Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya,
imeamua kuwa rais mteule Uhuru Kenyatta atasalia kuwa rais mpya wa Kenya baada
ya kusema kuwa uchaguzi ulifanywa kwa njia huru na ya haki.
Uchaguzi wenyewe ulifanyika tarehe
nne mwezi Machi, ambapo hesabu ya kura ilimpa ushindi Kenyatta kwa zaidi ya
laki nane.
Rais wa mahakama hiyo jaji mkuu
Willy Mutunga alisema kuwa mahakama imekubali kwa kauli moja kuwa uchaguzi
ulifanywa kwa njia ya huru na wazi na kuwa Kenyatta na mgombea mwenza wake
walichaguliwa kihalali.
Uamuzi huu una maana kuwa Uhuru
Kenyatta ndiye ataapishwa kama rais mpya wa Kenya tarehe tisa mwezi ujao
Kesi hiyo iliwasilishwa katika
mahakama ya juu zaidi na mpinzani mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga baada ya
uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa Uhuru
alishinda uchaguzi kwa kumpiku Raila kwa asilimia 50.07 huku Raila akipata asilimia
43.28. Matokeo haya yalizuia kufanyika kwa duuru ya pili ya uchaguzi kwa kura
8,100.
Bwana Odinga aliishutumu tume huru
ya uchaguzi na mipaka kwa kuhujumu matokeo ya uchaguzi ili kumpa ushindi Uhuru
Kenyatta.
Uchaguzi wa urais, wabunge na
wajumbe wengine wa serikali, ulifanyika tarehe nne mwezi Machi, ukiwa wa kwanza
tangu uchaguzi uliokumbwa na ghasia mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu
zaidi ya elfu moja.
Bwana Kenyatta na mgombea mwenza
wake ,William Ruto,wanakabiliwa na kesi katika mahakama ya jinai kwa kuchochea
ghasia za mwaka 2007. Hata hivyo wamekanusha vikali mashtaka.
Mahakama ya juu zaidi inaweza
kuthibitisha ushindi wa Kenyatta au kuubatilisha uamuzi wa wakenya na hivyo
kuitisha uchaguzi mpya.
Vyovyote matokeo yatakavyokuwa kuna
wale watakaoghadhabika mno.
Rais anayeondoka mamlakani, Mwai
Kibaki amewataka wakenya kuwa watulivu na kukubali uamuzi wa mahakama lakini
wengi wanatagemea sana idara ya mahakama ambayo imekuwa na mageuzi makubwa na
ambayo sasa watu watu imani nayo.
Mawakili wa Odinga wanasema kuwa
kesi yao ilihusisha madai ya kuhujumu hesabu ya kura pamoja na matatizo ya
usajili wa wapiga kura na vile vile matatizo ya mitambo ya usajili wa wapiga
kura.
Mnamo Ijumaa mahakama ya juu zaidi
ilidurusu matokeo ya kura katika vituo 22 vya kupigia kura. Na pande zote mbili
zilisema matokeo yalithibitisha misimamo yao.
Kenyatta ameutaja uchaguzi huo kama
ishara ya kukuwa kwa demokrasia Kenya na ulifanywa kwa njia ya amani.
Tume ya uchaguzi, pia imesisitiza
kuwa uchaguzi ulikuwa huru licha ya hitilafu za kimitambo
Wachunguzi wa kimataifa nao walisema
kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na kuwa tume huru ya uchaguzi uliendesha
uchaguzi huo kwa uwazi.
Post a Comment