumaa, Desemba 14, 2012), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ilunde kwenye uwanja wa shule ya msingi Ilunde katika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi alisema atawapatia
trekta hilo kama mkopo ili nao wakirudisha trekta jingine, liweze kukopeshwa kwa kikundi kingine. “Hapa naanzisha ‘Kopa trekta lipa trekta’. Litakuja likiwa na jembe lake pamoja na harrow,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

“Ni lazima tuondokane na kilimo cha jembe la mkono kwa sababu hakina tija na zaidi nasisistiza kuondokana na kilimo cha matuta kwa sababu kinatumia nguvu nyingi na kupoteza eneo kubwa ambalo lingetumika kupanda mazao,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alielezwa matatizo yanayowakabili wakazi hao yakiwemo ubovu wa barabara ya kutoka Inyonga (km. 60) na ukosefu wa wauguzi wa kike kwa ajili ya akinamama wajawazito. Pia waliomba kupatiwa minara wa mawasiliano ya simu kwa sababu wanapotaka kupiga simu, wanalazimika kupanda mti mmoja tu ambao uko km.12 kutoka kijijini hapo.

Akijibu maombi yao, Waziri Mkuu aliwaita Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda na Mhandisi wa Wilaya hiyo ili watoe maelezo kwa wananchi hao. Kuhusu wauguzi, mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Emmanuel Kamgobe alisema wanashugulikia suala hilo.

Naye Mhandisi wa wilaya hiyo, Injinia Godfrey Majuto alisema katika mwaka ujao wa fedha, wilaya imetenga sh. Milioni 60 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Inyonga – Ilunde na wameainisha kilometa tano ambazo ni korofi zaidi.

Mchana huu Waziri Mkuu alifungua bweni la wasichana kwenye shule ya sekondari ya Ilela ambalo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 52. Ujenzi wa bweni hilo umegharimu sh. milioni 36/-.

Naye mbunge wa viti maalum mkoa wa Katavi, Dk. Pudenciana Kikwembe ameahidi kutoa vyandarua, mashuka na mablanketi kwa ajili ya wanafunzi wote 52 wa kwanza watakaolala kwenye bweni hilo.

Kesho (Jumamosi, Desemba 15, 2012) atakagua kituo cha afya cha Inyonga na kuzindua mradi wa madawati kwa shule za tarafa ya Inyonga.Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top