JESHI la polisi mkoani Ruvuma linawashikilia watu wawili akiwemo Diwani wa kata ya Ruchiri (CCM ) Wilaya ya Namtumbo kwa tuhuma za kuwapiga wauguzi wawili wa zahanati ya kanisa katoriki jimbo kuu la songea parokia ya Namtumbo kigango cha Chengena sehemu mbalimbali za mwili kwa mawe, fimbo na mateke na kumsababishia muuguzi mmoja kati yao kulazwa katika hospitali ya serikali ya mkoa.
Akizungumza na NIPASHE jana mchana ofisini kwake kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Mrakibu mwandamizi wa polisi George Chiposi aliwataja watuhumiwa kuwa ni Zacharia Mapunda maarufu kwa jina la chepa (46) ambaye ni diwani wa kata ya Ruchiri na mtoto wake Andrew Mapunda (24) mkazi wa kijiji cha Chengena.
Aliwataja wauguzi waliojeruhiwa kwa kupigwa ni Emmacurata Komba (29) na Rose komba (35) ambao wote ni wauguzi wa zahanati wa kanisa katoliki jimbo kuu la songea parokia ya Namtumbo kigango cha Chengena.
Kaimu kamanda Chiposi alisema kuwa tukio hilo lilitokea januari 13 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi huko katika kijiji cha Chengena ambako inadaiwa Emmacurata na Rose walipigwa na Diwani wa kata ya Ruchiri ambaye alishilikiana na mtoto wake Andrew.
Alifafanua zaidi kuwa inadaiwa kiini cha ugomvi kuwa ni kwamba awali Emmacurata alikuwa ni mpangaji wa nyumba inayomilikiwa na mapunda maarufu kwa jina la Chepa ambaye ni diwani wa kata hiyo na kutokana na juhudi zake nyumba hiyo aliikarabati kwa kuisakafia na kuweka milango pamoja na madirisha mapya.
Alibainisha zaidi kuwa pamoja na jitihada hizo alizozifanya Emmacurata inadaiwa watoto wa diwani hawakutaka mpangaji huyo aendelee kuishi kwenye nyumba ya baba yao kwa madai kuwa kwa muda mrefu alikuwa halipi kodi ya pango la nyumba.
Alisema kutokana na mvutano huo Emmacurata alifikia huamuzi
wa kuama nyumba hiyo na kwenda kuamia nyumba nyingine ambayo ilikuwa
bado haijakamilika kwa kutokuwa na madirisha na milango hivyo aliamua
kwenda kwenye nyumba aliyokuwa akiishi awali kungoa madirisha na milango ili akaweke kwenye nyumba nyingine ambayo alitarajiya kuamia ndipo ugomvi ulianza kwa diwani wa kata hiyo Mapunda kwa kushilikiana na mtoto wake Andrew walimpiga Emmacurata kwa mawe, mateke na ngumi sehemu mbalimbali za mwili.
Kaimu kamanda Chiposi alifafanua zaidi kuwa wakati ugomvi huo ukiendelea ghafla Rose alifika kwenye eneo la tukio na alikwenda kuamua ugomvi naye alipigwa jiwe kichwani ambaye alipelekwa kwenye hospitali ya serikali ya Wilaya ya namtumbo ambako alitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Alisema baadae hali yake ilibadilika ghafla kuwa mbaya kisha alikimbizwa katika hospitali ya serikali ya mkoa ambako amelazwa anaendelea kupata matibabu katika wodi grade namba 2.
Alisema polisi inafanya upelelezi kuhusiana na tukio hio na kwamba utakapokamilika watuhumiwa wanatarajiwa kufikisha mahakamani kujibu mashitaka yanayo wakabili.
Hata hivyo mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Dr. Benedicto Ngaiza alipohojiwa na NIPASHE kwa njia simu kuhusiana na majeruhi wa tukio hilo alisema kuwa Rose Komba aliletwa hospitalini hapo januari 13 mwaka huu majira ya saa za usiku akiwa na hali mbaya lakini kwa hivi sasa anaendelea vizuri licha ya kuwa bado hajaruhusiwa kurudi nyumbani.
Post a Comment