Loading...

Bungeni hakukaliki

Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla (kushoto), akiwasiliana na mwenzake wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga ndani ya Ukumbi wa Bunge Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Baadhi ya wabunge jana waliendelea kutumia fursa ya mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu kurushiana vijembe na maneno ya kuudhi mambo ambayo yalisababisha mivutano ya kikanuni, huku mmoja wao akionya kwamba ikiwa haki hiyo itaendelea bungeni hakutakalika.

Chimbuko la mivutano hiyo ni kauli zilizotolewa na Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Juma Nkamia ambaye alimjibu Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi kwamba “haongei na mbwa bali anazungumza na mwenye mbwa.”

Kadhalika Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliwapiga vijembe viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akisema kwamba kuna wabunge ambao wana “mimba zisizotarajiwa bungeni”.

Vijembe hivyo viliendelea jioni baada ya Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje kusema Serikali iliyopo madarakani haina uwezo, haina ujuzi na imepoteza imani ya watu kutokana na kushindwa kuwatatulia wananchi matatizo yaliyopo.


Naye Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa akieleza kuwa Serikali ina tatizo kwa kuwa kuna “akili ndogo inatawala vichwa vikubwa.”

Alitumia kifungu cha kitabu kitakatifu cha Biblia cha Mithali 27:22 kinachosema kuwa “mpumbavu ukimchukua ukimchanganya na ngano kwenye kinu atabaki na upumbavu wake.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Wenje na Msigwa walikiuka kanuni za Bunge kutokana na matamshi yao.

Naibu Spika, Ndugai alionya lugha hizo bungeni akiwasihi wabunge kuacha kutumia, kauli iliyoungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Anna Abdallah ambaye alieleza kukerwa na udhalilishaji wa wanawake bungeni.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Paulina Gekul akitumia Kanuni ya 68 (7) alikilaumu kiti cha Spika kwa kukaa kimya wakati wabunge wanatukana bungeni. “Kama hali hii itaendelea, humu ndani kutakuwa hakutawaliki,” alisema Gekul.

Pia Moses Machali (Kasulu Mjini -NCCR-Mageuzi) na Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF) waliomba mwongozo wa Spika wakitumia Kanuni ya 64 inayozuia lugha za kuudhi bungeni.


Lusinde alianza kuipiga vijembe hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na baadaye alidai kwamba wapo wabunge wenye mimba zisizotarajiwa ambao wanaharibu nchi.

“Ukiangalia kuna watu wanataka kuvuruga nchi wakati wana watoto wachanga. Mimi mtoto wangu wa mwisho ana miaka minane halafu Slaa (Dk Willibrod, Katibu Mkuu Chadema) wa kwake sijui ana wiki ngapi,” alisema Lusinde na kuongeza: “Hawa wapinzani tuachieni mimi na Mwigulu (Nchemba, Naibu Katibu Mkuu CCM).”

Baada ya Lusinde kumaliza Sakaya aliomba mwongozo wa Spika kuhusu utaratibu akitumia Kanuni ya 64(1) (g) , akisema kauli yake kwamba kuna wabunge ambao ni viongozi wana mimba zisizotarajiwa ni ya kuudhi.

Chanzo: Mwananchi



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top