MKAZI mmoja Samwel  Liungi (37) wa kijiji cha Suluti kilichopo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma amekufa papo hapo baada ya kufukiwa na kifusi wakati anachimba madini aina ya Gamarine kijijini hapo na polisi inawahoji watu watatu akiwemo mmiliki wa mgodi huo Godwin Sanga (45) mkazi wa kijiji hicho.

Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimethibitishwa na Kaimu Kamanda wa polisi wa Mkoa  wa Ruvuma Mrakibu Mwandamizi wa Polisi George Chiposi, zimesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 30 mwaka huu majira ya saa 7.30 mchana huko katika kijiji cha Suluti kilichopo nje kidogo ya makao makuu ya Wilaya ya Namtumbo.

Kaimu kamanda Chiposi amebainisha kuwa inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, huko katika kijiji cha suluti kwenye eneo la machimbo madogo ya madini aina ya gamarine yaliyopo kijijini hapo Liungi alifukiwa na kifusi ndani ya shimo alimokuwa anachimba madini hayo na kufa papo hapo.

Alisema kuwa mgodi huo, unaomilikiwa na Sanga, ulikuwa na wachimbaji madini watatu ambao aliwataja kuwa ni Abi Rashid (37), Bakari Hashim (25) na Liungi ambaye kwa sasa ni marehemu na kwamba chanzo cha kubomoka mgodi huo bado hakijafahamika.

Hata hivyo, kaimu kamanda Chiposi alieleza kuwa kufuatia kutokea kwa tukio hilo, jeshi la polisi linawashikilia watu watatu akiwemo mmiliki wa mgodi huo ambao wanaendelea kuhojiwa ili kubaini chanzo cha tukio hilo.