Loading...

Makinda atumika kumfuta Sitta

  Spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Anne Makinda

Na Josephat Isango
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai, wanasemekana kutumiwa na maadui wa demokrasia na mafisadi kummaliza kabisa aliyekuwa Spika wa Bunge hilo, Samuel Sitta na kundi lake.

Habari za kuaminika kutoka vyanzo mbalimbali zimebainisha kuwa kile kilichotokea bungeni na kusimamiwa kikamilifu na Makinda ulikuwa ni utekelezaji wa matakwa ya wanasiasa na viongozi kadhaa wenye nguvu za fedha ambao waliumizwa vibaya na aina ya uongozi na maamuzi ya Sitta alipokuwa akikalia kiti hicho.

Inadaiwa kwamba mbali na kumkomoa, Makinda pia ameelekezwa kuhakikisha kuwa Sitta anamalizwa kisiasa, kwa kuwasulubu pia wabunge waliokuwa wakimuunga mkono, wakiwamo wale wa vyama vya upinzani hususan wa CHADEMA.

Moja ya chanzo chetu cha habari kimesema kuwa wanasiasa hao wakiwamo watendaji kadhaa wa serikali, walichukizwa na msimamo wa Sitta, hasa kusimamia ukweli na haki, na kuonekana kuwapendelea zaidi wabunge wa upinzani kuliko wale wa CCM.

Katika mkakati huo, iliamriwa kuwa nguvu zote alizotumia Sitta kuisulubu serikali na wanasiasa walioguswa masilahi yao, zivunjwe, likiwamo suala la kuunda na kuunganisha kamati ya hesabu za mashirika ya umma, na ya hesabu za serikali kuwa pamoja, kisha kuhakikisha inaongozwa na mbunge kutoka chama tawala.

Mbali na mipango hiyo, chanzo chetu kimesema kuwa mabadiliko hayo ya kamati yamefanywa kutokana na hofu ya kuumbuka kwa serikali kutokana na matumizi mabaya ya fedha, ikiwa kamati hizo zitaendelea kuwa chini ya wapinzani.

Katika mpango huo, Naibu Spika Ndugai, amejikuta akilazimika kukubaliana na maagizo ya mkuu wake wa kazi, licha ya ukweli kwamba ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati maalumu iliyoundwa katika Bunge la Tisa lililoongozwa na Sitta, ikiwa na lengo la kuleta mfumo mzuri wa utendaji wa Bunge, ikiwa ni pamoja na kurejesha hadhi yake ya kuiwajibisha serikali.

Ndugai katika kukamilisha azima ya Sitta, alilazimika na kamati yake iliyoundwa na wabunge wengine, Dk. Harrison Mwakyembe, Nimrod Mkono, Beatrice Shelukindo, Dk. Willibrod Slaa na Hamadi Rashid Mohamed, ilifanya ziara katika Bunge la Kenya, Uganda, India, Mauritius na Zimbabwe.

Kutokana na ziara hizo za mafunzo, Ndugai na kamati yake walipendekeza kutungwa kwa mambo yatakayolifanya Bunge lisimamie masilahi ya taifa badala ya vyama, vikao vyake kuoneshwa wazi kwa njia ya runinga ili wananchi waone na ripoti za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali zijadiliwe na Bunge pamoja na kuondoa miswada yoyote iliyokuwa inaletwa kwa dharura bungeni.

Ni kamati ya Ndugai ndiyo ilipendekeza kuwa Kamati ya Mashirika ya Umma, (POAC), Kamati ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ziongozwe na upinzani ili kuongeza uwajibikaji wa serikali kwa Bunge.

Mbunge mmoja wa CCM ambaye amekuwa bungeni kwa muda mrefu (jina linahifadhiwa) alikiri kusikitishwa na uamuzi wa Spika Makinda, na kuonesha hofu ya kuvunjika kwa heshima na hadhi ya Bunge.

“Inasikitisha sana, maana sasa tunaelekea kuvunja hadhi ya Bunge na kulinda uozo wa serikali.
“Katika Bunge la Tisa, Sitta alijitahidi kuwa jasiri, kutopindisha ukweli ili kuilinda serikali, na alizielewa vizuri kanuni hasa ile ya 8 inayosema: “Hata kama Spika ametoka katika chama fulani anapaswa atende haki kwa pande zote,” alisema mbunge huyo.

Mbunge huyo alisema vurugu zilizotokea bungeni zilitokana na maamuzi mabaya ya kiti cha Spika, kinyume kabisa cha hotuba yake ya kwanza alipochaguliwa kushika wadhifa huo ya kuliunganisha Bunge kuwa moja.

Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu, mmoja wa wajumbe wa iliyokuwa kamati ya Ndugai, Nimrodi Mkono, alisema hawezi kusema lolote kuhusiana na kuondolewa kwa kamati hizo, ingawa alikiri kuwa walichokishauri na kukubaliwa na Bunge kilikuwa cha maana na manufaa kwa taifa.

Kuhusiana na vurugu zilizotokea, Mkono alisema kelele za wapinzani zilikuwa sahihi hasa baada ya kuona kuwa wanaonewa, kutokana na uchache wao, hivyo kulazimika kupiga kelele ili hoja zao zisikiwe na Watanzania.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, alishangaa kuunganishwa kwa Kamati ya Mashirika ya Umma pamoja na ile ya Hesabu za Serikali, huku akihoji kama Spika na wabunge wa CCM wapo tayari kuwa na mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kutoka upinzani.

Akihojiwa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, kiongozi mmoja mashuhuri hapa nchini, amelaani aliouita uendeshaji mbovu wa shughuli za Bunge, na kuongeza kuwa kumetokana na udhaifu wa serikali yenye wabunge wasiojali masilahi ya taifa.

Alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa kauli ya hivi karibuni ya Makinda wakati akitoa maoni mbele ya wajumbe wa kamati ya kukusanya maoni ya Katiba, ya kutaka Spika atoke nje ya chama, ilionesha kuwa huenda hata yeye analazimika kutekeleza maagizo na maelekezo ya chama na serikali yake hata kama hayataki.

CHANZO:   http://www.freemedia.co.tz



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top