Rais wa Madagascar, Mheshimiwa Andry Rajoelina amewasili mjini Dar Es Salaam mchana wa leo, Ijumaa, Desemba 14 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini.
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mjini Dar Es Salaam ambako ndege iliyomleta
Rais Rajoelina ilitua saa sita na dakika 45 mchana, amelakiwa na mwenyeji wake,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais
Kikwete na Rais Rajoelina wamekula chakula cha mchana na wanatarajiwa kuanza
mazungumzo rasmi baadaye leo.
Rais
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) amepewa jukumu na viongozi
wenzake ndani ya Jumuiya hiyo kukutana na viongozi wa Madagascar kuwaelezea
maamuzi ya mkutano wa viongozi hao wa SADC uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini
Dar Es Salaam.
Rais
Kikwete tayari amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Marc Ravalomanana,
kiongozi wa zamani wa Madagascar aliyeondolewa madarakani na Rajoelina.
Kwenye
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, mwanzoni mwa
wiki hii, Mheshimiwa Ravalomanana alithibitisha kuwa amekubaliana na maamuzi ya
viongozi wa SADC.
Post a Comment