KARANI mmoja
wa mahakama ya mkoa wa Ruvuma amepandishwa kizimbani katika mahakama ya
hakimu mkazi wa mkoa wa Ruvuma kwa tuhuma za kuiba nyara za serikali zilizokuwa
zimehifadhiwa kwenye stoo ya kuhifadhia vilelezo zenye thamani ya shilingi
962,500.
Ilidaiwa na upande wa
mashtaka na mwendesha mashtaka wa serikali ambaye ni mwanasheria wa ofisi ya
mwanasheria Kanda ya Songea Tulibake Juntwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama
ya mkoa wa Ruvuma Casmil Mwalunyungu kuwa Sadick A. Makundi (49) ambaye ni
karani wa mahakama ya mkoa wa Ruvuma anashtakiwa kuwa akiwa mtunza stoo ya
mahakama aliiba vipande viine kati ya vipande nane vya meno ya tembo.
Juntwa alibainisha
zaidi mahakamani hapo kuwa tukio hilo lilitokea
kati ya Mei 25 mwaka jana na Januari 16 mwaka huu katika majira yasiyofahamika
kwenye ofisi ya mahakama ya mkoa wa Ruvuma wakati akiwa mtunza funguo za stoo
hiyo.
Alisema kuwa vipande
hivyo vya meno ya tembo vilipokelewa mahakamani kama kielelezo cha kesi ya
uhujumu uchumi namba 9 ya mwaka 2007 ambayo iliisha Mei 25 mwaka jana ambapo
mahakama ilikuwa imeamuru nyara hizo za serikali ziuzwe kwa kupitia idara ya
wanyamapori kisha fedha hizo ziingizwe serikalini.
Aidha, mwanasheria huyo
wa serikali Juntwa alibainisha zaidi mahakamani hapo kuwa maafisa wa idara ya
wanyamapori walipomfuata Makundi ambaye kwa sasa ni mshitakiwa hakutaka kutoa
nyara hizo za serikali hadi alipoamriwa tena na hakimu mkadhi mfawidhi wa
mahakama ya mkoa wa Ruvuma Frank Mahimbali na kukuta meno 4 kati ya meno 8
hayapo kwenye stoo hiyo wakati funguo za stoo hiyo alikuwa anazo mshitakiwa
Makundi.
Hata hivyo, mshitakiwa
Makundi baada ya kusomewa shitaka hilo amekana na yuko rumande baada ya kukosa
mtu wa kumdhamini hadi Februari 18 mwaka huu kesi itakapotajwa tena na kwamba
kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa na hakimu mkazi mfawizi wa mahakama ya wilaya
ya Mbinga kwa madai kuwa mshitakiwa ni mtumishi wa mahakama ya mkoa hivyo ni
lazima kesi hiyo isikilizwe na hakimu wa mahakama nyingine ili kuepuka
malalamiko.
Post a Comment